Huyu Miraji 'Sheva' mbona mtakoma Ligi Kuu Tanzania

Muktasari:
Ujanja wake wa kukaa katika nafasi sahihi na kutumia vyema nafasi uliirahisishia kazi Simba baada ya nyota huyo kupachika mabao mawili yaliyokuwa na umuhimu mkubwa katika mchezo huo.
Dar es Salaam. Simba walikuwa na mabadiliko kadhaa katika kikosi chao ambapo Tairone Santos, Gerson Fraga, Francis Kahata na Miraji Athuman walianza wakichukua nafasi za Clatous Chama, Ibrahim Ajibu, Erasto Nyoni na Sharaf Shiboub.
Mabadiliko hayo yalionekana kuipa uimara Simba ambayo ilionyesha kiwango bora katika mchezo huo kwa kumiliki mpira kwa muda mrefu na kutengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao tofauti na Ruvu Shooting ambayo ilikuwa ikishambulia kwa kushtukiza.
Mwamuzi Ludovick Charles kutoka Mwanza alijitahidi kulimudu pambano hilo kutokana na kuwa katika maeneo sahihi na kuyaona vyema matukio yaliyokuwa yakijiri ndani ya uwanja ingawa kuna nyakati alitetereka katika
Kwa upande wa wachezaji wa timu zote mbili kila mmoja kwa nafasi yake alitoa mchango wake katika kuhakikisha timu inapata matokeo na ifuatayo ni tathmini ya jinsi kila mchezaji alivyocheza katika mechi ya jana.
Ruvu Shooting
Mohamed Makaka-7
Aliinusuru timu yake isipigwe nyingi kama baadhi ya mechi zao za nyuma za Ligi Kuu mbele ya Simba, kwani jana aliokoa hatari nyingi zilizoelekezwa langoni mwake.
Aliipanga vyema safu yake ya ulinzi ingawa alikuwa na tatizo katika ukamataji wake wa mipira.
Omary Kindamba-5
Muda mrefu aliutumia katika kujilinda na alishindwa kupanda mbele kupandisha mashambulizi na mara kwa mara alikuwa akibutua mipira ambayo ilipotea kirahisi na kunaswa na wachezaji wa Simba.
Kassim Simbaulanga-3
Alishindwa kumdhibiti Francis Kahata na upande wake ndio ulikuwa ukitumiwa mara kwa mara na Simba katika kupitisha mipira kuelekea langoni mwa Ruvu Shooting.
Alifanya faulo za mara kwa mara ambazo laiti Simba wangezitumia wangeweza kufunga idadi kubwa ya mabao.
Renatus Morris-6
Alitumia vyema umbo lake lililojengeka kumdhibiti Meddie Kagere. Alihakikisha hampi nafasi mshambuliaji huyo wa Simba kuleta madhara langoni mwao
Rajab Zahir-6
Alikuwa na mawasiliano mazuri na Morris na alijitahidi kuokoa hatari zilizoelekezwa langoni mwake hasa mipira ya juu lakini alijisahau katika kumdhibiti Miraji Athuman kuifungia Simba bao la kuongoza.
Zuberi Dabi-5
Hakuilinda vyema safu yake ya ulinzi kwani alishindwa kuziba mianya ya Simba kupenyeza mipira jambo lililoiweka safu ya ulinzi ya Ruvu Shooting katika wakati mgumu mara kwa mara.
Emmanuel Martin-3
Hakushuka kumsaidia beki wake wa pembeni lakini pia kasi yake ilikuwa chini kiasi ambacho
Shaban Msala-2
Alishindwa kuiunganisha timu lakini pia hakumsaidia Dabi katika kutibua mipango ya Simba na alicheza rafu za mara kwa mara ambazo zilisababisha aonyeshwe kadi ya manjano.
Sadat Mohamed-5
Kutokana na kutopata huduma sahihi kutoka kwa viungo wake, alijikuta akitumia nguvu kubwa kusaka mipira lakini mara chache alizopata nafasi aliwasumbua walinzi wa Simba na alijitahidi kufanya mashambulizi ambayo hata hivyo hayakuzaa matunda.
Said Dilunga-3
Muda mwingi alilazimika kurudi nyuma kutafuta mipira na hakuwa na madhara pindi Ruvu Shooting ilipokuwa inashambulia na haikushangaza kuona akitolewa dakika ya 57 kumpisha Fully Maganga
Edward Christopher-5
Alimchosha beki wake wa pembeni kwani hakushuka kusaidia ulinzi lakini pia alikuwa na mchango hafifu katika kushambulia na alitolewa mnamo dakika ya 61 kutoa nafasi kwa Abdulrahman Mussa aliyeingia.
Simba
Aishi Manula-7
Hakupata mashambulizi ya mara kwa mara ingawa alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la Sadat Mohamed katika dakika ya 18 ambalo lingeweza Ruvu Shooting, bao la kuongoza.
