Ihefu yaanza kuisoma Simba

Muktasari:

  • Ihefu baada ya kumaliza kuichapa Azam bao 1-0 mchezo uliopita wa Ligi Kuu katika Uwanja wa Highland Estates, Mbarali Marchi 13 vijana hao walipewa mapumziko mafupi.

MBEYA. KATIKA kuhakikisha Ihefu FC inakwenda kushinda mchezo wa robo fainali wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) utakaopigwa mapema mwezi ujao dhidi ya Simba na leo

Jumatatu timu hiyo inarejea kambini kwaajili ya kuanza mazoezi.
Ihefu baada ya kumaliza kuichapa Azam bao 1-0 mchezo uliopita wa Ligi Kuu katika Uwanja wa Highland Estates, Mbarali Marchi 13 vijana hao walipewa mapumziko mafupi.

Afisa Habari wa Ihefu, Peter Andrew alisema baada ya mapumziko hayo wanaamini yatawafanya wachezaji kuwa na morali nzuri ya ushindani katika mchezo ujao.

"Kila mmoja anahitaji mapumziko anapofanya kazi ili aweze kurejesha nguvu na tunaimani baada ya siku kadhaa wachezaji na benchi la ufundi watakuwa wamefikia lengo la program yao.

"Hii ni hatua kubwa kwetu kufika robo fainali ndio maana tunahitaji kuweka nguvu nyingi huko ili tuweze kusongo mbele zaidi kwenye mashindano haya makubwa," alisema Andrew.
Hata hivyo kocha wa Ihefu, Zuberi Katwila alisema utakuwa mchezo mgumu kwao kutokana na umuhimu wa mchezo huo hasa kwa timu zote mbili kuwa na malengo yao.

"Tunajua tutakutana na ushindani mkubwa sababu ya uimara wa vikosi lakini tumejipanga kufanya vyema katika mchezo huo ili kufika mbali zaidi kwenye mashindano haya.

"Wachezaji wapo vyema na tutaendelea na mazoezi yetu kama kawaida tunavyofanya siku zote tunapokuwa na michezo sababu tukimaliza mchezo wa ASFC tunakutana nao wenye ligi," alisema Katwila.

Katibu Mkuu wa Ihefu, Zagalo Chalamila alisema uongozi imara waliokuwa nao wa kuhakikisha timu inakuwa bora ndio sababu ya wao kufanya vyema masimu huu.

"Kuna mahali tuligundua tumekosea ndio maana msimu uliopita tukashuka daraja lakini msimu huu baada ya kuanza vibaya ikatupasa tukae chini na kujipanga," alisema Chalamila.