JKU yaiweka pabaya New City ZPL

Muktasari:
JKU ni miongoni mwa timu nane zilizoshiriki Kombe la Muungano mwaka huu na kufika fainali ikipoteza mbele ya Yanga kwa kufungwa bao 1-0 na leo imefanikiwa kuiondoa New City katika ZPL.
NEW City imejiweka pabaya kwenye Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) baada kuchezea kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Maafande ya JKU katika mechi iliyopigwa jana Jumatatu usiku.
Mechi hiyo iliyopigwa kuanzia saa 1:50 usiku ilichezwa kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Unguja na ilihitimisha rasmi safari ya New City inayoungana na Inter Zanzibar na Tekeleza zilizoaga ZPL wikiendi iliyopita.
Neva Kaboma alianza kuitibulia New City kwa kufunga bao la kwanza dakika ya nane kabla ya Ali Rashid kuongeza la pili dakika ya 18 na kufanya mabao hayo yadumu hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili Ali Rashid aliongeza bao la tatu dakika ya 70 na msumari wa mwisho katika jeneza la New City ipigiliwa na Tarik Mkonga dakika ya 88.
JKU ni miongoni mwa timu nane zilizoshiriki Kombe la Muungano mwaka huu na kushika nafasi ya pili kwa kufunga bao 1-0 katika fainali mbele ya Yanga iliyoibuka Bingwa.
Kwa sasa Ligi ikiingia raundi ya 24 na kusaliwa na mechi za raundi sita kufunga msimu, timu moja inatafutwa kukamilisha nne zinazotakiwa kushuka kwa mujibu wa taratibu za ZPL.