Huyu Morrison Yanga imesajili mcheza freestyle badala ya soka

TUPO msibani, legend supastaa wa NBA, Kobe Bryant, amefariki dunia juzi. Wakati huohuo anga la soka linapambwa na fundi madoido, Bernard Morrison wa Yanga. Yote yanajadiliwa kijiweni. Luqman Maloto na Dk Levy wanagombea microphone ili kujenga hoja.
LUQMAN: Pole kwa msiba Daktari.
DK LEVY: Kobe Bryant amekufa kibabe sana. Fikiria alikuwa kwenye helikopta kumpeleka mtoto wake mazoezini. Watu kama Kobe wanapokufa, hatupaswi kulia, tunatakiwa kusherehekea maisha yake. Wa kumsikitikia ni kale katoto kake ka Gianna. Kalikuwa na ‘fyucha’ ya kutuonesha. Kobe achana naye. Tusherehekee tu.
LUQMAN: Kwa hiyo Kobe amekupa hasira, sio huzuni au sio?
DK LEVY: Huzuni ipo, Gianna alikuwa binti mdogo na alikuwa na mengi ya kutuonesha. Kobe pia pengine angeendelea kuihudumia dunia kwa namna tofauti. Watu wengine watano waliofikwa na mauti kwenye ajali ya helikopta, kuna huzuni. Ila baada ya masikitiko, akili ikae mahali pake. Kobe alikuwa mtu, alikaa juu kabisa ya dunia. Kuna watu walicheza na wanacheza kikapu, Kobe hakucheza kikapu, alikichezea na kilimpa kila kitu. Kobe alipata kila ambacho kinaotwa na yeyote anayetamani kuwa staa wa kikapu. Ndio maana tangu Kobe alipostaafu na mimi siku hizi siangalii hizo mambo tena.
LUQMAN: Unapitwa kama huangalii NBA sasa hivi. NBA ina watu sana. Kumbe huoni mavitu ya King LeBron James, Steph Curry, Kevin Durant, Russell Westbrook, James Harden, Kyrie Irving, Klay Thompson, Andre Iguodala, sijui niendelee?
DK LEVY: Unamuuliza nani? Endelea kutaja vibenten vyako. Huyo umemwita King ndio hasa alinifanya niache kufuatilia NBA baada ya Kobe. Mtu mtoto sana, lakini anajipandisha mabega kujilinganisha na wanaume wa kweli. Hicho kibenten ulichokiita King, eti wanakifananisha na Michael Jordan, unataka baada ya hapo nifurahie kikapu NBA? Kilichonivutia kutazama kikapu ni kwa sababu wanaume walikuwa wakicheza. Jordan, Kobe, Dennis Rodman, Scottie Pippen, Larry Bird, Magic Johnson, halafu kuna lile jitu kubwa Shaquille O’Neal.
Sasa utamlinganisha Kevin Durant na Larry Bird? Au Iguodala na Scottie Pippen? Thubutu kumlinganisha LeBron wako na Magic Johnson nikuchabange makofi sasa hivi. Nilipenda kuangalia kikapu kwa sababu kilichezwa na big men kwenye court, sio sasa hivi mnatujazia vibenten uwanjani, halafu anayeonekana ni bora mbele ya watoto wenzake, anajiita King. Huo ujinga peleka hukohuko.
LUQMAN: Hayo yote yameletwa na msiba wa Kobe au kuna lingine? Chuki zako ni King James kutakata? Funguka.
DK LEVY: Ukiendelea kuiita hiyo simbilisi inayopenda kupayuka ni King hiki kikao kitavunjika sasa hivi. Huyo mpayukaji anacheza na watoto halafu anajisifu. Angeingia kukutana na wanaume kama Patrick Ewing tungeona kama angefurukuta. King ni mmoja, ni Jordan. Huwezi kumwita LeBron King wakati kuna Kobe ambaye alifanya mambo makubwa na hakuwa na kidomodomo. LeBron anachowazidi akina Kobe ni mdomo. LeBron ni big mouth kuliko Jordan, Kobe na wengine wote. LeBron hata mtoto mwenzie Kevin Durant akiwa kwenye kiwango chake huwa hatambi. Si uliona KD alipokuwa Golden State Worriers na LeBron akiwa Cavaliers, jinsi ambavyo LeBron hakufurukuta?
LUQMAN: Kumbe huwa unaangalia na unafuatilia, ulijiuaje kama KD alimfunika LeBron?
