Jide ni Commando zaidi ya Binti Machozi - 2

Muktasari:
JUDITH Wambura Mbibo kesho anasherehekea siku yake ya kuzaliwa, akitimiza umri wa miaka 41. Ni mtu mzima. Lakini amepitwa miaka miwili na Shakira mwenye umri wa miaka 43, na amezidiwa miaka 10 na Jennifer Lopez ambaye mwezi ujao anatimiza miaka 51.
JUDITH Wambura Mbibo kesho anasherehekea siku yake ya kuzaliwa, akitimiza umri wa miaka 41. Ni mtu mzima. Lakini amepitwa miaka miwili na Shakira mwenye umri wa miaka 43, na amezidiwa miaka 10 na Jennifer Lopez ambaye mwezi ujao anatimiza miaka 51.
‘Age Ain’t Nothing But A Number’. Umri si chochote ila ni namba tu. Aliimba staa wa zama zake Aaliyah (sasa marehemu).
Jide bado anadai. Na wazungu wanasema ‘Life Begins at 40’. Wanaafikiana na kitabu kilichotungwa mwaka 1932 na mwandishi wa vitabu wa Kimarekani, Walter B. Pitkin kilichoitwa ‘Life Begins at Forty’ na kuongoza kwa mauzo. Jina la kitabu hicho limekuwa msemo maarufu sana wa hamasa. Wanamaanisha ukiwa na miaka 40, unaweza kuishi kiwerevu vizuri zaidi kwa sababu una uzoefu zaidi wa maisha. Hivyo Jide ndio kwanzaa kesho anatimiza mwaka mmoja tu ndani ya “yale maisha yanayoanza ukiwa na miaka 40.”
Kama maisha yanaanza ukiwa na miaka 40, Jide anayaanza akiwa na rekodi za kila aina katika kazi yake ya Bongofleva, ambazo kila msanii anayeinukia nchini angetamani kuwa nazo.
Tangu alipotambulishwa katika game kupitia wimbo ‘Mambo ya Fedha’ alioshirikishwa katika albam ya tano ya Sugu ya ‘Millenia’ ya mwaka 2000, na kisha kuachia wimbo wake wa kwanza uliomtangaza sana wa ‘Machozi’, Jide hakurudi nyuma.
Aliachia ‘hit’ baada ya ‘hit’ na albam za kutosha zikafuata kuanzia ‘Machozi’ (2000), ‘Binti’ (2003), ‘Moto’ (2005), ‘Shukrani’ (2007), ‘Ya 5. The Best of Lady Jaydee’ (2012), ‘Nothing But The Truth’ (2013) hadi ‘Woman’ (2017).
Jide ni mshindi wa zaidi ya tuzo 36 zikiwamo za ndani na za Afrika. Ni gwiji.
Hata hivyo, hajafika alipo kirahisi. Amepitia ‘struggles’ nyingi za maisha binafsi na ya kikazi na ndio sababu naamini kumuita Commando ndio stahiki yake kuliko kumuita Binti Machozi, japo yote ni majina yake maarufu ya utani.
Katika maisha binafsi, alikuwa mke wa mtangazaji Gadner G. Habash na katika kazi alikuwa chini ya Ruge Mutahaba (sasa marehemu) ambaye alikuwa muasisisi wa lebo ya kusimamia wasanii ya Smooth Vibes.
Kote huko alipita katika mabonde na milima. Alikuwa na nyakati za furaha na mafanikio na pia alikuwa na nyakati za migogoro mikubwa iliyofikia kupelekana mahakamani na kutoleana kauli za maapizo.
Wimbo wake uliotamba wa ‘Wanaume Kama Mabinti’ ulihusishwa na mgogoro wake wa kiuhusiano na Gadner, akidaiwa kwamba aliutunga kumshambulia mwanaume huyo aliyeaminika alimpenda sana.
Jide aliwahi kudaiwa kutunga karibu albam nzima ya kumchana mwanaume huyo walipotofautiana.
Ndoa yao ilipoingia mgogoro yalifuatia malumbano ya kwenye magazeti yaliyoambatana na tuhuma hizi na zile zikiwamo za usaliti wa ndoa. Na mwisho wa yote, wawili hao wakatengana.
Kimuziki, Jide alikuwa kwa muda mrefu tu ndiye msanii mwenye mafanikio zaidi nchini. Mapema tu alimiliki mjengo wake mkali, akatembelea gari kali zaidi, huku akiingiza mkwanja wa maana kutokana na shoo zake akiwa na bendi yake aliyoimiliki ya Machozi Band iliyokuwa ikitumbuiza kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge.
Akawa na shoo ya maisha yake halisi kwenye televisheni ya EA TV iliyokwenda kwa jina la ‘Diary ya Lady Jaydee’.
Lakini kutofautiana na wasimamizi wake kulizua mgogoro mkubwa.
Alifikia kusema nyimbo zake zisipigwe na Radio Clouds FM na hata akifa “wasiende kumzika. Wakienda wapigwe mawe.”
Kupitia blog yake, Jide aliandika kuwa anatamani afe kabla ya Ruge na Joseph Kusaga na akifa wasiende kumzika. Mabosi hao wa Clouds Media Group wakamshitaki. Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ikatoa hukumu mwaka 2016 ya kumuamuru Jide aombe radhi kwa kauli zake za kuwachafua.
Kuanzishwa kwa Skylight Band iliyotamba na wimbo ‘Caroline (Mbona wenzako wanacheza lakini wewe umenuna)’, ambayo iliwachukua mastaa kadhaa wa Machozi Band, kama Johnico Flower, Aneth Kushaba na Sam Machozi, kulihusishwa na mpango mchafu maalum wa kutaka kumsambaratisha Jide. Ni kweli? Ukweli wanao wahusika.
Ila kwa vyovyote iwavyo, Commando bado anasonga.