JKU yabeba tena Ngao ya Jamii Zenji

JKU Znz Pict
JKU Znz Pict

Muktasari:

  • Msimu uliopita JKU ilitwaa taji hilo kwa kuifunga KMKM kwa mabao 5-2 katika mechi iliyopigwa Septemba 9 na leo ikikutana tena na Chipukizi waliowavua taji la Kombe la Shirikisho (ZFF) kwa ushindi wa mezani, iliuanza msimu mpya wa 2024-2025 kwa ushindi huo wa mabao ya kila kipindi.

MABINGWA wa Ligi Kuu Zanzibar, JKU jioni ya leo Jumapili imefanikiwa kutetea tena Ngao ya Jamii baada ya kuinyoosha Chipukizi kwa mwaka 2-0 katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja.

Msimu uliopita JKU ilitwaa taji hilo kwa kuifunga KMKM kwa mabao 5-2 katika mechi iliyopigwa Septemba 9 na leo ikikutana tena na Chipukizi waliowavua taji la Kombe la Shirikisho (ZFF) kwa ushindi wa mezani, iliuanza msimu mpya wa 2024-2025 kwa ushindi huo wa mabao ya kila kipindi.

Katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho uliopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba mechi ilivunjika katika muda wa nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1 na dakika ya 103

JKU ilipata bao la pili lililokataliwa na mwamuzi akidai mfungaji ameotea na kuishia kufanyiwa fujo na pambano hilo kuivunjika na ZFF kuipa ushindi Chipukizi na klabu zote na mwamuzi kuadhibiwa.

Hata hivyo, Chipukizi licha ya kubeba ubingwa na tiketi ya mechi za Kombe la Shirikisho, timu hiyo ilishindwa kushiriki na nafasi yake kuchukuliwa na Uhamiaji na leo ilishuka Uwanja wa Amaan kutaka kuidhibitishia JKU haiwawezi, lakini ikakutana na aibu na kufumuliwa mabao hayo mawili.

Bao la kwanza la JKU liliwekwa kimiani dakika ya 9 tu ya mchezo na Ahmed Khamis bao lilidumu hadi wakati wa mapumziko licha ya Chipukizi kutoka Pemba kucharuka kutaka kulisawazisha bao hilo.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko na kuongeza kasi ya mchezo, lakini ni maafande wa JKU waliotakata tena kwa kuandika bao la pili dakika ya 82 kupitia kwa Koffi Hamza na kuifanya timu hiyo kubebea taji hilo la kwanza msimu huu ikitoka kung'olewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

JKU ilifungwa nje ndani na Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 9-1, kwani awali ililala 6-0 na ziliporudiana ililambwa mabao 3-1, mechi zote zikichezwa jijini Cairo, baada ya maafande hao kuamua kukubaliana na ombi la wapinzani wao la kutaka mchezo wa ugenini ukapigwe huko huko.

Uamuzi huo wa JKU kuhama uwanja wa nyumbani wa New Amaan na kwenda Cairo, ulifanywa pia na waliokuwa wawakilishi wengine wa visiwani, Uhamiaji iliyoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya ambapo mechi zote zilipigwa mjini Tripoli.

Kupigwa kwa mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ni ishara ya kufunguliwa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) itakayoanza wiki ijayo ikishirikisha jumla ya timu 16 zikiwamo nne mpya zilizopanda daraja ambazo ni Muembe Makumbi City, Inter Zanzibar, Junguni na Tekeleza.

Timu hizo zinachukua nafasi ya Ngome, Kundemba, Jamhuri na Maendeleo zilizoshuka daraja wakati JKU ndio waliotwaa ubingwa kwa kukusanya pointi 66 ikiitemesha KMKM taji ililokuwa ikilishikilia kwa misimu mitatu mfululizo.