Huyu Kagere ataendelea kusumbua tu Ligi Kuu Bara

Muktasari:
Katika mechi hizo 10 imeshuhudiwa jumla ya mabao 19 yakitupiwa nyavuni na wachezaji 17, mmoja akijifunga na wawili kila mmoja akifunga mara mbili, huku wengine 14 wakifunga bao moja moja.
PAZIA la Ligi Kuu Bara msimu wa 2019-2020 limefunguliwa kwa kuchezwa mechi 10 za raundi ya kwanza, huku Lipuli FC na Simba wakichuana kileleni wakifanana kila kitu.
Lipuli walipata ushindi wa kushangaza wa 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Iringa, huku Simba ikiendeleza ubabe wake kwa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Nazo Namungo FC na Polisi Tanzania zikitakata nyumbani, licha ya kuwa ni wageni wa ligi hiyo kwa msimu huu.
Kumbuka timu hizo zimepanda daraja toka la Kwanza (FDL), Namungo ikicheza kwa mara ya kwanza, huku maafande wa Polisi wakiirejea baada ya kushuka enzi ikifahamika kama Polisi Moro.
Yanga ambayo wiki iliyopita iliwatoa kimasomaso mashabiki wake kwa kupata ushindi ugenini katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana, walianza vibaya nyumbani.
Timu hiyo ilikumbana na kipigo cha kushtukiza kutoka kwa Wazee wa Kupapasa, Ruvu Shooting ya Masau Bwire, ikilala 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, ikiwa ni mara mara ya kwanza ndani ya misimu minne kupoteza mchezo wa kwanza tangu mwaka 2014.
Wanachama na mashabiki wa Yanga hawaamini kama Ruvu ambayo katika mechi zaidi ya 10 walizowahi kukutana na chama lao la Jangwani haijawahi kupata ushindi kwao, wamewanyoosha.
Hata hivyo, soka ndivyo lilivyo huwa lina maajabu yake na moja ya mojawapo ni hayo ya Yanga kupapaswa na Ruvu katika mechi ya ufunguzi na kuifanya mabingwa hao wa kihistoria kuanza vibaya.
Katika mechi hizo 10 imeshuhudiwa jumla ya mabao 19 yakitupiwa nyavuni na wachezaji 17, mmoja akijifunga na wawili kila mmoja akifunga mara mbili, huku wengine 14 wakifunga bao moja moja.
Inawezekana ni kweli ni mapema mno kuanza kubashiri, lakini ni vigumu kujizuia kulieleza hili, kuna kila dalili kwamba, Meddie Kagere ataendelea kusumbua tena msimu huu kama ilivyokuwa ligi iliyopita.
Katika msimu uliopita aliwakimbiza sana mabeki wa timu pinzani. Aliwatesa sana makipa kwa kuwatungua. Katika msimu huo wa kwanza kwake kucheza Tanzania, Kagere alimaliza akiwa ndiyeMfungaji Bora. Mabao yake 23 yalitosha kumfanya awe kinara dhidi ya nyota wa timu nyingine akiwamo, Heritier Makambo aliyekuwa Yanga.
Makambo alipompokea kijiti Eliud Ambokile aliyekuwa Mbeya City katika kiti cha kutupia nyavuni msimu uliopita, Mkongoman huyo aliwakimbiza wenzake. Hata hivyo Kagere alitumia mechi za viporo vya timu yake ya Simba kumpiku naqa kumaliza juu yake.
Salim Aiyee mzawa pekee aliyefukuzana na wageni hao alimaliza wa pili kwa mabao 18, moja zaidi ya Makambo aliyekuwa wa tatu.
Ni kweli ligi ndio kwanza imeanza na wachezaji wakitoka kwenye mapumziko, hivyo sio rahisi kuweza kutabiri ligi itakavyokuwa msimu huu, lakini muda utakuja kuthibitisha hili. Kagere atabaki kuwa mmoja ya washambuliaji watakaotetemesha pia msimu huu. Tayari ameshatupia mabao mawili akiwa sawa na Lucas Kikoti wa Namungo, lakini akiendeleza rekodi yake ya kuwa nyota wa kigeni kuwa wa kwanza kufunga katika mechi za Ligi Kuu. Msimu uliopita alifunga bao dhidi ya Prisons kabla ya Makambo kumjibu katika mechi yao ya Mtibwa Sugar. Makambo hayupo. Hata msimu huu anaweza kusumbua tena.
Hii ni kwa sababu kwa sasa hakuna mabeki wa kazi. Mabeki vitasa sampuli ya kina Aggrey Morris, Kelvin Yondani ama Juuko Murshid au Yakub Mohammed kwa sasa ni wachache katika Ligi yetu. Na hapo ndipo naona wazi Kagere ataendelea kusumbua tu hata ndani ya msimu huu. Usibishe! Huyu jamaa anajua soka. Ana kipaji na anajituma sana uwanjani.
