Ishu ya Saido ipo hivi... wanne waachwa Dar

KIPA namba moja wa Yanga, Djigui Diarra amemaliza utata baada ya alfajiri ya jana kutua nchini na fasta akaungana na wenzake kwa safari ya kwenda Songea kwa mchezo wao dhidi ya KMC, huku Kocha Nasreddine Nabi akizidi kumtega kiungo mshambuliaji kutoka Burundi, Saido Ntibazonkiza.

Saido amekuwa hana namba kikosi cha Nabi, kutokana na kocha huyo kumpa kipaumbele Fiesal Salum ‘Fei Toto’ na kwenye msafara huo wa Songea uliondoka saa 4:30 asubuhi, nyota huyo wa kimataifa ni miongoni mwa wachezaji wanne walioachwa jijini Dar es Salaam.

Kuachwa kwa Saido kunazidi kumpa wakati mgumu Jangwani, kwani hali ni tofauti na ilivyokuwa aliposajiliwa akitokea Vital’O ya Burundi na alikuwa akianza na kuifungia timu hiyo mabao manne na kuasisiti matatu. Hata hivyo, moto alionao Fei Toto unamfanya aongeze juhudi kumshawishi Nabi.

Yanga tayari ipo Songea kwa mchezo wao wa kesho dhidi ya KMC ikiwa ni mfululizo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa imetua mjini humo na wachezaji 24, huku Saido, Yassin Mustafa, Dickson Ambundo na Mapinduzi Balama wakiachwa kwenye msafara huo.

Yanga itakuwa na mtihani dhidi ya KMC kwani katika mechi yao ya mwisho ya msimu uliopita, vijana wa Jangwani walijikuta wakilazimika kusawazisha bao kipindi cha pili baada ya wapinzani wao hao kutangulia kupata bao la dakika 28 likiwekwa kimiani na beki David Bryson aliyepo Yanga kwa sasa.

Bao la kuchomoa la Yanga la dakika ya 46 liliwekwa wavuni na Yacouba Songne, ingawa katika mechi ya awali Yanga ilishinda 2-1 jijini Mwanza, ikiwa ni miezi michache tangu wafumuliwa 1-0 na vijana hao wa Kinondoni lililowekwa na Salim Aiyee katika msimu wa 2019-2020.

Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Yanga Hafidh Saleh alisema timu yao imeshafika Songea baada ya kuondoka Dar na jumla ya wachezaji 24, huku akithibitisha kuwaacha nyota wanne akiwamo Saido.

“Nyota wote walioondoka na timu wapo kwenye hali nzuri ya mchezo na wanawaheshimu wapinzani wao wamejiandaa kwa ajili ya kuendeleza mazuri waliyoyafanya katika michezo miwili ya mwanzo,” alisema.

Kuhusu walioachwa Saleh alisema wote ni majeruhi isipokuwa Saido aliyeshindwa kufanya mazoezi na wenzake tangu amerudi kutoka kuitumikia timu yake ya taifa, hivyo kocha Nabi hajaona umuhimu wa kuondoka naye kwenda kwenye mechi hiyo ya kesho kwenye Uwanja wa Majimaji.

Naye nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alisema baada ya mapumziko kupisha michezo ya kufuzu kushiriki kombe la Dunia kwa timu ya Taifa sasa wameungana pamoja kama timu na wanatarajia mazuri kuelekea mchezo huo.

“Tumeanza vizuri kwa kushinda michezo miwili ya mwanzo tunahitaji mwendelezo huo kwa kupata matokeo Jumanne. Tunawaheshimu wapinzani wetu lakini lengo letu ni moja tu, kukusanya pointi tatu muhimu,” alisema na kuongeza;

“Tumekamilika kila idara, tuna kikosi bora na kipana ambacho kila mchezaji anatamani kupata nafasi ili aonyeshe kile alichonacho hiyo ndio inaweza ikawa chachu ya mafanikio ndani na Yanga ya sasa.”

Nyota walioondoka na wanaendelea kujifua leo kwa mara ya mwisho ni pamoja na Diarra Djigui, Erick Johola, Ramadhan Kabwili, Mwamnyeto, Yannick Bangala, Dickson Job, Paul Godfrey, Kibwana Shomari, Shabani Djuma, David Brayson, Abdallah Shaibu na Adeyum Saleh.

Wengine ni Mukoko Tunombe, Khalid Aucho, Jesus Moloko, Farid Mussa, Zawad Mauya, Deus Kaseke, Ditram Nchimbi, Feisal Salum na washambuliaji Fiston Mayele, Heritier Makambo, Yusuf Athumani na Yacouba Songne.