Prime
Huyu ndiye kocha mpya wa Yanga, rekodi zake zipo hivi...
Muktasari:
- Uteuzi wa kocha huyo raia wa Afrika Kusini, umekuja baada ya Mei 6, 2026 Yanga kuachana na Pedro Goncalves, kisha kikosi hicho kunolewa kwa muda na Abdihamid Moallin aliyefanikiwa kutetea taji la Ligi Kuu ya NBC.
KLABU ya Yanga, leo Julai 10, 2026 imemtambulisha Manqoba Mngqithi kuwa kocha mkuu wa kikosi cha timu hiyo.
Uteuzi wa kocha huyo raia wa Afrika Kusini, umekuja baada ya Mei 6, 2026 Yanga kuachana na Pedro Goncalves, kisha kikosi hicho kunolewa kwa muda na Abdihamid Moallin aliyefanikiwa kutetea taji la Ligi Kuu ya NBC.
MANQOBA NI NANI?
Jina lake kamili ni Manqoba Brilliant Ferrimant Mngqithi, miongoni mwa makocha wenye heshima kubwa sana katika soka la Afrika Kusini.
Akiwa na zaidi ya miongo miwili ya uzoefu katika ukocha, amejijengea sifa kama mmoja wa wataalamu mahiri wa mbinu za mchezo, kiongozi mwenye maono na kocha aliyetwaa mataji mengi katika historia ya soka la Afrika Kusini.
Mzaliwa huyo wa Aprili 25, 1971, katika eneo la Umzimkhulu, mkoani KwaZulu-Natal, Mngqithi hakuanza maisha yake akiwa uwanjani.
Awali alikuwa mwalimu wa shule, lakini mapenzi yake kwa soka yakamshawishi kuachana na taaluma hiyo na kujitosa kwenye ukocha.
Uamuzi huo uliibadilisha kabisa historia ya maisha yake na baadaye akapata Leseni ya UEFA A, moja ya leseni zinazotambulika katika ukocha wa soka.
Safari yake ilianzia katika klabu za Maritzburg City, Moja United, Highlanders na timu ya Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal kabla ya kupewa nafasi ya kuinoa Golden Arrows mwaka 2007.
Ndani ya kipindi kifupi alionyesha uwezo mkubwa wa kiufundi na mwaka 2009 akaandika historia kwa kuiongoza Golden Arrows kutwaa ubingwa wa MTN8 baada ya kuichapa Ajax Cape Town mabao 6-0katika fainali, ushindi ambao bado unatajwa kuwa miongoni mwa matokeo makubwa zaidi katika historia ya mashindano hayo.
Baada ya mafanikio hayo, aliendelea kujenga wasifu wake kupitia klabu za AmaZulu na Chippa United kabla ya kurejea Golden Arrows.
Hata hivyo, hatua kubwa zaidi katika maisha yake ya ukocha ilifika mwaka 2013 alipoungana na Mamelodi Sundowns.
Akiwa Sundowns, alianza kama kocha msaidizi chini ya Pitso Mosimane na baadaye akafanya kazi pamoja na Rhulani Mokwena.
Katika kipindi hicho alikuwa sehemu muhimu ya benchi la ufundi lililoiongoza Sundowns kuwa moja ya klabu bora Afrika kwa kutwaa mataji ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, CAF Champions League mwaka 2016 na CAF Super Cup mwaka 2017.
Mwaka 2020 alipandishwa kuwa kocha mkuu wa pamoja (co-head coach) sambamba na Rhulani Mokwena, huku wawili hao wakiiongoza Sundowns kutwaa mataji mawili mfululizo ya ligi.
Baadaye aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo mwaka 2024, lakini akaondoka mwishoni mwa mwaka huo baada ya matokeo kutokidhi matarajio ya uongozi wa klabu.
ANA MATAJI 11
Katika maisha yake ya ukocha, Mngqithi ameweka rekodi ya kutwaa jumla ya mataji 11 makubwa. Ameshinda Ligi Kuu ya Afrika Kusini mara tano, CAF Champions League mara moja, CAF Super Cup mara moja, Nedbank Cup mara moja, Telkom Knockout mara moja na MTN8 mara mbili. Kati ya hayo mataji 11, moja la MTN8 ameshinda akiwa Golden Arrows, huku yaliyobaki akiwa Mamelodi Sundowns.
FALSAFA YAKE
Mbali na mafanikio hayo, Mngqithi anafahamika kwa falsafa yake ya soka inayosisitiza umiliki wa mpira, uchezaji wa pasi nyingi na mashambulizi ya haraka kupitia mfumo wa 4-3-3.
Pia ni kocha anayependa kukuza vipaji vya vijana na kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao katika ngazi ya juu.
KUREJEA GOLDEN ARROWNS NA KUTUA YANGA
Machi 2025, alirejea kwa mara ya tatu kuifundisha Golden Arrows akiwa na jukumu la kuijenga upya timu hiyo.
Katika msimu wa 2025-2026 aliiongoza kumaliza nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini akiwa amekusanya pointi 41, jambo lililoonyesha kuwa bado ana uwezo mkubwa wa kushindana katika kiwango cha juu.
Licha ya kuondoka Golden Arrows mwishoni mwa msimu huo baada ya mkataba wake kumalizika, Mngqithi anaendelea kuwa mmoja wa makocha wanaoheshimika zaidi Afrika.
Rekodi yake ya mataji, uwezo wa kujenga timu na falsafa yake ya kisasa ya soka, ni sababu zilizowafanya mabosi wa Yanga kumchagua kwenda kuinoa timu hiyo inayohitaji kupambania mataji zaidi msimu ujao wa 2026-2027.
Pia, hitaji kubwa la Yanga ni kufanya vizuri mashindano ya CAF, baada ya 2022-2023 kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa kanuni ya bao la ugenini, sasa wanataka kubeba ubingwa wa CAF ambapo msimu ujao watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.