JICHO LA MWEWE: Papaa Molinga amefichua kinachoendelea Yanga

Tuesday June 16 2020
MOLINGA PIC

WIKI iliyopita mchezaji aliyetamba zaidi alikuwa David Molinga wa Yanga. Sio kutamba uwanjani. Kutamba nje ya uwanja. Huwa inatokea mara chache kwake kutamba uwanjani. Ana uwezo mkubwa wa kutamba nje ya uwanja. Molinga alisusa kwenda zake Shinyanga na Yanga ambayo juzi ilicheza na Mwadui na kushinda 1-0. Shukrani kwa bao la kiungo, Mapinduzi Balama. Nadra kwa washambuliaji wa Yanga kufunga siku hizi. Ndio ukweli wenyewe huo.

Kwanza kabisa Molinga alikimbilia katika vyombo vya habari. Nasikia mkataba wake hamruhusu kufanya hivyo. Tayari lilikuwa kosa lakini tuliweke kando kidogo. Kwanini alisusa? Inasemekana sio mara ya kwanza. Katika vyombo vya habari alimshutumu sana kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwassa kwamba hampendi. Ilishangaza kidogo. Mkwassa ndiye aliyempa nafasi mara kwa mara licha ya mashabiki kudhani kwamba, Molinga angeondoka na kocha wake wa zamani, Mwinyi Zahera ambaye ndiye alimleta nchini.

Kitu cha kushangaza, kocha mkuu wa Yanga, Luc Emely alipotua nchini aliamua kumbeba Molinga na kwenda naye Shinyanga. Hapa inamaanisha kwamba kocha mkuu aliamua kuwa na nguvu bila ya kujali hisia za msaidizi wake wala viongozi waliokuwa hapa.

Nasikia kutua kwake katika kambi ya Yanga kulipeleka mpasuko ambao uliwafanya baadhi ya mastaa kama, Lamine Moro kutaka kumsusia Molinga timu. Molinga akakiri kosa na kuomba msamaha. Hapa unajiuliza, kwanini kocha mkuu alimbeba mtovu wa nidhamu?

Hii inatoa picha moja kubwa. Kwamba kocha mkuu na Msaidizi hawana mawasiliano na hawana mwelekeo mmoja. Kama Luc angekuwa na msaidizi wake kutoka Ubelgiji halafu akamuacha Dar es Salaam, lazima kungekuwa na mawasiliano kati ya Luc na msaidizi wake kuhusu kilichotokea kwa Molinga.

Hii ndio hasara ya kocha mkuu na msaidizi kujikuta katika kapu moja kila mmoja akitokea katika njia yake. Kama Mkwassa angekuwa chaguo la kwanza la Luc basi ni wazi kwamba, wangekuwa marafiki na kungekuwa na uhusiano mkubwa wa kikazi baina yao.

Advertisement

Kifupi ni kwamba ambacho Mkwassa hakipendi basi na Luc naye angelazimika kutokipenda. Leo Molinga yuko kambini Shinyanga akimsikiliza zaidi Mzungu na sio Mkwassa. Hii ni wazi kwa sababu Molinga alisema wazi kwamba Mkwassa hampendi.

Lakini, jaribu kuona nguvu ya mtovu wa nidhamu katika timu. ilikuwaje akaingia katika pambano la juzi? Inaonyesha Mzungu hajajali kabisa kilichotokea kati Mkwassa na Molinga. Nadhani Mzungu kama asingekuwepo nchini basi Molinga asingekaa benchi hata kama angepelekwa na ndege na viongozi. Hilo lipo wazi. Lakini, Yanga ipo ovyo ovyo sana kwa sasa, haiendeshwi kama taasisi. Tulimsikia Meneja wa timu, Abeid Mziba na msemaji wa Yanga, Hassan Bumbuli jinsi ambavyo Molinga aliwagomea. Hata hivyo, Afisa habari mwingine wa Yanga, Antonio Nuggaz aliondoka na Molinga kwa mbwembwe katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam huku akijinasibu kwamba yeye ndiye aliyefanikisha mambo.

Maelewano kati ya Nuggaz na wenzake yako ovyo. Sijui kwanini hakusimama upande wa wenzake. Au hata kama yamekwisha, sijui kwanini alijinasibu vile katika vyombo vya habari wakati wenzake walikuwa wameongea tofauti saa 24 zilizopita.

Lakini, hili la Molinga nalo linatukumbusha jinsi Yanga ilivyoanguka. Imeanguka kweli kweli uwanjani. Mshambuliaji mwenye mabao nane tu katika Ligi anawasumbua kweli kweli. Ana mabao nane katika mechi nyingi tu.

Vipi kama yeye angekuwa ni Mohamed Hussein Mmachinga aliyefunga mabao 26 ya Ligi ndani ya msimu mmoja angefanyaje? Si angetaka akodiwe ndege binafsi kwa ajili ya kuungana na timu Shinyanga? Wamepita akina Edibily Lunyamila, lakini hawakuipelekesha timu hivi. Leo mchezaji mmoja mzito uwanjani, anayekosa mabao bado anaipasua Yanga. Achana na akina Mmachinga, Molinga hajafikia hata kiwango cha akina Herritier Makambo au Amis Tambwe ambao wameondoka Yanga hivi karibuni.

Natazamia wataachana naye mwishoni mwa mkataba wake, lakini vipi kama Luc akisema anataka kuwa naye? Nadhani Yanga watabakiwa midomo wazi. Watakuwa na nguvu ya kumdhibiti kocha wakati juzi tu amewaonyesha nguvu yake katika sakata hili?

Simba wameanza kuficha mambo yao vema. Sidhani kama wao ni malaika lakini kwa sasa nadhani wameanza kuficha mambo yao kama taasisi yenye mwelekeo bora wa kiungozi. Wala wanajijua wanavyokwenda wenyewe na kuna usiri mkubwa katika uendeshaji wa mambo yao.

Yanga wanakwenda katika mchakato wa mabadiliko wakiwa hoi kama taasisi. Hakuna nidhamu katika timu. Molinga amefichua tu jinsi ambavyo mambo yanakwenda ovyo ovyo kwa sasa pale Jangwani.

Advertisement