Shomary Kapombe-8
Aliwaweka katika wakati mgumu Ruvu Shooting kutokana na kasi yake na krosi ambazo alikuwa akipiga ambazo mojawapo ilizaa bao la kwanza lililofungwa na Miraji Athuman.
Mohammed Hussein-6
Mara kwa mara alipanda mbele kushambulia kwa sababu hakupata upinzani changamoto kutoka kwa winga aliyekuwa anakabana naye.
Hata hivyo idadi kubwa ya krosi zake hazikuwafikia walengwa kwani ziliokolewa na safu ya ulinzi ya Ruvu Shooting.
Tairone Santos-8
Alikuwa na siku nzuri katika mchezo wa jana. Alikuwa imara katika kujilinda kwa kuondosha hatari zilizoelekezwa langoni mwake lakini pia alishiriki kushambulia mara kwa mara na jitihada zake zilizaa matunda kwa kufunga bao la pili la Simba katika dakika ya 47 akimalizia mpira wa kona wa Mohammed Hussein
Pascal Wawa-6
Kazi kubwa ilifanywa na Tairone na jukumu lake kuu lilikuwa ni kutoa sapoti kwa mwenzake lakini mara kwa mara alishiriki kuichezesha timu kuanzia nyuma.
Fraga Vieira-6
Aliilinda vyema safu ya ulinzi ya Simba kwa kuziba mianya ya Ruvu Shooting kupenya kwenda langoni mwa Simba na alihakikisha anakuwa wa kwanza kuucheza kila mpira aliowania na wapinzani.
Francis Kahata-7
Utulivu na uwezo wake wa kupiga pasi zinazofikia walengwa kwa usahihi ulimuweka katika wakati mgumu beki wa Ruvu Shooting, Kassim Simbaulanga ambaye alilazimika kumchezea faulo za mara kwa mara. Alitolewa dakika ya 80 baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Deo Kanda lakini alipika bao la tatu kwa kumpa pasi ya kichwa, Miraji Athuman aliyefunga kwa shuti la mguu wa kulia.
Mzamiru Yassin-6
Aliiunganisha vyema timu na kuichezesha huku akishirikiana na Fraga katika kuilinda safu yao ya ulinzi.
Alicheza bila kuchoka ingawa kuna nyakati alichelewa kufanya uamuzi pindi alipokuwa na mpira mguuni.
Meddie Kagere-5
Alikuwa na siku ngumu kutokana na kuwekewa ulinzi mkali na safu ya ulinzi ya Ruvu Shooting ambayo wakati mwingine ilimchezea rafu za kimyakimya lakini hata hivyo alionyesha uwepo wake kwa kushiriki katika kupika bao la tatu lililofungwa na Miraji.
Miraji Athuman-9
Ujanja wake wa kukaa katika nafasi sahihi na kutumia vyema nafasi uliirahisishia kazi Simba baada ya nyota huyo kupachika mabao mawili yaliyokuwa na umuhimu mkubwa katika mchezo huo.
Alikuwa tishio kwa walinzi wa Ruvu Shooting ambao walipata wakati mgumu kumdhibiti
Hassan Dilunga-6
Pamoja na kuwasumbua mabeki wa Ruvu Shooting, alikosa ubunifu wa kupiga pasi zenye madhara na badala yake alipiga pasi nyingi za pembeni ambazo ziliwafanya mabeki wa timu pinzani kujipanga na kuwahi kutibua mipango.
Walioingia
Fully Maganga-3
Hakupata nafasi ya kutoa mchango kwa timu yake kwani aliingia katika kipindi ambacho Simba ndio walikuwa wanatawala mchezo.
Moses Shaban-5
Alijitahidi kutibua mipango ya Simba kwa dakika 17 alizocheza lakini mwishoni alijikuta akipata wakati mgumu baada ya wapinzani wao kuongeza idadi kubwa ya wachezaji wenye asili ya kushambulia.
Abdulrahman Mussa-3
Alilazimika kurudi mara kwa mara kusaidia katika ulinzi jambo lililoipunguza nguvu ya Ruvu Shooting mbele.
Deo Kanda-6
Uwepo wake uwanjani uliwalazimisha Ruvu Shooting kubaki nyuma jambo lililoiweka Simba salama na kuweza kulinda ushindi wake.
Ibrahim Ajibu-7
Aliingizwa kwa jukumu la kuhakikisha Simba inakuwa na mpira na kupoteza muda ambalo alilifanya na muda mfupi aliocheza aliwahenyesha walinzi wa Ruvu.
Sharaf Shiboub-4
Dakika kumi alizocheza hazikumtosha kufanya makeke na alipoteza nafasi ya kufunga bao la nne baada ya kupiga kichwa kilichotoka nje.