Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Joshua: Yanga? Nyie acheni tu!

Oscar Joshua

Muktasari:

Kila mdau wa soka anatambua kuwa soka kwa sasa ni ajira iliyobadilisha asilimia kubwa ya maisha ya wachezaji wengi nchini kutoka kwenye utegemezi na kujiendeshea maisha yao na familia zao kupitia mchezo huo.

KIATU kinachobana akijuaye mvaaji! Huu ni msemo maarufu sawa na ule wa siri ya mtungi aijuaye kata.

Kila mdau wa soka anatambua kuwa soka kwa sasa ni ajira iliyobadilisha asilimia kubwa ya maisha ya wachezaji wengi nchini kutoka kwenye utegemezi na kujiendeshea maisha yao na familia zao kupitia mchezo huo.

Hata Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipotangaza kuanza kuwakata kodi wachezaji ilimaanisha kuwatambua kama wafanyakazi na mchangio wao mkubwa katika kulijenga taifa katika kuelekea kuwa na nguvu kubwa kiuchumi.

Mmoja ya wachezaji ambao wanalishukuru soka kumbadilishia maisha ni beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua ‘OJ’ ambaye anasema asingeweza kutua Jangwani kama sio kipaji cha soka kilichobebwa na miguu yake.

Joshua, mmoja wa mabeki waliojaliwa mwili jumba anasema soka limembadilishia maisha yake na kumpa maendeleo yake binafsi na familia yake na anashangaa wachezaji wasiotambua thamani ya miguu yao uwanjani.

Akizungumza na Mwanaspoti, beki huyo ambaye amepoteza namba kwa Haji Mwinyi Mngwali kuanzia Yanga mpaka timu ya taifa, Taifa Stars amefichua mambo mengi ikiwamo mbio za kuelekea kwenye usajili wa dirisha dogo.

Ukimya Jangwani

Joshua anaweka bayana kwamba licha ya kwamba anaozea kwenye benchi, lakini hawezi kukurupuka kutimka Jangwani kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo linaloendelea.

Anasema klabu ya Yanga aliyojiunga nayo mwaka 2010 akitokea Ruvu Shooting, ina siri nzito ya mafanikio yake kisoka na kimaisha na ni vigumu kuitema kienyeji, kwani bado anaamini anayo nafasi ya kuitumikia pale mwalimu atakapoamua kumpa nafasi tena.

“Nyuma ya mafanikio yangu kuna Yanga, klabu hii ina siri nzito kwangu kwani mali nilizonazo zimetokana na klabu hiyo ingawa sipendi kuweka wazi kila kitu,” anasema.

Joshua anasema klabu zinazoonekana tajiri katika Ligi Kuu Bara, ni Simba, Yanga, Azam FC, na amezizungumzia kwamba mchezaji makini anapoingia kuzitumikia timu hizo bila maisha yanabadilika hata heshima kwa jamii inajengeka.

“Kipato ambacho mchezaji wa Yanga, Simba na Azam FC, wanachopata si sawa na timu nyingine ambazo hazina uwezo ni kama zipo kwa ajili ya kukuza na kuviendeleza vipaji vya wachezaji ambao wanasajiliwa na klabu hizo,” anasema.

Ubora wa vigogo

Beki huyo anasema ubora wa klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam unatokana na kusaka makocha wa kimataifa pamoja na wachezaji wa kigeni ambao huwa mfano na changamoto kwa wazawa.

Anasema leo Donaldo Ngoma (Yanga), Kipre Tchetche (Azam) na Hamis Kiiza (Simba) ni mfano wa wachezaji wanaosaidia kuchochea ushindani katika soka la Tanzania kwa umahiri wao uwanjani na kusaidia wachezaji wa timu nyingine kujipanga kweli kweli.

“Ukiwa mchezaji makini, mapro hawa wanaweza kukufanya uwe mahiri zaidi kwani changamoto wanazokuta ni kubwa na kukuhamasisha,” anasema.

Ndoto

Joshua anasema imefika wakati sasa Yanga ikawa na wivu wa kimaendeleo kwani mtazamo wao uwe anga la kimataifa na si kuangalia mechi za ndani pekee jambo ambalo ni faida kwa wachezaji wake kujulikana katika mataifa mbalimbali kuliko kusubiria Taifa Stars tu.

Anasema Yanga ni klabu ilisajili wachezaji wenye ushindani wa namba , hivyo kuna changamoto kubwa, hivyo anasema anachukulia jambo hilo kama njia ya kutimiza ndoto zake za kufika mbali kisoka.

“Nina malengo yangu siwezi kuwa Yanga ilimradi tu, naamini kila kazi ina changamoto na ugumu wake, lakini kubwa najipanga ili kufika ninakokutamani hasa kimataifa,” anasema. Alifichua kuwa ni ngumu kuapa kwamba hawezi kuondoka Yanga kwani anajua kila jambo huwa na mwisho wake, lakini kwa sasa ni mapema kuweza kubashiri mpaka wakati ufike.

“Hakuna jambo lisilo na mwisho ila kwa kuwa mwisho wake bado sina muda wa kuzungumzia hilo kwa sasa nafanya yanayonihusu kupambana kwa ajili ya kuhakikisha Yanga, inatetea ubingwa msimu huu,” anasema.

Ushindani Bara

Joshua anasema kuwa Ligi Kuu ya msimu huu imekuwa na ushindani mkubwa, na imekuwa vigumu kuweza kutabiri mapema klabu gani itakayoibuka kuwa bingwa, kwani ndio kwanza mechi za raundi 10 tu kati ya 30 zimeshachezwa mpaka sasa.

“Yanga inayo nafasi kubwa, sawa na Azam, Simba, Mtibwa na hata Coastal Union inategemea wanarudi vipi kwenye duru jingine, ila ukweli ligi ni gumu mno,” anasema.

Joshua mwenye taaluma ya Uandishi wa Habari, anasema timu yoyote ambayo itarudi kwa kasi kubwa na kufanya kweli kwenye mechi zake ndiyo yenye nafasi ya ubingwa ikizingatiwa kuwa safari hii Ligi Kuu inatoa mwakilishi mmoja tu wa Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo ushindani ni mkubwa.

Utabiri wake

Beki huyo mwenyeji wa jiji la Mwanza aliyezaliwa miaka 29 iliyopita, hata hivyo anaipa nafasi kubwa Yanga kutetea taji kwa mara ya pili msimu huu, licha ya kuwepo mchuano mkali kati yao na Azam inayoongoza msimamo kwa sasa.