Ilamfya anataka kurudi Simba

MSIMU wa Ligi Kuu Bara 2020/21 umemalizika huku timu na wachezaji wakirudi kujipanga kwa ajili ya msimu ujao na wale waliotolewa kwa mkopo wanarejea kwenye timu zao za zamani.

Mmoja wa wachezaji anayetaka kurejea alikotoka ni mshambuliaji wa Simba, Charles Ilamfya aliyekuwa anakipiga KMC kwa mkopo.

Akiwa ndani ya KMC mchezaji huyo amefunga mabao manne pekee, huku akibakiza mkataba wa miaka miwili Simba hivyo anahitaji kurudi kwenda kupigania namba na kina John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu.

Msimu uliopita, Bocco ndiye kinara wa mabao wa ligi akiwa amefunga bao 16, Mugalu amemaliza na mabao 15 wakati Kagere amefunga bao 13.

Ilamfya alisaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Simba akitokea KMC mwanzoni mwa msimu huu na kucheza mechi kadhaa kabla ya kurudishwa KMC kwa mkopo wakati wa dirisha dogo.

“Bado nina mkataba na Simba, mkataba wangu wa mkopo KMC umemalizika juzi, hivyo narudi Simba na wao ndio wataamua hatima yangu.

“Najua sasa Simba wana washambuliaji bora ambao kila mmoja kwa nafasi yake anafanya vizuri, lakini sio kigezo cha kushindwa kurudi pale na kufanya vizuri kwani uwezo ninao na nitaenda kuipambania Simba,” alisema Ilanfya.