JICHO LA MWEWE : Nguvu kumhalalisha Molinga inachekesha

Muktasari:

Makocha na viongozi wanashirikiana kuwajua wachezaji ambao, wanawahitaji na wanaweza kuwasajili mwishoni mwa msimu. Papaa Zahera huwa anawaaga tu Yanga na kuwaambia ‘Nakwenda kuleta mshambuliaji’. Inachekesha kidogo.

MPIRA wetu una matatizo gani? Kuna mahala tumekwama. Huwa namsikiliza Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera anavyotetea wachezaji wake anaowaleta nchini. Alianza kwa kipa anayeitwa Kindoki. Sasa hivi ameamua kumpigania mshambuliaji wake, David Molinga.

Majuzi Molinga alifunga mabao mawili katika pambano dhidi ya Polisi Tanzania na mtu aliyepumua zaidi ni Zahera. Kwanini ajiweke katika nafasi ya kutoa machozi na damu kwa ajili ya mchezaji ambaye watu hawamfahamu?

Zahera anatumia nguvu nyingi kwa sababu amemleta mchezaji ambaye viongozi wake, mashabiki wa Yanga, na waandishi wa habari hawana uhakika naye. Swali linarudi palepale. Kwanini alete mchezaji ambaye anamfahamu yeye tu peke yake?

Mfumo wetu wa usajili upo ovyo. Kwanza kabisa huwa tunasaka wachezaji wakati dirisha la uhamisho limefunguliwa. Wenzetu wanasaka wachezaji wakati michuano mbalimbali ikiendelea. Wanakwenda kuskauti wachezaji.

Makocha na viongozi wanashirikiana kuwajua wachezaji ambao, wanawahitaji na wanaweza kuwasajili mwishoni mwa msimu. Papaa Zahera huwa anawaaga tu Yanga na kuwaambia ‘Nakwenda kuleta mshambuliaji’. Inachekesha kidogo.

Matokeo yake Zahera anakwenda kumchukua mchezaji, ambaye anamfahamu yeye mwenyewe tu. Mchezaji amefika akiwa mzito. Unajiuliza, timu kubwa kama Yanga ina muda wa kumsubiri mchezaji mpya tegemeo apungue uzito kwanza ndipo ipate matunda?

Kuna tofauti kati ya mchezaji aliyeongezeka uzito akiwa ndani ya klabu, na mchezaji mpya anayewasili akiwa mzito. Huyu Molinga amewasili klabuni akiwa mzito. Ina maana hakujiandaa kuja Yanga.

Lakini, hapo hapo kama alikuwa anakuja kwa ajili ya kuchezea Yanga, ina maana Yanga hawatambui ukubwa wao na kwamba ni timu yenye ushindani mkubwa ndani ya kikosi na haina muda wa kumsubiri mchezaji mpya awe fiti kwa muda wake?

Dunia ya leo ina washambuliaji kibao walio fiti na wanaosaka timu. Yanga haikuwaona kwa sababu ama haina pesa na inataka wachezaji wa bure, au inaburuzwa na Zahera. Kwanini aletwe mchezaji, ambaye kocha anatumia nguvu kubwa kumtetea kuwa atakuja kuwa mzuri baadaye.

Kwa Kindoki, Zahera alipambana kupitiliza. Katika kutaka kuhalalisha uzuri wa Kindoki ingawa watu tulikuwa tunafahamu kwamba alikuwa mbovu, kuna hadi maneno yakapenyezwa kwamba Yanga ilikuwa haina kocha mzuri wa makipa. Yote hii ilikuwa ni harakati za Zahera kumtetea Kindoki.

Tatizo hili la usajili wa magumashi limefanywa hata na watani zao Simba. Wabrazil watatu wa Simba walipofika tulipowauliza viongozi ‘marafiki zetu’ kuhusu ubora wa wachezaji wao majibu yake yalikuwa yanachekesha sana. Wangejibu ‘Mmoja anaonekana yuko vizuri kidogo’. Hivi kwanini tunabahatisha? Vipi kwa hao wawili wengine wakoje?

Kilichoonekana ni kwamba Wabrazil hao walinunuliwa kwa jicho la bosi mmoja tu mwenye pesa zake. Viongozi na kocha wa Simba, Patrick Aussems hawakupata kuwaona hao wawili wengine wakicheza soka hapo kabla. Kweli tupo makini?

Mchezaji kuchemsha katika jezi ya klabu fulani kubwa ni kitu cha kawaida. Wilfried Zaha alichemsha akiwa na Manchester United. Lakini, watu walifahamu uwezo wake akiwa na Crystal Palace na hata Sir Alex Ferguson alipomnunua alitumia macho ya watu wengine kuhalalisha manunuzi yake.

Hata Adam Salamba aliponunuliwa na Simba mashabiki wa Simba na viongozi wengi walikubali kununuliwa kwake. Mambo hayajaenda sawa na watu wote wameona na wameridhika kwamba, walinunua mchezaji wa maana ambaye hakuweza kumudu ushindani wa namba Simba au vinginevyo.

Lakini, kwanini Zahera na wajanja wachache wanaanza kuchukua mchezaji kwa kutumia jicho la mchezaji mmoja na kisha mtu huyo huyo aliyemleta anaanza kutumia nguvu kuhalalisha ubora wake? Dunia imeishiwa wachezaji kiasi hiki? Sitaki kabisa kuamini hili.

Mwisho wa siku, mchezaji wa aina ya Molinga kama alikuwa katika mipango ya kuchukuliwa na Yanga basi angewekwa katika majaribio na kisha katika programu maalumu ya kupunguza mwili kabla ya kuingia katika kikosi cha kwanza.

Angeweza kukaa na Yanga akifanya programu mbalimbali za kuwa fiti kabla ya kuchukuliwa katika dirisha la Januari. Wakati huo nafasi yake ingekuwa imechukuliwa na mchezaji, ambaye alikuwa yuko fiti na ubora wa kuitumikia Yanga katika mashindano mbalimbali.

Kitu hiki hiki nawalaumu Simba kwamba, kwanini hao Wabrazil wengine wawili ambao inaelezwa kuwa ni wachezaji wa kawaida nafasi zao zisingekwenda kwa wazawa walio fiti au wachezaji wa kigeni walio fiti na uwezo zaidi na badala yake wakapewa mkataba kabla ya kuonyesha uwezo wao kwa macho ya wote?

Mpira wetu bado unaendeshwa kijanjakijanja sana. Simba na Yanga sio timu za majaribio kutokana na ukongwe wao.

Sio timu za kuandaliwa nafasi ukiwa mchezaji mgeni halafu ukasubiriwa uwe fiti ndipo uonyeshe makali yako.

Ni timu ambazo unapaswa kuingia ukiwa hauna kasoro na kuonyesha makali yako moja kwa moja. Labda kwa sababu wachezaji wamepotea nchi hii lakini, zamani hatukuwa na majaribio ya wachezaji kama akina Molinga.

Ushindani ulikuwa mkubwa.