Idriss Mbombo anakiwasha Zambia, abeba tuzo ya ufungaji bora

Muktasari:
- Mbombo ambaye alijiunga na Nkana Januari 2024 akitokea Azam FC, amemaliza ligi akifunga mabao 13 sawa na Titus Chansa wa Power Dynamos ambao wote wameshinda tuzo hiyo.
MSHAMBULIAJI wa Nkana FC, Idriss Ilunga Mbombo, ametwaa Tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Soka Zambia maarufu MTN Super League Football msimu wa 2024-2025.
Mbombo ambaye alijiunga na Nkana Januari 2024 akitokea Azam FC, amemaliza ligi akifunga mabao 13 sawa na Titus Chansa wa Power Dynamos ambao wote wameshinda tuzo hiyo.
Katika usiku wa utoaji tuzo za MTN Super League Football, sherehe zilizofanyika jana Mei 30, 2025 Garden Court, Kitwe, Mbombo alikuwa miongoni mwa waliokabidhiwa tuzo yake.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ameisaidia Nkana FC kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zambia.
Mbombo raia wa DR Congo, aliitumikia Azam aliyojiunga nayo Julai 2021 akitokea El Gouna ya Misri, kisha akaondoka Januari 2024 akirejea Zambia na kutua Nkana alipo sasa huku mkataba wake ukimuweka kikosini hapo hadi Juni 2026.