JIWE LA SIKU: Maajabu ma5 ya Gamondi

KUNA watu walimchukulia poa Miguel Gamondi. Kocha huyo kutoka Argentina, alipotangazwa na Yanga mwishoni mwa msimu uliopita kuna watu walimuona anakuja kuzingua tu.

Hii ilitokana na ukweli mtangulizi wake, Nasreddine Nabi aliondoka Yanga akiwa ameweka rekodi ya kusisimua. Kocha Nabi alitoka kuifikisha Yanga kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa timu ya Tanzania kucheza hatua hiyo, tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa Kombe la CAF na Kombe la Washindi Afrika.

Hiyo ni mbali na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara bila kupoteza misimu miwili iliyopita na kuiongoza Yanga kucheza mechi 49 mfululizo bila kupoteza ikiwa pi ni rekodi ambayo inaweza ichukue muda mrefu kabla ya kufikiwa au kupitwa hata na Yanga wenyewe.

Hivyo, baada ya Yanga kuachana na Nabi Juni 15 mwaka jana, mashabiki wa timu hiyo waliamini huenda wangefanya vibaya katika michuano mbalimbali kutokana na imani kubwa waliyokuwa nayo kwa raia huyo wa Tunisia.

Wengi waliamini kocha yeyote ambaye angeajiriwa Yanga asingeweza kufikia mafanikio ya Nabi na Juni 24, uongozi wa klabu hiyo ilipomtangaza Gamondi walimchukulia poa, kwa vile hakuwa na rekodi yeyote tamu na hasa ugeni wake wa kufundisha soka ukanda wa Afrika Mashariki.

Lakini mwamba huyo amewawathibitisha mashabiki kwamba mabosi wa Yanga hawakukosea kumpa kibarua hicho, kwani ndani ya muda mfupi amefanya maajabu matano yaliyomfanya ajitofautishe sio na Nabi tu, bali karibu makocha kadhaa waliowahi kupita Yanga tangu timu hiyo ilipocheza mara ya kwanza makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1998.

Mwanaspoti linakuletea maajabu na rekodi tano zilizowekwa na kocha huyo aliyewahi kuzinoa timu mbalimbali za Afrika Kaskazini na Afrika Kusini zinazomfanya sasa ajitengenezee ufalme ndani ya timu hiyo.


KUIVUSHA MAKUNDI
Gamondi aliipeleka timu hiyo makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25 kufuatia kufanya hivyo mara ya mwisho 1998 wakati huo ikinolewa na kocha wa muda, Tito Mwaluvanda aliyempokea Mwingereza, Steve McLennan.

Mwaluvanda alipewa timu hiyo akiwa hana umaarufu wowote na aliyekuwa Mwenyekiti, Rashid Ngozoma Matunda ambapo kikosi hicho kiliangukia kundi la kifo na ASEC Mimosas (Ivory Coast), Manning Rangers (Afrika Kusini) na Raja Casablanca ya Morocco.

Kwa wakati huo, mechi ya kwanza tu Yanga ilichapwa mabao 6-0 na Raja Casablanca, ikachapwa 3-0 na ASEC Mimosas kwenye Uwanja wa Uhuru kisha ikaenda Afrika Kusini kupambana na Manning Rangers na kuambulia kichapo kingine cha mabao 4-0.

Baada ya hapo ikapoteza ugenini 2-1 dhidi ya ASEC Mimosas, 1-1 na Manning kisha sare ya mabao 3-3 na Raja Casabalanca kwenye Uwanja wa Uhuru na kumaliza michezo sita ya hatua ya makundi ikiwa imefunga mabao matano tu na kuruhusu 19.

Gamondi aliyewahi kufundisha timu mbalimbali amefika hatua hiyo ya makundi baada ya miaka hiyo 25 kufuatia kuifunga Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo kwani awali ilikuwa haijawahi kushinda.

Yanga ilikuwa haijawahi kuifunga Al Merrikh katika mechi za CAF ila chini ya Gamondi timu hiyo ya Sudan ilipoteza mabao 2-0 ya Kennedy Musonda na Clement Mzize ikiwa uwanja wa nyumbani Rwanda kisha marudiano jijini Dar es Salaam kuchapwa 1-0.

Maajabu yake ni kwamba ameipokea timu na moja kwa moja kuipeleka makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kitu ambacho hakijawahi kufanywa hata na Nabi, kwani kocha huyo aliyepo kwa sasa FAR Rabat ya Morocco katika miaka miwili na nusu aliyokuwapo Yanga, alikwama mara mbili aking'oka hatua ya awali mbele ya Rivers United ya Nigeria, kisha ikaatolewa raundi ya kwanza na Al Hilal ya Sudan.


ROBO FAINALI
Ushindi wa mabao 4-0, ilioupata Yanga dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria juzi katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, imemfanya Gamondi kuandika rekodi mpya baada ya kuivusha robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo tangu michuano hiyo ilipobdilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika mwaka 1997.

Kwa mara ya kwanza Yanga iliwahi kucheza hatua ya robo fainali enzi hizo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970 na kucheza makundi 1998 ila tangu hapo haikuwa na maajabu hadi msimu uliopita kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Pia iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016 na 2018 huku ikifika robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika 1995.


