Ibenge aishtukia Simba

WAKATI Msimbazi ikikiri kwamba ni ngumu kumpata Kocha Florent Ibenge wa AS Vita na timu ya taifa ya DR Congo, kocha huyo amevunja ukimya juu ya taarifa za kila mara za kutakiwa Simba pamoja na klabu nyingine nchini ikiwamo Yanga na Azam, huku akiishtukia klabu hiyo.

Mwanaspoti imebaini kuwa Simba, Yanga na hata Azam zimekuwa zikimmezea mate Ibenge, lakini dau lake hasa mshahara ni jambo linalowakatisha tamaa, kwani imebainika kocha huyo ndani ya Vita anavuta mshahara wa mwezi wa Dola 15,000 ambazo ni zaidi ya Sh 34 milioni.

Mbali na mshahara, pia posho anazopata ndani ya klabu hiyo na hata timu ya taifa ya DR Congo imemfanya Ibenge awe mgumu kutoka kwao, japo juzi alipoulizwa kuhusu tetesi za kutakiwa Simba alisema yupo tayari kufanya kazi kokote, kama klabu za Tanzania zinamhitaji kweli.

“Nimeona tetesi nikihitajika na timu hizo na ni jambo zuri kwangu, lakini bado nina mkataba na klabu yangu ya AS Vita na DR Congo na sipendi kuziongelea sana tetesi kwani kilichonileta hapa sicho hicho. Ila naamini ipo siku naweza kuja Tanzania kufundisha moja ya timu hizo.”

AISHTUKIA

Kuhusu kupangwa tena na Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Ibenge alisema kundi lao ni gumu, huku akikiri kuwa Wekundu wa Msimbazi ni bora na wanaweza kuwasumbua.

“Simba ni timu nzuri nakumbuka tuliifunga nyumbani, lakini tulipokuja hapa walitufunga na kutufanya tushindwe kusonga mbele, hivyo tupo kwenye kundi gumu,” alisema Ibenge.

Katika msimu wa 2018-2019 timu hizo ilipangwa kundi moja na Al Ahly na JS Saoura na katika mechi yao ya kwanza ugenini, Simba ilifungwa mabao 5-0 kisha nao kushinda nyumbani 2-1 na kufuzu robo fainali wakiiacha AS Vita na JS Saoura zikikwama.

Ibenge alisema anaamini mechi za msimu huu zitakuwa ngumu kwani kuna mabadiliko makubwa kwa timu zote, huku akisisitiza Simba inaweza kuwasumbua kwa namna ilivyo sasa akidai amekuwa akiifuatilia na kuona ilivyoimarika zaidi.

Simba itaanza mechi zao za Kundi A iliyoapngwa pia na Al Merreikh ya Sudan ugenini kwa kuvaana na AS Vita Februari 12 kabla ya kurudiana nao Machi katika moja ya mechi zao mbili za mwisho kumaliza hatua hiyo ya makundi kuwania kutinga robo fainali.