JIWE LA SIKU: Njia, viunzi Simba itapitia kurejesha ufalme wake

Muktasari:

  • Ukiacha makocha wapya na wachezaji wachache ambao wataungana na timu huko huko Misri kama kipa Mmisri Ayoub Lakred, ambaye ameongeza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia timu hiyo, jeshi la Simba linajumuisha nyota wapya 11 wakiwamo saba wa kigeni na wanne wazawa waliotokea timu mbalimbali.

SIMBA inashusha mashine mpya mfululizo. Yaani kinaingia chuma, kinafuata chuma. Ni mwendo wa sura za kazi tu. Na jana jeshi zima la Wekundu wa Msimbazi lilianza mambo huko Ismailia, Misri iliko kambi ya maandalizi ya msimu mpya.

Ukiacha makocha wapya na wachezaji wachache ambao wataungana na timu huko huko Misri kama kipa Mmisri Ayoub Lakred, ambaye ameongeza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia timu hiyo, jeshi la Simba linajumuisha nyota wapya 11 wakiwamo saba wa kigeni na wanne wazawa waliotokea timu mbalimbali.


Nguvu kubwa iliyotumika katika kujenga upya timu ni jambo lililotarajiwa baada ya Simba kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo hasa baada msimu wa tatu kukumbana na sapraizi kubwa zaidi -- kipigo kikali kutoka kwa wapinzani wao wa jadi, Yanga cha mabao 5-1 na kisha 2-1.

Kufungwa na mtani jumla ya mabao 7-2 katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara ni jambo linalouma. Kuukosa mara tatu mfululizo ubingwa ambao iliubeba kwa misimu minne mfululizo kuanzia msimu wa 2017-18 hadi 2020-21, ni jambo linalouma zaidi. Na kukosa hata nafasi ya pili ya kwenye ligi ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikuwa ni maumivu maradufu ambayo hayavumiliki.

Isingekuwa rahisi kwa Simba kufumba macho na kuingia katika msimu wa nne na kikosi kilekile kilichopotea katika misimu mitatu ya kutoka mikono mitupu kuja kukabiliana na wapinzani wao Yanga ambao wanazidi kuimarika na Azam ambayo ilianza mapema kushusha vifaa kutoka Colombia na kwingineko baada ya kuing'oa Simba katika nafasi ya pili ya ligi msimu uliopita.

Nguvu hii kubwa ya Simba katika kuleta mashine mpya, ilitarajiwa.

Kupitia makala haya, Mwanaspoti linakuletea njia na viunzi vya kuruka ambavyo Simba inatarajiwa kupita katika kusaka kurejesha utawala wake katika soka la nchi hii.


KUBORESHA KIKOSI

Kitendo cha kukosa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo, viongozi wa Simba wakaamua kufanya maboresho makubwa ya kikosi kwa kuangalia namna bora ya kujipanga upya kwa msimu ujao ili walete ushindani ambao utakidhi mahitaji ya timu hiyo.

Kati ya mikakati mizuri iliyofanya katika kikosi hicho, ni kuondoa nyota ambao wameonekana kukwama kwa misimu ya nyuma na kuleta damu changa itakayoleta vitu tofauti, huku suala la umri mdogo likiwa kigezo kikubwa kilichozingatiwa.

Katika wachezaji 11 waliotambulishwa, 10 kati yao wana umri wa chini ya miaka 24 ambao ni Joshua Mutale, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua, Abdulrazack Mohamed Hamza, Valentino Mashaka, Augustine Okejepha na Debora Fernandes Mavambo.

Wengine ni Omary Abdallah Omary, Valentino Nouma na Chamou Karaboue huku kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Fountain Gate FC, zamani Singida Black Stars akiwa ndiye mwenye umri mkubwa zaidi wa miaka 28.


MUUNGANIKO (CHEMISTRY)

Ukiangalia wimbi hilo lote la wachezaji wapya, ni dhahiri Simba itahitajika muda kwa ajili ya kutengeneza muunganiko wa timu (chemistry), hii ni kutokana na wengi wao kutoka mataifa mbalimbali na hawajazoeana namna ya uchezaji kwa pamoja.

Haitokuwa kazi ya siku moja au mbili japo jambo nzuri wameanza maandalizi ya msimu wakiwa pamoja (pre-season) ambayo itafanyika katika mji wa Ismailia Misri kwa takribani wiki tatu ambazo zitaanza kutengeneza muunganiko wa kikosi hicho.


