Ihefu yafanya kweli Samia Cup, Mbeya City yabebeshwa zigo

Thursday August 04 2022
SAMIA PIC
By Saddam Sadick

Kyela. Ihefu imeanza vyema michuano ya kombe la Samia baada ya kuikandika Mbeya City bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Kipija wilayani hapa.

Mechi hiyo ambayo ni ya kwanza katika kundi hilo A, licha ya City kutumia wachezaji wa timu ya Vijana ((U-20), Ihefu haikujali kutokana na kuweka nyota wake wote waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao.

Timu hiyo ya wilayani Mbarali ilitumia vyema dakika za mapema kupata bao hilo lililofungwa na Joseph Mahundi dakika ya nane na kudumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Vijana wa City walionekana kutulia na kuonesha soka safi kwa kutibua mipango ya wapinzani wao na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa Ihefu kuondoka kibabe na alama tatu na kujiweka pazuri kwenye kundi lao A.

Hata hivyo licha ya ushindi huo, Ihefu watajilaumu kwa kushindwa kufunga mabao hasa kupitia kwa Chirwa na Kibaya ambao walipata nafasi kadhaa na kushindwa kuzitumia.

Baadhi ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia michuano hiyo wamewatupia lawama uongozi wa Mbeya City kwa kuwajazia wachezaji vijana tofauti na timu zingine zinazoshiriki mashindano hayo.

Advertisement

Halima Yusuph mdau wa soka na shabiki wa Mbeya City amesema timu hiyo haijawatendea haki kwani walijitokeza kuangalia wachezaji waliosajiliwa lakini wameambulia patupu.

"Sawa tumemuona Tshishimbi na Chirwa lakini hata Mbeya City walipaswa walete wachezaji wao tuone ni nani wamesajiliwa, hii inaondoa utamu wa mashindano" amesema Halima.

Naye Victor Dickson amesema kuwa michuano hiyo ni muhimu haswa kwa timu za Ligi Kuu ambazo siku chache zitaanza ligi na kwamba kanuni zingeweka masharti kwa timu zinazodharau michuano hiyo.

"Kwanza wamechelewa kufika uwanjani hadi mechi inaisha usiku, lakini bado wanaleta wachezaji wa timu ya vijana jambo ambalo si lengo la michuano hii, kimsingi wajitathimini" amesema Dickson.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Soka mkoani Mbeya (Mrefa), Lucas Kubaja amesema kitendo walichofanya City siyo cha kiungwana kwani kwa hali hiyo inaondoa ladha ya mashindano na kwamba wanaamini hakitajirudia.

"Hizi ni changamoto zimejitokeza kwa sababu inaondoa ladha ya michuano na malengo ya waandaaji FA na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, lakini tunashukuru limejadiliwa na limepata ufumbuzi halitajitokeza" amesema Kubaja.

Advertisement