JIWE LA SIKU: Freddy, Sarr hii ni shoo yenu Ivory Coast

KOCHA Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha mjanja sana. Baada ya kugundua timu hiyo haitashuka tena uwanjani leo kuvaana na Mtibwa Sugar, fasta ameamua kuja na mbinu mpya ili kuhakikisha mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast inakuwa nyepesi ugenini kabla ya kuialika Jwaneng Galaxy.
Simba itavaana na vinara wa Kundi B waliotangulia robo fainali Asec, Ijumaa Februari 23 mjini Abidjan, kabla ya kurudi nyumbani mapema mwezi ujao kumalizana na Jwaneng Galaxy kutoka Botswana na iwapo itapata matokeo mazuri kwenye mechi hizo mbili itafuzu kwa mara nyingine hatua ya robo fainali na kuzidi kuboresha rekodi zake ndani ya CAF.
Katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa freshi, Benchikha amefichua furaha aliyo nayo kwa kuahirishwa kwa mchezo wa Ligi Kuu uliokuwa upigwe kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakiwa wenyeji dhidi ya Mtibwa Sugar, akiupongeza uongozi wa Simba na Bodi ya Ligi, huku akisisitiza kazi aliyonayo kwa sasa ni kuimarisha eneo la ushambuliaji linalotumiwa na kina Michael Freddy, Pa Omar Jobe na wenzao ili apate mabao, lakini akiwabana pia viungo wakabaji wa timu hiyo.
Eneo la kiungo lina mafundi kama Babacar Sarr, Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin na Fabrice Ngoma, kocha akisema kama maeneo hayo mawili yatazingatia mbinu atakazowapa basi ana matarajio makubwa ya kufanya vizuri zaidi.
Freddy, Pa Jobe na Sarr ni kati ya wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba katika dirisha dogo lililofungwa mwezi uliopita wakiwamo viungo washambuliaji wazawa, Edwin Balua, Ladack Chasambi na Saleh Karabaka ambao bado wanajitafuta mbele ya mastaa wengine waliowakuwa kikosini kwa sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Benchikha alisema kusogezwa mbele kwa mchezo huo ni hatua nzuri kwao kwao, timu ilikuwa imecheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi na kuwachosha wachezaji, lakini sasa anapata muda wa kujiandaa kwa mchezo huo wa kimataifa wa Kundi B akiamini akirekebisha mambo kazi itakuwa rahisi kwao.
Benchikha alisema kuna maeneo mawili anaenda kuyafanyika kazi na kuyapa mbinu mpya kabla ya kusafiri kwenda Ivory Coast kwa lengo la kutotaka kupoteza mbele ya wapinzani wao hao waliotoka nao sare nyumbani.
“Asec ni timu ngumu na mechi hiyo sio rahisi kabisa kwa upande wetu, licha ya kuwa walishacheza mchezo wa kwanza na wachezaji wanafahamiana ila bado kazi ipo,” alisema Benchikha na kuongeza;
“Kwenye maandalizi haya nitazingatia zaidi eneo la ushambuliaji ili kuwafanya wachezaji wa eneo hilo wawe bora zaidi hasa katika kutumia nafasi na kufunga, lakini pia eneo la kati hawatakiwi kuruhusu bao la mapema na kuhahakikisha wapinzani hawapati upenyo wowote.”
Katika mechi mfululizo ilizocheza Simba tangu kurejea tena kwa Ligi Kuu, timu hiyo imeonekana kupata matokeo mazuri kwa shida sana. Ukiacha ushindi wa 4-0 dhidi ya Tabora United, Simba imeshinda bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, imetoka sare ya 1-1 dhidi ya Azam na kuzifunga Geita Gold na JKT Tanzania bao 1-0 kila moja. Kiujumla Simba imekuwa ikicheza soka ambalo bado haliridhishi. Ingeweza kupoteza mechi dhidi ya Azam na dhidi ya JKT Tanzania, ambazo kiuhalisia zilipoteza nafasi nyingi za wazi za kuwazamisha Wekundu wa Msimbazi. Hii sio ishara njema unapokuwa unaenda kukutana na timu kubwa zenye ushindani katika michuano mikubwa zaidi katika ngazi ya klabu barani Afrika.
Lakini Simba anakuwa mnyama tofauti kabisa anapokuwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Hakufika robo fainali ya michuano ya CAF mara nne katika miaka mitano iliyopita kibahati. Ni kwa sababu Wekundu wa Msimbazi wanatisha sana wanapotambua hii ni michuano ya CAF.
Hii inapaswa kuwa shoo ya nyota wanaotokea Afrika Magharibi. Freddy mechi hii unachezwa nchini mwake Ivory Coast, wakati Sarr ni raia wa Senegal na Jobe kwao ni Gambia. Nyota hao wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo tayari wameonyesha kwamba wana kitu. Jobe, Sarr na Freddy, kila mmoja amefunga bao moja kwenye Ligi Kuu Bara. Huu ni mwanzo mzuri ukizingatia timu imecheza mechi nne tu tangu ligi irejee baada ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023. Kwa dalili nje hizi, Benchikha hatakosea kuwapa wakali hao wasimamie shoo kwenye ukanda wa nyumbani kwao.
Simba, licha ya mechi hizo nne kuvuna jumla ya pointi 10 na kuifanya ipande hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi 36 baada ya mizunguko 15, ikiwa nyuma ya Yanga yenye alama 43, kocha Benchikha alisema bado hafurahishwi na namna timu inavyopoteza nafasi za mabao na pia kuelemewa na wapinzani, japo anakiri kucheza mechi mfululizo katika ratiba ni tatizo.
Benchikha alisema anaamini wachezaji wakizingatia atakachowaelekeza, huenda furaha ya mashabiki wa Simba ikawa maradufu, kwani timu hiyo ina kikosi imara chenye wachezaji wenye ubora wa hali ya juu, ila hawajawa watulivu tu.
Mechi dhidi ya Asec, ndio inayoonekana ngumu kwa Simba, kwani haina rekodi ya kushinda ikiwa ugenini dhidi ya wapinzani wao hao wanaoongoza kundi wakiwa na pointi 10 baada ya mechi nne, kuliko mchezo wa mwisho mbele ya Jwaneng ambayo imeonekana sio tishio kwenye kundi hilo hadi sasa.
Hata hivyo, Simba inapaswa kuwa makini kwani misimu miwili iliyopita iliwatoa nishai Kwa Mkapa kwa kuwang’oa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kwa kuwafunga mabao 3-1 na kufuzu kwa faida ya bao la ugenini kutokana na ushindi wa 2-0 iliyopata Simba ugenini na kufanya matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 3-3.
Katika mechi ya kwanza baina ya Simba na Asec iliyopigwa Dar es Salaam, Saido Ntibazonkiza aliwafungia Wekundu bao la penalti, huku wageni wakipata kupitia kwa Serge Pokou aliyewasawazishia kipindi cha pili, ilhali Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi tano ikifuatiwa na Jwaneng yenye nne wakati Wydad CA ikiburuza mkia ikiwa na alama tatu.