BENCHI JIPYA LA UFUNDI

Julai 5, mwaka huu, Simba ilitangaza benchi jipya la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu, Fadluraghman 'Fadlu' Davids, kocha msaidizi, Darian Wilken, kocha wa makipa, Wayne Sandilands, kocha wa viungo, Reidoh Berdien na mtathimini michezo, Mueez Kajee.

Fadlu alikuwa straika wa Vasco Da Gama, Avendale Athletico, Silver Stars, Maritzburg United zote za Afrika Kusini kabla ya kustaafu soka 2012, ambapo ametua Simba baada ya kuachana na Raja Casablanca alikokuwa msaidizi wa Josef Zinnbauer.

Msimu uliopita, Fadlu aliipa Raja ubingwa wa Ligi ya Morocco sambamba na Kombe la Mfalme huku akipenda kutumia mfumo wa mabeki wanne, viungo wakabaji wawili, viungo washambuliaji watatu na straika mmoja yaani 4-2-3-1 ambao Simba inautumia.

Kitendo cha kocha huyo kutua na wasaidizi wake wote raia wa Afrika Kusini ambayo ndiyo nchi anayotokea, huenda kikaleta tija kubwa katika kikosi hicho kwani watakuwa wanaongea lugha moja jambo litakalorahisisha utendaji wao wa kazi pamoja.

Kocha huyo amepewa jukumu hilo baada ya kuondoka kwa Mualgeria, Abdelhak Benchikha aliyeondoka Aprili 28, mwaka huu kwa matatizo ya kifamilia baada ya kutwaa taji la Kombe la Muungano lililohitimishwa Aprili 27, 2024 huko visiwani Zanzibar.

Fadlu amekuwa chini ya makocha bora na wenye uwezo wa juu ambapo alikuwa chini ya Mjerumani, Josef Zinnbauer aliyewahi kuzifundisha Hamburger SV inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani, Lokomotiv Moscow (Urusi) na Orlando Pirates kutoka Afrika Kusini.

Mwingine ni kocha wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes', Milutin Sredojevic 'Micho', aliyefanya kazi naye katika timu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini sambamba na Rhulani Mokwena kwenye kikosi hicho hicho pia.

Mwingine ni Mjerumani, Ernst Middendorp aliyekuwa kocha wa zamani wa Singida Fountain Gate ambaye walifundisha pamoja katika kikosi cha Maritzburg United cha Afrika Kusini akiwa kocha msaidizi kisha baadaye kukiongoza akiwa kocha mkuu.

Licha ya uzoefu mkubwa ambao Fadlu amepata kutoka kwa makocha wakubwa na wazoefu, ila haitokuwa rahisi kwake kwa sababu atakutana na presha kubwa hasa ile ya wapinzani wao wakubwa Yanga ambao msimu uliopita iliwachapa jumla ya mabao 7-2.

Kocha huyo aliyezifundisha timu kama Moroka Swallows, St George, Kaizer Chiefs pamoja na Golden Arrows, anapaswa kujua Simba sio klabu ya kuvumilia kocha kwani tangu msimu wa 2017-2018, hadi sasa tayari imeajiri makocha 10 na kuwatimua.

Makocha hao ni Pierre Lechantre, Patrick Aussems, Sven Vandenbroeck, Didier Gomes, Pablo Franco, Zoran Maki, Juma Mgunda, Roberto Oliveira 'Robertinho' na Abdelhak Benchikha ambao kwa nyakati tofauti waliondoka licha ya uzoefu wao.


UBORA WA WAPINZANI

Waswahili walisema, 'usijisifu una mbio, bali mfikirie na anayekukimbiza', hii maana yake ni kwamba licha ya Simba kutamba juu ya usajili walioufanya ila ni lazima pia ijipange vizuri kutokana na maboresho ambayo wapinzani wake wameyafanya.

Yanga ambayo imetawala kwa misimu mitatu mfululizo katika Ligi Kuu Bara na matajiri wa jiji la Dar es Salaam, Azam FC iliyowanyima nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao wamezidi kujiimarisha huku wakiwa na wachezaji ambao wamezoeana zaidi na kuunda timu tishio kwa kuongeza wakali wengine.

Kwa upande wa Yanga tayari imefanya maboresho ya wachezaji wapya ili kuongeza nguvu ambapo imeinasa saini ya aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama na kuongeza washambuliaji wawili, Prince Dube na Jean Baleke kikosini humo.

