It’s Not Over… Mnyama anachapa

Muktasari:

UNAAMBIWA kabla Manchester United na Liverpool hazijashuka Uwanja wa Old Trafford kuvaana katika Ligi Kuu ya England (EPL), mashabiki wa Simba watakuwa tayari wanashangweka kwa chama lao kutimba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

UNAAMBIWA kabla Manchester United na Liverpool hazijashuka Uwanja wa Old Trafford kuvaana katika Ligi Kuu ya England (EPL), mashabiki wa Simba watakuwa tayari wanashangweka kwa chama lao kutimba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ndio, Simba itashuka Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni kuikaribisha Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya ligi hiyo ya Afrika ikiwa na faida ya ushindi wa mabao 2-0 iliyopata ugenini.

Kwa namna Kocha Didier Gomes na wasaidizi wake walivyojipanga na mzuka walionao mastaa wa Simba ni wazi hakuna kitakachoizuia isiandike historia nyingine ya kuwa timu ya kwanza nchini kucheza makundi ya Afrika mara mbili mfululizo. Msimu uliopita ilitinga hatua hiyo na kwenda hadi robo fainali na kutolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, lakini hakujawahi kutokea timu ya Tanzania kufuzu makundi mfululizo katika michuano yoyote ya Afrika kwa ngazi ya klabu.

Simba inahitaji sare tu leo isonge mbele, lakini kwa jinsi ilivyokuwa ikijifua mazoezini Uwanja wa Boko Veterani, ni wazi mnyama haachi kitu na Galaxy inapasuka tena, japo bado inatakiwa kuingia uwanjani na tahadhari ili kulinda rekodi yao ya kutimiza siku 3,171 ikiwa nyumbani bila kupoteza mechi yoyote ya michuano hiyo ya Afrika.

Simba ilifungwa mara ya mwisho CAF Februari 17, 2013 ilipolala 1-0 kwa Recreative do Libolo ya Angola na kukaa miaka mitano bila kushiriki michuano hiyo kabla ya kurejea na kasi mpya miaka mitatu iliyopita ikicheza mechi 13, ikishinda 10 na kutoka sare tatu tu.


GOMES AMALIZA KAZI

Katika mazoezi ya Simba tangu irejee kutoka Botswana, Kocha Gomes amekuwa akikomalia wachezaji wake kutumia mipira ya krosi na friikikii, huku washambuliaji na viungo wakipewa mbinu za kutupia nyavuni, kitu kinachoiweka Galaxy kwenye wakati mgumu leo.

Lakini ukiondoa hilo, ndani ya uwanja, Simba inaonekana kujipanga vyema kimbinu ili kushinda kwa jinsi benchi la ufundi lilivyoisoma Galaxy katika mchezo uliopita.

Mbinu ya kupiga pasi fupi za harakaharaka katika kujenga mashambulizi ndio inaonekana itakuwa silaha ya kwanza kwa Simba leo, japo inaweza kubadilika kulingana na namna Galaxy itakavyocheza.

Gomes alisema anajua wapinzani wao wamekuja nchini na nia ya kutaka kupindua meza baada ya kichapo cha nyumbani, ila amejipanga vyema kuhakikisha wanatimiza lengo la kutinga makundi kwa mara nyingine kabla ya kuanza hesabu za kufika mbali zaidi msimu huu.

“Mechi haijaisha, ndio maana nakazania kuwapa mbinu vijana wangu ili kuhakikisha tunawapa furaha mashabiki wetu. Sio mechi rahisi kwani wapinzani wetu nao ni wazuri,” alisema Gomes, huku msaidizi wake. Hitimana Thierry anayeisimamia timu katika michuano hiii kutokana na Gomes kupigwa ‘stop’ na CAF, aliongeza; “Tumewaona Galaxy katika mchezo wa awali, pia tumetazama mechi zao nyingine. Ni timu nzuri, hivyo lazima tujiandae vyema kukabiliana nao tupate ushindi nyumbani.”

Kinachoipa jeuri Simba ni kuingia katika mchezo huo wakiwa na kikosi kilichokamilika japo itamkosa Chris Mugalu aliye majeruhi.

“Wachezaji wote wako fiti kwa mechi hii na yeyote anaweza kupangwa na akafanya vizuri,” alisema Hitimana.


