JIWE LA SIKU: Pacome hapana, mwambieni ukweli Mayele

Unaweza kusema ni kama vijana wa mtaani waliochukuliana mwanamke. Mashabiki wa Yanga na Fiston Mayele kwa sasa ni mwendo wa kurushiana maneno. Ni mwendo wa vijembe tu. Ni taarabu.

Mashabiki hawataki kumuacha Mayele aende. Mayele hataki kuwaacha Yanga waende.

Mayele akishindwa kufunga analaumu Yanga. Yanga ikishindwa kufanya vizuri, Mayele anakuja na vijembe. Kuna tatizo kubwa moja tu naliona - Yanga wanapenda kupitiliza.

Yanga wanajisahau sana. Wamekuwa na tabia ya kumpenda mtu kupitiliza. Mayele ni mchezaji mzuri, lakini Yanga walimpenda kupitiliza na ndiyo maana hadi leo bado wanarushiana maneno. Iko hivi, wachezaji wote wakubwa hupendwa na mashabiki duniani kote. Wachezaji wakubwa hugeuka kuwa kipenzi cha mashabiki, lakini Yanga naona wamezidi.

Yanga wanapenda kupitiliza na wakati mwingine wanampa sifa mchezaji ambazo hata hastahili. Mayele ni mchezaji mzuri lakini Yanga walimpa sifa kupitiliza.

Mayele anaweza kufunga nafasi moja kwenye tano zinazotengenezwa. Sio mchezaji mbaya hata kidogo, lakini alipewa utukufu asiostahili na ndiyo maana bado anasumbua mtandaoni.

Kuna muda watu wengi huwa tunajitanua sana na kuona tumekuwa wakubwa. Wakati mwingine unakuwa mkubwa sio kwa sababu ya uwezo wako, ni taasisi iliyopo nyuma yako.

Mayele sio mchezaji mbaya, lakini Yanga imechangia sana kumkuza. Yanga ilijengwa kwa kumpa yeye ufalme.
 Hakuwa na maajabu sana ni kwa sababu tu aliikuta na Yanga yenyewe inajitafuta. Kuna muda Yanga walikuwa wanamuona Mayele kama Pele. Wamesahau kabisa kama pale Jangwani wamewahi kupita watu kama kina Mohammed Hussein

‘Mmachinga’. Yanga punguzeni kusifia watu kupitiliza.
 Hiki ndicho kinachofanya kelele za Mayele na mashabiki wa Yanga ziendelee. Kwa bahati mbaya, Mayele pia anaonekana ni mtu anayeamini kwenye ushirikina.

Mara leo kataja majini. Mara kesho katajwa kurogwa. Tabu juu ya tabu. Ukiniuliza kama Mayele ni mchezaji mzuri, jibu langu ni ndiyo. Ukiniuliza kama alikuwa anapewa safi anazostahili, jibu langu ni hapana.

Kuna sifa alipewa lakini kimsingi hakustahili. Wananchi wanapenda kupitiliza. Ukitazama namba za misimu miwili ya kwanza ya mshambuliaji wa zamani wa Simba, Meddie Kagere utagundua kuwa alifunga mabao mengi kuliko Mayele.

Yanga wanawatukuza sana wachezaji wao mpaka wanapitiliza. Yanga wakati mwingine wakubali tu kuwa maisha lazima yaendelee. Mayele ni lazima pia ajue kuwa kuna sifa alikuwa anapewa na mashabiki wa Yanga ambazo hakustahili.
Pale Yanga wamepita wafalme wengi sana. Angerudi nyuma akasome. Yeye angeendelea kupambana na hali yake. Unamkumbuka kocha aliyepita wa Yanga? Nasreddine Nabi? Kiukweli kocha huyo alifanya kazi nzuri, lakini Yanga pia walimpamba kupitiliza.

 Kocha Nabi alifika mahali akawa anaitwa profesa. Yanga wanapenda kupitiliza. Baada ya kuondoka kwa Nabi, wengi walidhani Yanga itayumba. Nabi pamoja na kazi nzuri aliyowafanyia Wananchi, alishindwa kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa sasa timu iko chini ya Miguel Gamondi na imefika hatua ya robo fainali. Nabi na Mayele wanarukaruka huko waliko. Yanga inazidi kwenda mbele. ‘Yanga wapunguze mahaba niue kwa wachezaji wao.’

 Yanga wapunguze sifa zilizopitiliza kwa makocha wao. Kuna muda wanajipa ugumu wenyewe kwa sifa wanazotanguliza. Hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu. Sio dhambi hata kidogo mashabiki kuwapenda wachezaji wao, lakini kuwe na kiasi. Sifa zisipitilize,
Mayele alikuwa mchezaji mzuri lakini Yanga walimpa sifa hata asizostahili.


Kwa sasa na yeye angepunguza anachoandika kwenye mitandao naamini angeendelea kufanya vizuri. Sio mchezaji hatari kivile, lakini bado anaweza kucheza popote Afrika na akafanya vizuri.
Ni muda wa watu wanaomsimamia kumwambia ukweli. Anapaswa kuendelea kupambana uwanjani sio mitandaoni. Kuamini kama anarogwa na Yanga ni kupoteza muda wake. Mchezaji anayejitambua hawezi kukaa anawaza kurogwa na timu ambayo ameshaachana nayo. Anapaswa kujua kuwa ligi ya Misri sio kama yetu. Yupo kwenye ligi bora Afrika. Yupo kwenye ardhi yenye mafanikio zaidi Afrika. Ushindani ni mkubwa mno. Sio kama ligi yetu akikosa nafasi nne, bado inakuja nyingine.

Wananchi na nyie punguzeni kuwapa makocha na wachezaji wenu sifa wasizostahili. Naona mlianza kujimimina kwa Maxi Nzengeli, lakini kwa sasa kidogo mmerudi nyuma. Mlishaanza kumuona kama Kylian Mbappe. Tayari naona Pacome Zouzoua mnamuona kama Zinedine Zidane.

Haya ndiyo matatizo ya mashabiki wa Yanga. Tabia ya kuwapa watu sifa wasizostahili wakati mwingine huwafanya wajione kama miungu watu.

Maxi ni mchezaji mzuri, lakini kumuona ana uwezo kama wa Mbappe ni kumdanganya bure.

Pacome ni fundi kwelikweli wa boli, lakini kumfananisha na Zidane ni matusi makubwa. Ukiniuliza mimi kelele za Mayele na mashabiki wa Yanga nitakuambia chanzo ni Yanga wenyewe. Wamemjaza kichwani na kuna muda anajiona kama kweli ni Pele. Nadhani hili ndilo kosa la Yanga.  Kupenda kupitiliza. Mahaba niue.

Njia bora ya Mayele kuwaziba mdomo mashabiki wanaomcharua ni kuendelea kufunga mabao na kuisaidia klabu yake kushinda mataji. Njia bora kwa Yanga ya kumfunga mdomo Mayele ni kuendelea kushinda makombe bila yeye. Mpira ni mchezo wa hadharani, kila mtu ashinde mechi zake.