Ukiangalia usajili wa Chama utaona kabisa Yanga imedhamiria kuendeleza ufalme kutokana na ubora wa nyota huyo wa Zambia hasa katika kutengeneza mashambulizi huku uwepo wa Dube na Baleke ni wazi mabeki watakuwa na kazi kubwa msimu ujao.

Viongozi wa Yanga ni kama wametatua changamoto ya eneo la ushambuliaji ambalo tangu aondoke Fiston Mayele aliyejiunga na kikosi cha Pyramids FC cha Misri msimu wa 2022-2023, hakuna mshambuliaji aliyeweza kuvaa viatu vyake ipasavyo kikosini.

Licha ya msimu uliopita, nyota raia wa Ivory Coast, Joseph Guede aliyejiunga na kikosi hicho Januari mwaka huu akitokea Tuzlaspor FC ya Uturuki kufunga mabao sita ya Ligi Kuu Bara, bado viongozi wa Yanga wamekuwa hawana imani kwake.

Kwa upande wa Azam FC, licha ya kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita, changamoto kubwa ambayo iliyoiangusha ilikuwa ni eneo la ushambuliaji hali iliyopelekea michezo mingi kucheza kwa kutumia viungo washambuliaji.

Hii inaonyesha wazi kwani msimu uliopita kiungo mshambuliaji, Feisal Salum 'Fei Toto' ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa timu hiyo akifunga mabao 19, nyuma ya kinara na mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, Stephane Aziz KI wa Yanga aliyefunga 21, ambaye pia ni kiungo.

Kutambua ukubwa wa tatizo hilo, viongozi wa Azam FC wakaboresha kikosi hicho kwa kuinasa saini ya mshambuliaji, Jhonier Blanco, kutoka klabu ya Aguilas Doradas inayopatikana katika mji wa Rionegro, inayoshiriki Ligi Kuu ya kwao Colombia. 

Blanco aliyezaliwa Oktoba 18, 2000, alianzia soka lake kwenye akademi ya Club Deportivo Estudiantil kabla ya kujiunga na timu ya Ligi Kuu ya Aguilas Doradas kisha kutolewa kwa mkopo kujiunga na klabu ya daraja la kwanza ya Fortaleza CEIF.


Akiwa na Fortaleza, aliibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza Colombia (Categoría Primera B) ambapo alifunga mabao 13, msimu wa 2022/2023 na kuipandisha daraja huku msimu uliopita akifunga mabao 18 katika mechi 26 za mashindano yote.


KUPEWA MUDA

Presha ya mashabiki ndiyo iliyowasukuma baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo kujiuzulu nafasi zao ambao miongoni mwao ni aliyekuwa Mwenyekiti, Salim Abdallah 'Try Again' na kumpa kijiti Mwekezaji na Rais wa Heshima, Mohamed Dewji 'Mo'.

Wakati Try Again akitangaza kujiuzulu nafasi hiyo, alimuomba Mo Dewji kuchukua kiti hicho ingawa kama utakumbuka kabla ya hapo MO Dewji alikuwa Mwenyekiti wa Bodi kisha kujiuzulu Septemba 2021 na kukaa nje kwa miaka minne hadi aliporejea mwaka huu.

Mashabiki wa Simba hawapaswi kuwapa wachezaji presha hususani kutokana na aina ya mastaa iliowasajili na badala yake inapaswa kuwaunga mkono kwa kiasi kikubwa huku wakitambua itawachukua muda kidogo kuzoeana ili kutengeneza kikosi imara.

Miongoni mwa nyota ambao wataangaliwa zaidi ni kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ohoua aliyetokea Stella Adjame ya kwao Ivory Coast ambaye anatazamiwa kama mbadala wa Clatous Chama kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kwa msimu uliopita.

Nyota huyo msimu uliopita akiwa na kikosi hicho cha Stella Adjame, alikuwa mchezaji bora (MVP), wa Ligi Kuu ya Ivory Coast baada ya kufunga jumla ya mabao 12 na kutoa asisti zilizozaa mabao mengine tisa hivyo kuwavutia mabosi hao wa Msimbazi kumsajili.

Takwimu zake ndizo ambazo zitamfanya kuangaliwa zaidi ingawa mashabiki wa timu hiyo wanapaswa kuendelea kumuunga mkono na kumpunguzia presha kwani kama tulivyosema awali, wachezaji wengi ni wapya na wanahitaji muda wa kuzoeana kwa pamoja.