MASTAA MZUKA MWINGI

Mastaa wa Simba wameonekana kuwa na mzuka mwingi mazoezini wakionyesha kiu ya kutaka kuwapa raha mashabiki wao na beki Shomari Kapombe kwa niabaya ya wenzake alisema wapo tayari kwa vita na anaamini watashinda ili waingie makundi.

Kapombe alisema mashabiki wanatakiwa wawe na imani nao na hawatawaangusha kwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika uwanja wa nyumbani.

“Tunaingia kwenye mchezo huu kama tunaanza moja, tumeshasahau kabisa matokeo tuliyoyapata ugenini,” alisema Kapombe na kuongeza;

“Mabao ya mapema kule ndio ilikuwa mbinu ya mchezo ule, naamini kocha atakuja na mbinu nyingine nyumbani na mashabiki wasiwe na hofu tumejianda kuwapa furaha.”

Kama Simba itaitupa nje Galaxy, basi kuna mastaa tisa wataandika historia Msimbazi kwa kufuzu maakundi mara tatu wakiwa na kikosi hicho ambao ni Aishi Manula, Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, John Bocco, Mzamiru Yassin, Medie Kagere na Jonas Mkude

Akizungumzia hilo, Kapombe alisema linawapa ari na hamasa zaidi ya kupata ushindi leo

“Kiukweli kwetu ni jambo kubwa na linatupa nguvu zaidi ya kupambana, ila hata kwa wachezaji wengine wanatamani tupate ushindi ili nao waweke historia ya kucheza hatua hii kubwa ambayo inazipa heshima timu na wachezaji,” alisema Kapombe.


REKODI ZAIBEBA

Simba inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na historia nzuri ya kibabe katika michuano ya kimataifa ikicheza uwanja wa Benjamin Mkapa.

Tangu ilipofungwa na Recreativo Libolo ya Angola, Februari 17, 2013 hadi sasa, Simba imetimiza jumla ya siku 3171 bila kupoteza mechi yoyote ya mashindano ya CAF nyumbani kwani imecheza jumla ya mechi 13, ikishinda 10 na kutoka sare tatu, ikifunga pia mabao 29 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara matano tu.

Pia Simba imekuwa na historia ya kufanya vizuri dhidi ya timu za Kusini mwa Afrika inapokuwa nyumbani na ushahidi wa hilo ni mechi zao tano dhidi ya timu za ukanda huo, ikishinda nne na kutoka sare moja tu dhidi ya UD Songo ya Msumbiji. Imefunga jumla ya mabao 15 dhidi ya matatu iliyoruhusu na ushindi wao mkubwa nyumbani ni wa mabao 4-0 dhidi ya FC Platinum na ule wa 4-1 kwa Mbabane Swallows ya Uswatini, kisha kuipiga 3-1 Nkana ya Zambia na 3-0 Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, huku ililazimishwa sare ya 1-1 na UD Songo iliyowang’oa misimu miwili iliyopita.


WASAUZI WATUPU

Mchezo huo ulioruhusiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mashabiki 15,000 tu kuingia kwa Mkapa utachezeshwa na waamuzi wote kutoka Afrika Kusini ambapo kati atakuwa Abongile Tom, akisaidiwa na Elphas Sitole na Athenkosi Ndongeni watakaoshika vibendera wakati mezani mwamuzi wa akiba atakuwa ni Eugine Mdluli, huku Kamisaa akiwa ni Mzimbabwe Bryton Malandule.


MZIKI ULIVYO

Katika mchezo wa leo kikosi cha Simba kinaweza kisiwe na mabadiliko na kile kilichocheza mechi iliyopita jijini Gaborone, Botswana.

Kuna uwezekano mkubwa wa Wekundu hao kuanza na wachezaji walewale, langoni akisimama kipa Aishi Manula, akisaidiwa na mabeki Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Enock Inonga ‘Varane na Pascal Wawa ‘Sultan’, Lwanga Taddeo ‘Injinia’, Bernard Morrison ‘MB3’, Sadio Kanoute, John Bocco ‘Adebayor, Rally Bwalya na Hassan Dilunga ‘HD’.


Imeandikwa na Charles Abel, Thomas Ng’itu na Ramadhan Elias