Huyo Sakho balaa tupu

KAMA unamchukulia poa winga wa Simba, Pape Ousmane Sakho basi pole yako, kwani jamaa naye ana balaa, akivunja ukimya na kuanika alivyojipanga kurudi kwenye Ligi Kuu Bara kwa kishindo, huku akiipiga kijembe Yanga inayoongoza msimamo kwa sasa akisema siku zinahesabaika kwa namna walivyopania kupindua meza.
Sakho mwenye mabao mawili katika Ligi Kuu, likiwamo alilofunga jana dhidi ya Biashara Utd, aliliambia Mwanaspoti baada ya kupata changamoto ya majeraha yaliyomtibulia awali, lakini safari hii yupo fiti na moto anaokuja kuuwasha kwenye ligi hautazimika kwani kama timu wana jambo msimu huu.
Alisema changamoto ya majeraha yalisababisha hata kuwekwa kwenye orodha ya wachezaji waliokuwa mbioni kuachwa Simba, lakini baada ya kusalia na kuanza kufanya mambo kwenye mechi dhidi ya Azam sasa gari limewaka, huku akiitisha Yanga kwamba japo hakucheza mechi ya mkondo wa kwanza, lakini atakapokutana nao mwezi ujao wajiandae kwani kiu yake ni kuitungua na kupunguza makali ili timu yao itete ubingwa.
“Nashukuru tangu mechi ya Azam ile ya Ligi Kuu Bara mpaka wakati huu nimekuwa kwenye kiwango ingawa sio katika ubora kama ule ambao naamini ninao na nahitajika kuutoa na kuisaidia timu,” alisema.
“Nilipata nafasi ya kukaa naye kocha (Pablo Franco), aliniambia anaamini katika uwezo wangu na kama nitaongeza mazoezi na kumsikiliza yale maelezo yake naweza kucheza katika kiwango bora zaidi ya sasa.
“Baada ya kuniambia hivyo mbali ya mazoezi ya timu nimekuwa nikifanya yangu binafsi na kumsikiliza zaidi vile ambavyo ananipatia maelekezo nikiwa uwanjani na imani yangu nitakwenda kuonyesha kiwango bora na kuisaidia Simba kufanya vizuri katika mashindano.”
Sakho alisema ingawa bado ni mgeni katika ligi, ila kulingana na kikosi cha Simba kilivyo na kiu ya kufanya vizuri bado wapo katika mbio za ubingwa na wanaweza kuutetea mara ya tano.
Alisema kuna wakati walikutana na changamoto na kushindwa kupata ushindi, ila kwa sasa wamerudi na nguvu katika mashindano ya ndani pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ukiangalia tumeshinda kwa ushindi mkubwa michezo ya Kombe la Shirikisho (ASFC). Tumefanya vizuri michezo ya ligi pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika na tunaamini tunavuka hatua ya makundi na kwenda robo fainali,” alisema Sakho.
“Natamani kucheza kwenye kiwango bora zaidi ya wakati huu ili kuona timu yangu inafanya vizuri sio kufunga mabao tu, bali kuwa msaada kwa wengine kufanya vizuri kulingana na majukumu yetu yalivyo kwani lengo ni moja kuona Simba inaendelea kuwa bora.”
MABEKI HAWA
Sakho alisema miongoni mwa mabeki ambao wamemvutia nchini ni Shomary Kapombe ndio maana katika kikosi cha Simba ni miongoni mwa watu wake wa karibu tangu siku za mwanzo alipotua.
“Kapombe yupo na sifa nyingi kulingana na mahitaji ya beki wa kulia, ndio maana amekuwa akinivutia mpaka amekuwa rafiki yangu wa karibu hata tukiwa nje ya maisha ya timu,” alisema Sakho.
“Kuhusu beki anayeweza kunizuia Yanga nilicheza ile mechi ya ufunguzi wa msimu (Ngao ya Jamii) ila nilikuwa bado na ugeni katika timu na ile ya ligi sikucheza kwa vile nilikuwa majeruhi, lakini kwa ile ijayo nadhani sahihi kulijibu hili baada ya kucheza nao tena. Naheshimu kila beki niliyekutana naye ila nachoangalia ni namna gani nitakuwa imara na bora zaidi ya kila atakayekuwa ananizuia ili kuifanikisha timu yangu kufanya vizuri.”
Sakho alitua Msimbazi msimu huu akitokea Teunguethya kwao Senegal, huku akionekana tegemeo.