Ndio, hivi huwa mnamuangalia anavyopambana uwanjani? Mnamfuatilia jinsi asivyochoka haraka. Huwa mnamuona alivyo mjanja na asiyekata tamaa kirahisi hata kama mipira ipo kwa makipa? Aina ya uchezaji wake unafanana na ule wa Monja Liseki.
Mmoja ya washambuliaji bora waliowahi kutokea nchini. Kagere kwa mwili, stamini na umahiri wake ni kama ule wa Said Mhando. Yule straika wa zamani wa Mtibwa Sugar aliyeanzia kwenye ukipa kabla ya kugeuka mmoja ya washambuliaji waliowaliza makipa.
Anafanana na straika mmoja matata alikuwa akiichezea Abajalo FC. Louis Kibwana ‘Mfede’ a.k.a Baby ama Saad Bilo. Kwa wanaofuatilia soka la Tanzania, ninapomtaja Monja ama Mhando, watakuwa wanaelewa namaanisha nini. Labda kwa huyu Mfede ama Bilo ni kwa wale waliokuwa wakifuatilia Ligi Daraja la Tatu Kinondoni na hata michuano ya Kombe la Kinesi.
Ni kweli Kagere anaonekana umri umemtupa mkono. Achana na umri wa kwenye pasipoti yake, lakini kwa wanaomjua vyema wanakuambia jamaa kala chumvi kiasi chake hata kama tunaambiwa ana umri wa miaka isiyozidi 33. Hili ndilo lililowafanya baadhi ya mashabiki wanamkejeli kwa kumuita Babu a.k.a Mhenga na majina mengine ya kukera. Lakini jamaa wala hajali. Kwani anajua anachokifanya uwanjani. Kwanza ana nguvu na akili ya mpira. Anajua jinsi ya kuwanyamazisha wote wanaombeza. Kwa sababu anajua kufunga. Anafunga leo. Anafunga kesho, halafu anafunga tena hadi anakera! Ukiacha mabao 23 ya Ligi Kuu, mkali huyo pia alifunga mengine 14 katika michuano mingine ikiwamo sita ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga walioendesha kampeni ya kumkejeli yeye na Emmanuel Okwi msimu uliopita, kwa sasa hawamtanii tena! Wanahofia kuadhibiwa tena! Jamaa aliwanyamazisha Taifa kwa bao moja swafiii lilitibua kila kitu Jangwani. Ni mechi hiyo ndio iliyobadilisha upepo wa ubingwa wa msimu huo. Yanga watamtaniaje ilihali aliwanyamazisha? Huyu ndiye Kagere ‘MK14’ a.k.a Terminator. Kwa akili za mabeki hawa laini wa kizazi cha sasa. Wanawezaje kumzuia? Kwanini asiendelee kutesa? Kwanini asitetee kiatu chake cha Dhahabu?! Tena akijua kuwa Vodacom imerejea kudhamini Ligi Kuu? Anajua kabisa kama akimaliza kama kinara wa mabao ana mzigo wake wa maana, sasa kwa nini asifunge na kufunga? Kwa kuangalia usajili uliofanywa na klabu 20 za Ligi Kuu, huwezi kuona mabeki wa kumdhibiti. Pia hata mshambuliaji wa kuchuana naye, humuoni kwa haraka. Obrey Chirwa? Hapana! Salim Aiyee tena? Hapana! Kama alimshindwa msimu uliopita, atamwezea wapi msimu huu akiwa keshaizoea ligi vya kutosha? Kuna mtu anaweza kusema labda Juma Balinya au Ma ybin Kalengo ama Richard Djodi kama sio David Molinga? Hao wote msibeti kwao hata kidogo, kwani sioni wa kuchuana naye.
Hata kama soka lina maajabu, lakini kama we ni mnazi wa mchezo wa kubeti. Nakushauri tu, we beti kwa Kagere kwamba hata simu huu atasumbua. Hakuna mabeki katili wa kumzuia. Kwa msimu uliopita alizitungua timu 12 ikiwamo Azam, Yanga, Mbeya City ambao walipigwa mara mbili kama ilivyokuwa kwa Ruvu Shooting, Mwadui na Coastal Union. Wanapaluhengo waliosumbua msimu uliopita waligongwa. Prisons, Mbao, Singida United, JKT Tanzania na Ndanda wote walinyanyasika mbele ya Kagere.
Ni timu tisa tu, ambazo zilipona mbele ya straika huyo kutoka Rwanda. Kama timu pinzani zitashindwa kumdhibiti, kwanini msimu huu asiendelee kusumbuka wakati akili na kipaji cha soka anacho, huku miguu yake ikiwa bize kufanya yake kuliko mdomo kama baadhi ya wachezaji wengine? Ni kweli kuna wakati huwa anapotea uwanjani akikutana na wababe kama ilivyokuwa kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam. Ila humtokea mara chache.
Tusubiri tuone itakavyokuwa!