Ishu ya penalti iko hivi
Muktasari:
- Alifafanua kwamba hali hiyo inapelekea mchezaji kutokuwa sawa na anapoenda kupiga anakuwa na sintofahamu
WIMBI la kukosa penalti limezidi kuwakabili nyota wa Yanga na hivi karibuni, Obrey Chirwa, amekuwa kinara akikosa penalti tatu, lakini staa wa zamani wa timu hiyo, Said Bahanuzi, amedai kuwa anajua kinachomtokea mpachika mabao huyo.
Bahanuzi aliwahi kukosa penalti dhidi ya Al Ahly mwaka 2014 na kufanya Yanga iondoshwe Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema kuwa kupiga penalti si jambo jepesi kwani mara nyingi mpigaji hukumbwa na presha pamoja na kimuhemuhe.
Alifafanua kwamba hali hiyo inapelekea mchezaji kutokuwa sawa na anapoenda kupiga anakuwa na sintofahamu hususani timu ikiwa inategemea ushindi kutoka kwenye mkwaju huo.
“Mchezaji anapokosa penalti haimanishi kwamba ni mpigaji mbaya, hilo mbona hata Mbwana Samatta liliwahi kumtokea alipaisha juu akiwa na Taifa Stars. Kunakuwa na presha kubwa sana wakati wa kupiga,” alisema.
Naye beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua, alisema mara nyingi presha ya kuwaza kama unakwenda kupata ama kukosa inachangia upigaji wa ovyo wa penalti.
“Si jambo rahisi, ni tofauti na watu wanavyoamini,” alisema Joshua.