Hukumu ya Aveva na mwenzake yakwama tena

Thursday October 21 2021
aveva pic
By Hadija Jumanne

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Oktoba 28, 2021 kutoa hukumu katika kesi ya jinai namba 214/2017 inayomkabili , aliyekuwa Rais wa Klabu Simba, Evans Aveva na aliyekuwa makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka nane yakiweno ya kughushi, kujipatia fedha na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha bila Kamati ya Utendaji ya Simba, kukaa kikao.

Kesi hiyo ilipangwa leo, Oktoba 21, 2021  kutolewa hukumu.

Lakini Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, ambaye anayesikiliza shauri hilo, amesema kuwa  bado hajamaliza kuandika hukumu.

Hakimu Simba, baada ya kusema hayo ameahirisha kes hiyo hadi Oktoba 28, 2021, atakapotoa hukumu.

Hii ni mara ya pili kwa kesi hiyo kushindwa kutolewa hukumu ndani ya mwezi huu.

Advertisement

Kwani Oktoba 6, 2021 Mahakama hiyo ilishindwa kutoa hukumu dhidi ya washtakiwa hao kutokana na Aveva kutokuwepo mahakama, kwa kile kilichoelezwa kuwa ameenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa siku hiyo, baada ya washtakiwa hao kumaliza kujitetea.

Hata hivyo, leo, washtakiwa wote walikuwepo mahakamani hapo, ambapo walionekana katika viunga ya mahakama hiyo tangu saa 2: 30 asubuhi.

Awali, kesi hiyo ilipangwa kusomwa hukumu saa 3:00 asubuhi na muda huo ilipofika, Hakimu Simba aliwaambia washtakiwa hao kuwa  hukumu hiyo itaisomwa saa nane mchana.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka nane, yakiwemo ya  kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila Kamati ya Utendaji ya Simba, kukaa kikao.

Katika mashitaka la kughushi linawakabili washitakiwa wote, anadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Mashtaka mengine, Aveva na Nyange wanadaiwa kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.
Pia, vigogo hao wa zamani wa Simba wanadaiwa  kuhamisha fedha kiasi cha dola za kimarekani 319,212 zilizotokana na mauzo ya aliyekuwa mchezaji wake Emmanuel Okwi,  aliyeuzwa kwa Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia, bila Kamati  Utendaji ya Simba, kukaa kikao.

Advertisement