Jino moja: Wakiumia tu majanga kwenye timu zao

Muktasari:

Barca inategemea mabao mengine kutoka kwa wachezaji Lionel Messi, Philippe Coutinho na Ousmane Dembele, lakini hao hakuna hata mmoja namba 9 wa asili.

LONDON, ENGLAND

KUWA na straika wa kiwango cha dunia kwenye timu, hilo linakupa nafasi kubwa ya kushinda mechi, ukishinda mechi inamaana unashika taji lakini jambo kubwa ni uhakika wa kupata mabao.

Lakini, ni jambo la wazi kabisa haiwezekani kwa mchezaji mmoja kucheza kila mechi katika michuano yote bila ya kuwapo kwa mbadala wake, ambaye walau kidogo watakuwa wanakaribiana kwa uwezo ili kuifanya timu husika kutokuwa kwenye presha kubwa kama itatokea mchezaji huyo namba moja wao ni majeruhi au anatatizo lolote na hatakuwapo kwenye mechi.

Hata hivyo, kuna klabu kubwa Ulaya zinafanya makosa makubwa kwa kuwa na straika mmoja tu mwenye uwezo mkubwa na ikitokea amepata majeruhi basi inakuwa majanga maana hakuna mwingine mwenye uwezo wa kufunga kama aliyokuwa nao straika huyo namba moja.

 

5.Bayern Munich- Robert Lewandowski

Bayern Munich kwa sasa wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Bundesliga nyuma ya Borussia Dortmund. Wababe hao wa Ujerumani silaha yao ya mabao wanayoitegemea ni Robert Lewandowski baada ya kuonekana kama Sandro Wagner amekuwa si mtu mwenye uhakika sana kwenye kuwapatia mabao. Kikosi hicho cha Allianz Arena, kina mastaa wengine pia kwenye eneo la ushambuliaji kama vile Thomas Muller, lakini ukweli ni kwamba Lewandowski ndiye namba 9 wao makini zaidi anayewapata jeuri ya kujisifu na kuendelea kupambana kwenye michuano mbalimbali. Lewandowski kwa upande wake, amefunga mabao 23 katika mechi 25 za michuano yote aliyocheza kwa msimu huu. Hakika, Bayern wanamtegemea zaidi Lewandowski, kwa sababu hawana straika mwingine wa daraja lake kwenye kikosi.

 

4.Inter Milan- Mauro Icardi

Inter Milan ni timu nyingine inayomtegemea straika mmoja tu kufunga mabao yake, Mauro Icardi. Amefunga mabao 13 msimu huu, lakini mshambuliaji mwingine wanayemtegemea Inter ni Keita Balde, amefunga mabao manne tu. Hapo unaweza kuona tofauti kubwa sana ya ubora kwenye kufunga uliopo baina ya Icardi na Balde. Licha ya kwamba Inter kwa msimu huu wapo kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa Serie A, wababe hao wamekuwa wakitegemea zaidi mabao ya Icardi kwa sababu hawana mshambuliaji mwingine wa kati mwenye ubora mkubwa. Ukweli ni kwamba kama Inter watahitaji kuwapa wakati mgumu Juventus kwenye mbio za ubingwa wa Serie A basi ni lazima ifanye mchakato wa kusajili straika mwingine mwenye uwezo kama wa Icardi ili kujihakikisha mabao kwamba Muargentina huyo anapokuwa majeruhi, basi kuna mtu matata wa kuchukua nafasi yake.

 

3.Real Madrid- Karim Benzema

Kwa timu kama Real Madrid, ni kuna kubwa sana tena kubwa kwelikweli kwa kushindwa kuwa na straika mwingine mbadala. Kwa sasa macho yao yote yapo kwa Karim Benzema, ambaye amefunga mabao saba tu kwenye ligi na 12 kwa ujumla wake, kitu ambacho si kizuri kwa klabu kubwa kama hiyo. Mabao mengine Real Madrid imekuwa ikiyatapata kutoka kwa winga Gareth Bale. Kitendo hicho kimewagharimu pakubwa sana na ndio maana hadi sasa wamefunga mabao 30 tu kwenye mechi 20 walizocheza kwenye La Liga. Kwa hali ilivyo kwa sasa, Benzema akiumia tu basi ni majanga, hakuna namba 9 mwingine wa kuja kuzuba pengo lake la kufunga japo kwa uchache huo huo. Licha ya kwamba walimsajili Mariano Diaz kwenye dirisha lililopita, lakini si mtu wa kukaribiana na Benzema kwa viwango.

 

2.Tottenham- Harry Kane

Harry Kane ni straika matata kabisa kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur, ndani ya misimu mitatu iliyopita ametwaa Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England mara mbili. Angekinyakua pia msimu uliopita kama si Mohamed Salah kuwa kwenye msimu wake bora kabisa huko Liverpool. Straika huyo Mwingereza amefunga mabao 155 katika michuano yote aliyocheza tangu aanze kutumika kwenye kikosi cha kwanza msimu wa 2013/14. Lakini, kila wakati Kane anapopata majeruhi, Spurs wamekuwa kwenye hali mbaya sana kwa sababu hakuna mbadala wake mwenye kiwango kinachokaribiana naye.

Spurs haina straika mwingine mwenye uwezo kama wa Kane na ndio maana anapoumia kama ilivyo kwa sasa ni majanga.

 

1.Barcelona- Luis Suarez

Klabu nyingine kubwa kabisa huko Ulaya yenye straika mmoja tu matata na hana mbadala wake ni Barcelona. Barca wanategemea zaidi huduma ya mshambuliaji wao huyo namba moja na kwamba hawana namba 9 mwingine mwenye uwezo kama wa mkali huyo wa Uruguay.

Hiyo ni hatari zaidi kwa Barcelona, kwa sababu Suarez umri umeshakwenda na kama atakumbana na majeruhi, basi wakali hao wa Nou Camp watakuwa kwenye matatizo makubwa.

Sawa, Barca inategemea mabao mengine kutoka kwa wachezaji Lionel Messi, Philippe Coutinho na Ousmane Dembele, lakini hao hakuna hata mmoja namba 9 wa asili.