JKT, Simba hivi ndivyo itakavyokuwa

KESHO Februari 15, 2024 JKT Tanzania itaikaribisha Simba katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Sa-laam, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara huku rekodi mpya ya viingilio uwanjani ikitarajiwa kuwekwa.

Mchezo huo wa 15 kwa timu zote utakuwa wa kwanza kwa msimu huu kuwa na kiingilio sawa kwa wote cha Sh10,000, ambapo ni tofauti na mechi nyingine.

Iko hivi. Kutokana na uwanja wa Isamuhyo kutokuwa na eneo au majukwaa ya kutosha kwa ajili ya mashabiki, JKT imetangaza kiingilio cha mchezo huo kitakuwa hicho kwa mtu mmoja ikiwa ni kwa watu wote bila kuweka matabaka kama inavyofanyika katika viwanja vingine vinavyohodhi mechi za Ligi Kuu.

Hivyo basi, wadau na mashabiki wa daraja la juu watalipa kiasi hicho cha pesa sambamba na wale wa madaraja ya chini ambao katika mechi nyingi za ligi msimu huu wamekuwa wakilipa kati ya Sh3,000 hadi Sh5,000 kutokana na utaratibu wa timu mwenyeji.

Mechi zinazohusisha timu za Simba, Yanga na Azam zimekuwa zikiongoza kwa mashabiki kuingia viwanjani, lakini katika msimu huu mechi zote zilizocheza watu wameingia viwanjani kwa viingilio kuanzia Sh3,000, 5,000 huku 10,000 ikiwa ni kwa ma-jukwaa maalumu.

Kiingilio cha JKT huenda kikapunguza idadi ya mashabiki uwanjani katika mchezo huo kwani ni gharama kubwa kulinganisha na utaratibu uliozoeleka kwenye mechi za Ligi Kuu.

Afisa Habari wa JKT,  Masau Bwire amesema tiketi za mchezo hu zitapatikana online, maeneo ya karibu ya uwanja huo na zitauzwa siku ya mchezo saa 3:00 asubuhi.