Huyu mama alimdunda mtu ngumi akaangukia nje ya ulingo

Muktasari:

  • Wiki chache baadaye Wolfe alitetea ubingwa wake alipokutana na Valley kwa kumaliza pambano katika raundi ya sita akimuacha Valley hawezi kuzungumza.

KATIKA kila mchezo yapo matukio ya kushangaza na kuhesabika kuwa ni sehemu muhimu ya historia ya mchezo huo.

Miongoni mwao ni ile ya mwanamama wa Marekani, Ann Wolfe ambaye ameweka rekodi ya kunyakua ubingwa wa dunia wa ngumi za uzito wa viwango tofauti. Maelezo juu ya maisha yake na picha yapo katika ukumbi wa kimataifa wa wanamasumbwi wanawake uliopo nchini Marekani.

Mwanamama huyo ambaye sasa ana miaka 51 ni mkufunzi wa ndondi wa klabu mbalimbali za wanawake na hasa chipukizi. Miongoni mwa wanamasumbwi wa kike maarufu wanaotamba Marekani hivi sasa wamepitia katika mikono yake.

Wolfe ambaye alizaliwa Austin, Texas nchini humo na mama aliyehamia akitokea Oberlin, Louisiana alitumia muda wake mwingi wa utotoni barabarani kutokana na mama’ke kutokuwa na eneo la malazi ya uhakika.

Mama huyo alirudi Austin 1996 na watoto wake wawili wa kike. Baada ya kuwa hana makazi ya kudumu huku akifanya kazi ya kubeba makarai ya zege katika kampuni za ujenzi alikutana na mkufunzi wa ndondi ambaye alivutiwa na umbo lake na hasa misuli na kumtaka ajiunge na mchezo wa kupigana ndondi.

Alishiriki katika mashindano mbalimbali ya ngumi za ridhaa na baadaye kujiunga na ngumi za kulipwa. Katika ndondi za ridhaa alishiriki michezo minne na kushinda mitatu na kushindwa mmoja. Mwaka 1998 alishiriki katika mashindano ya ubingwa wa Marekani aliibuka bingwa baada ya kumshinda Tami Hendrickson wa Seattle kwa pointi 50 –39 katika nusu fainali, kisha akamfumua Shanie Keelan baada ya sekunde 46 tangu raundi ya kwanza ya mchezo.

Baadaye Wolfe alimshinda Vienna Williams kwa pointi na kubeba ubingwa wa Marekani wa ndondi wa viwango vya kati.

Kisha akakutana na Gina Nicholas wa nchini humo aliyejulikana kama ‘Radi Nyepesi’ na kuchukua ubingwa na uzito mwepesi wa kati (middle weight) ambao ulikuwa wazi.

Mwanamasumbwi aliyefuatia kupata kipigo kutoka kwa Wolfe ni Marsha Vaaley ambaye alivumilia makonde, lakini akajikuta analazimika kusalimu amri katika raundi ya sita ya pambano hilo la raundi 10 la uzani wa juu kuwania taji la uzito mwepesi (super middleweight).

Wolfe alikuja kulipiza kisasi cha kichapo alichopata kutoka kwa Mafoodh miaka michache kabla na kunyakua taji la ubingwa wa uzani wa juu wa uzito mwepesi (super middleweight) la Shirikisho la Ngumi Amerika Kaskazini (Naba).

Akiwa katika Jiji la Mississippi, Wolfe aliifikia rekodi ya Henry Armstrong ya kuwa bingwa wa mataji matatu tofauti alipochukua lile la Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (Iba) katika uzito mkubwa mwepesi (light heavyweight) kwa kumtoa nje ya ulingo katika raundi ya kwanza mchezaji nyota maarufu wa zamani wa mpira wa kikapu, Vonda Ward ndani ya dakika moja na sekunde nane.

Ward alipata mtetereko wa shingo kwa vile alipopigwa konde alirushwa nje ya kamba na kuanguka chini. Alipelekwa hospitali akiwa katika hali mbaya kutokana na maumvivu ya shingo na kichwa. Kipigo kile kinahesabiwa hadi hii leo ndicho kibaya zaidi katika historia ya ngumi za kinamama.

Wiki chache baadaye Wolfe alitetea ubingwa wake alipokutana na Valley kwa kumaliza pambano katika raundi ya sita akimuacha Valley hawezi kuzungumza. Mnamo Julai 19, 2005, Wolfe alimshinda Monica Nunez katika raundi ya saba walipokutana katika Jiji la Mississippi.

Wolfe alistaafu ngumi Agosti 20, 2005 kwa mara ya pili akimchapa Valerie Mafoodh kwa pointi katika pambano la raundi 10.