DK LEVY: Niulize leo timu gani imeshinda game nyingi Western Conference uone kama nitakujibu. Nishitukize kwa swali timu ipi inachechemea Eastern Conference uone kama utapata jibu. Kabla ya Kobe kustaafu kikapu, nilikuwa na taarifa za ligi ya NBA kwenye kila conference. Timu iliyofunga pointi nyingi. Mchezaji anayetisha kwa kutupia pointi tatu. Mchezaji mkali wa kucheza rebound, anayeasist sana na anayetumbukiza vikapu. Nilikuwa na rekodi zote. Ungenikuta nakesha kuangalia mechi za NBA. Sasa siku hizi ni nani wa kunishawishi kukesha? Hivyo vibenten vyako?
LUQMAN: Kaa na misimamo yako. Kizazi kimoja kinaondoka, kingine kinafuata. Huyo LeBron alianza kutikisa NBA Kobe akicheza, ila kwa vile umeamua kumponda, najua huwezi kuchagua maneno. Kama inakuuma shauri yako, yule anaitwa King James.
DK LEVY: Hivi utakuwa na akili lini? Huyo LeBron alimkuta Kobe katika zama zake? LeBron alitamba mbele ya Kobe kwa sababu wakati huo Kobe alikuwa ameshakuwa mtu mzima. Angemkuta na moto wake akaona. Wewe ni sawa na wanaosema Nandy ni mkali kuliko Jaydee kwa sababu sasa hivi Nandy anawika kuliko Jaydee. Wanashindwa kuvuta picha ni muda mrefu kiasi gani Jaydee amelitawala game kama vile hakuna mwingine wa kumpokea. Kibenten LeBron aling’ara mbele ya mwanaume Kobe kwa sababu mwanaume Kobe alikuwa amezeeka. Kama binadamu wangekuwa kama nyoka, unajichuna ngozi unarudi kuwa kijana, nakuapia usingemsikia LeBron wala Steph Curry. Maana wanaume halisi wangekuwa ulingoni mpaka leo.
LUQMAN: Sasa utaenda msibani kumzika Kobe au utakuwepo Dodoma kwenye shoo ya Jaydee miaka 20? Nafahamu wote hao ni watu wako.
DK LEVY: Kabla ya kufika huko, tafakari kuwa Kobe amekufa akiwa tajiri. Alikuwa na kila kitu. Anataka kumpeleka binti yake mazoezini, wanapanda helikopta. Hebu acha ujinga, waza na wewe kufa kibabe. Unakufa, familia inalia kukupoteza basi, sio inalia kukupoteza na ugumu wa maisha juu. Familia zetu, tukifa vilio ni vingi kwa sababu ya kufikiria magumu ya maisha baada yetu. Kobe ameacha kila kitu. Mkewe na watoto waliobaki, wanaumia kupoteza watu waliowapenda, hawalii baada ya mazishi wataishije. Hiyo ndio hamasa ya kuchukua. Sio unatoa macho.
LUQMAN: Sawa nimekulewa. Na nafahamu unazuga, ujanja wa kwenda kumzika Kobe huna, wewe saizi yako ni miaka 20 ya Lady Jaydee. Nasikia Yanga siku hizi wana kelele hao, kwamba kuna mchezaji amepata ujiko wa kutembea juu ya mpira. Dunia ina mambo hii.
DK LEVY: Anaitwa Bernard Morrison, mtoto kutoka Kumasi Ghana. Mpe mpira halafu kuhusu namna anavyouchezea na kutoa pasi, hilo mwachie yeye. Fundi sana yule jamaa. Nasikia wafugaji wa Simba wa pale Msimbazi wanaweweseka sana kwa habari za Morrison. Wafikishie pole zangu.
LUQMAN: Sasa pole ya nini? Mchezaji analeta michezo ya freestyle uwanjani kwenye soka na wewe unamsifia? Akina Messi, Ronaldo unadhani hawawezi kuufanya huo ujinga? Wanaweza sana, ila wanapokuwa kwenye mechi ni kazi kazi. Hiyo nafasi ya kuleta mbwembwe badala ya kutafuta magoli, ni ujinga mtupu. Ulimwona wapi Ronaldinho Gaucho anafanya yale maujinga ya Morrison? Mazoezini sawa. Katika freestyle it’s ok. Sio kwenye mechi kama alivyofanya Morrison kwa Prison. Kwa Morrison, Yanga wamechemka kusajili mchezaji wa freestyle, hatawapa matokeo, vinginevyo kocha amwonye kuacha mbwembwe acheze mpira na awe msikivu.
Mwenzake Chama wa Simba, alifikiri freestyle ndio soka, akaleta madoido, jukwaa linamshangilia. Kidogo apotee. Chezea mpira kama una sababu. Chezea mpira kwa faida ya timu yako. Sio kuchezea mpira kisa upo peke yako hakuna wa kukukaba, halafu unatoa pasi nyuma kwa madoido, badala kuitafutia nafasi timu yako ya kufunga magoli. Yule Morrison ni hasara jamaa yangu.