Huyu Bwashee anatisha jamani

Muktasari:
Hadi sasa rekodi hiyo Duniani inashikiliwa na raia wa Ecuador, Karl Egloff aliyetumia muda wa saa 6:53 kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro, rekodi aliyoweka mwaka 2014 akiivunja ya Kilians Jornet raia wa Hispania aliyetumia muda wa saa 7:20 kupanda na kushuka mlima huo mwaka 2010.
MTANZANIA Gaudence Lekule (31) ameweka rekodi ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa masaa 8:36 akiwa pia Mwafrika wa kwanza kufanya hivyo na kusema watalii kutoka nje ya nchi ndio siri iliyomhamasisha kupanda mlima huo kwa kasi hivi karibuni.
Hadi sasa rekodi hiyo Duniani inashikiliwa na raia wa Ecuador, Karl Egloff aliyetumia muda wa saa 6:53 kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro, rekodi aliyoweka mwaka 2014 akiivunja ya Kilians Jornet raia wa Hispania aliyetumia muda wa saa 7:20 kupanda na kushuka mlima huo mwaka 2010.
Lekule (31) aliyezaliwa Kijiji cha Kiraracha Wilaya ya Moshi, Kilimanjaro amemuomba Waziri mpya wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kutupia jicho michezo mingine kwani ina nafasi kubwa ya kutangaza na kuliletea sifa taifa.
“Nashukuru kuitangaza Tanzania kidunia na tayari nimepata mialiko mingi ya kwenda nje kushiriki mashindano ya Mountain Run,” alisema.
“Lengo langu ni kuweka rekodi katika milima mirefu duniani, hivyo bado naendelea na mazoezi na nitaendelea kufanya mazoezi hapa kwetu na baadaye nje ya Tanzania.”
Mara ya kwanza Mtanzania kuweka rekodi ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kasi kwa Afrika, ilikuwa kwa Simon Mtui ambaye alitumia muda wa saa 9: 20 mwaka 2006.
Kupanda mlima huo ni jambo linahitaji ujasiri na afya ya kutosha kwa mhusika.