KUMPIGA MWARABU 4-0
Haijawahi kutokea kwa timu yoyote ya Tanzania kupata ushindi mnono kwa klabu kutoka Afrika Kaskazini maarufu Waarabu, lakini chini ya Gamondi, Yanga imefanya kweli kwa kuifunga Belouizdad.
Sio kumfungwa Mwarabu tu, lakini ushindi ulioenda na soka tamu na la kusisimua lililowaduwaza Waalgeria ambao kwenye mechi ya kwanza nyumbani kwao, walishinda mabao 3-0, licha ya kupigiwa mpita mwingi vilevile.

Ushindi huo umeifanya Yanga kuvuka robo fainali kwani hata kama Belouizdad itashinda mechi ya mwisho dhidi ya Medeama ikiwa nyumbani na Yanga kupasuka kwa watetezi wa taji, Al Ahly ya Misri, bado matokeo baina yao yanaibeba vijana wa Gamondi na hilo ni ajabu jingine kwa kocha huyo Muargentina akiipiku rekodi ya Simba.

Simba ilikuwa ikishikilia rekodi ya kupiga timu ya Afrika Kaskazini kwa mabao mengi, ilipoifumua JS Saoura ya Algerias kwa mabao 3-0 katika michuano hiyo kwa msimu wa 2018-2019 kwa mabao ya Emmanuel Okwi na Meddie Kagere aliyefunga mawili na kuifanya kumaliza nafasi ya pili katika kundi D ikiwa na pointi tisa nyuma ya vinara Al Ahly.


KUMPIGA SIMBA MKONO
Kama kuna tukio lililomheshimisha Gamondi mbele ya mashabiki wa klabu hiyo na kuwatetemesha wale wa Msimbazi ni kipigo cha 5-1 ilichopewa Simba kwenye Ligi Kuu Bara.

Simba ilikuwa haijawahi kufungwa na Yanga idadi kama hiyo kubwa ya mabao tangu ilipolazwa 5-0 mwaka 1968, kipigo ambacho Simba ilikilipa kwa kishindo mwaka 1977 kwa kuifumua Yanga 6-0 kisha kupigilia msumari mwingine wa mabao 5-0 mwaka 2012. Vipigo hivyo viliifanya Yanga inyanyasike mbele ya Simba kwani kila walichokuwa wakikifanya walikejeliwa kwamba wameshindwa kulipa kisasi cha 6-0 cha zaidi ya miaka 40, lakini ujio wa Gamondi na miujiuza yake uwamerejeshea jeuri Yanga baada ya mechi hiyo ya Kariakoo Derby ya Novemba 5 mwaka jana.

Kipigo hicho kikubwa kwa Yanga dhidi ya Simba ndicho kilichomfukuzisha kazi kocha maarufu wa soka la Afrika Mashariki na Kati, Roberto Oliveira 'Robertinho', aliyekuwa akionekana anaijulia sana Yanga kwani ameshaitungua kama mara tatu kwenye mechi tofauti ikiwemo ya Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii, lakini mambo yamebadilika.


VIPIGO VIKALI
Achana na yote hayo, kocha Gamondi ameandika pia ajabu jingine la kutoa dozi nono karubu kwenye michuano yote ambayo timu hiyo iliyoshiriki chini ya Muargentina.

Yanga ilitoa dozi ya tano tano kwa wapinzani wake kwenye michuano minne tofauti ikiwamo Ligi Kuu Bara, Kombe la Mapinduzi, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Gamondi alianza kwa kuifumua Asas ya Djibouti kwenye mechi ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa kwa mabao 5-1, lakini kuna watu walimkebehi wakisema amewaotea vibonde, lakini akaja kwenye Ligi Kuu akaifumua JKT Tanzania kwa mabao 5-0 kabla ya kuifumua KMC kwa idadi kama hiyo ndipo akaifumua Simba kwa 5-1.

Moto wa Gamondi unaendelea kwenye mechi za Kombe la Mapinduzi kwa kuifumua Jamhuri kwa mabao 5-1, huku kwenye Kombe la ASFC, Yanga ilishinda 5-1 dhidi ya Hausung ya Njombe, kisha kuifumua Polisi Tanzania kwa mabao 5-0 na kutinga hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo. Rekodi inaonyesha hakuna kocha yeyote nchini aliyewahi kupata matokeo ya kupiga wapinzani 5G, hapo ni mbali na zile mabao 4-1 iliyoipiga Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu Bara kisha kuifumua Belouizdad 4-0 kuonyesha kwamba Yanga ya Gamondi ukikaa vibaya unapigwa nyingi na huwezi fanya lolote.


MSIKIE  GAMONDI SASA
Akizungumzia na Waandishi wa habari baada ya mchezo na CR Belouizdad, Gamondi anasema, siri kubwa ni ushirikiano mkubwa uliopo baina ya benchi la ufundi, wachezaji na viongozi ambao wamekuwa ni sehemu ya chachu ya mafanikio waliyofikia.

"Hii ni ya kila mmoja wetu lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya na kufika mbali zaidi ya hapa tulipo, tuna wachezaji wazuri ambao ndio wapambanaji wetu lakini huwezi kuacha kutoa pongezi kwa viongozi kutokana na hatua hii," anasema.