Job, Musonda watema cheche

YANGA jana ilitua nchini kutoka Kigali, Rwanda ilipoenda kuifumua Al Merrikh ya Sudan kwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mastaa wa timu hiyo akiwamo nahodha msaidizi, Dickson Job akitamba hata Dar, Wasudan hawachomoki.

Yanga ilipata ushindi huo wa kihistoria mbele ya Wasudan, kwani ilikuwa haijawahi kuifunga tangu zianze kukutana kwenye michuano ya CAF tangu 1973 na sasa inajiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga makundi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25 ilipocheza hatua hiyo mwaka 1998. Mara baada ya pambano hilo lililopigwa Uwanja wa Kigali Pele, Job alisema bado hawajamaliza kazi kwani wachezaji wa Yanga wamedhamiria kutotaka nyavu zao ziguswe na lengo kubwa ni kutinga makundi kwa kishindo na kuzima kelele kwamba hawana uwezo wa kufanya hivyo kutoka kwa mashabiki wa mtaa wa pili.     

Job alikiri mechi ilikuwa ngumu kutokana na aina ya uwanja, lakini walipambana kuhakikisha wanawapa raha mashabiki kaa walivyoahidi walipokuwa wanaoondoka Dar es Salaam na wanarudi nyumbani kumaliza kazi kwani Wasudani hawana chao mbele yao safari hii, licha ya kurudiana nao kwa tahadhari.

“Kushinda ugenini sio jambo rahisi, lakini sasa tunarudi Dar na wajue kabisa hatutawaacha salama, msimamo wetu ni kulinda nyavu zisiguswe na kama wachezaji tumejipanga kwa kujua mechi itakuwa ngumu kuliko ya hapa Kigali,” alisema Job aliyetua Jangwani akitokea Mtibwa Sugar, huku Kennedy Musonda akisema licha ya ushindi walioupata wamekutana na timu iliyowasoma kimbinu na kuziba njia zote.

“Akili kubwa imetumika hadi kupata matokeo haya ulikuwa ni mchezo mgumu tunashukuru tumefanikisha kwa kupata matokeo mazuri kazi iliyobaki ni uwanja wa nyumbani kwa dakika nyingine 90,” alisema Musonda na kuongeza;

“Baada ya dakika 45 za kwanza kocha alishtukia kitu kutoka kwa wapinzani jambo ambalo hata sisi kama wachezaji tuliliona na kumuahidi kocha kuwa tutafanya kila njia kuhakikisha tunapata matokeo na anashukuru baada ya kuingia kwake alitumia dakika 10 tu kufanya mambo kwa kufunga kwa kichwa,”  alisema Musonda, huku Stephane Aziz Ki akisema matokeo waliyopata ni zawadi kwa mashabiki waliojitokeza kwa wingi kuwapa sapoti huku akikiri kuwa ndio waliokuwa wanawapa nguvu zaidi kujiona kama walikuwa nyumbani.

“Ushindi ni kwa Watanzania na mashabiki wetu walioacha kazi zao na kuja kutupa sapoti Kigari ilikuwa kama Dar es Salaam tunaamini matokeo yamewapa nguvu ya kurudi nyumbani na furaha. Mchezo haukuwa rahisi ulikuwa mgumu tumepambana kuhakikisha tunapata matokeo ambayo yanaturudisha kiwanjani na nguvu zaidi dakika nyingine 90 za kusaka rekodi ya makundi.” alisema Aziz KI aliyeasisiti bao la pili la Yanga lililowekwa kimiani na mshambuliaji, Clement Mzize.