Huku Lipuli macho kwa Mrundi Haruna

Muktasari:
Wachezaji waliowapoteza ni Kipa, Mohammed Yusuph na beki wa kulia, William Lucian waliotimkia Polisi Tanzania, Paul Ngalema (Namungo), Miraji Athumani (Simba), Zawad Mauya (Kagera Sugar), Haruna Shamte (KMC) na Ally Mtoni aliyejiunga na Yanga.
MATUMAINI ya wakazi wa Iringa na vitongoji vyake msimu huu wa 2019/20 yapo mabegani mwa Mrundi, Haerman Haruna ambaye ni kocha mkuu wa timu hiyo na msaidizi wake, Samweli Moja.
Haermana ana kibarua kizito kwenye kikosi hicho kufuatia kocha aliyemtangulia, Seleman Matola kuifikisha timu hiyo msimu uliopita kwenye fainali ya Kombe la FA, ambayo walipoteza mbele ya Azam mkoani Lindi.
Kocha huyo mbali na kukabiliwa na mtiani huo, anawajibika kuijenga upya Lipuli, ambayo msimu uliopita pamoja na kuondokewa na kocha wao, Matola pia walipoteza karibu nusu ya wachezaji wao muhimu wa kikosi cha kwanza.
Wachezaji waliowapoteza ni Kipa, Mohammed Yusuph na beki wa kulia, William Lucian waliotimkia Polisi Tanzania, Paul Ngalema (Namungo), Miraji Athumani (Simba), Zawad Mauya (Kagera Sugar), Haruna Shamte (KMC) na Ally Mtoni aliyejiunga na Yanga.
MAANDALIZI
Haerman ambaye alikuwa akikijenga kikosi chake kwa michezo kadhaa ya kirafiki, anasema wako tayari kuanza msimu wa Ligi Kuu Tanzania na moja ya malengo yao ni kuhakikisha wanamaliza kwenye nafasi za juu.
“Hakuna kinachoweza kushindikana kikubwa ambacho huwa nakiamini ni jitihada, wachezaji wangu watapaswa kuwa na mitazamo chanya kwenye hili, hatushiriki Ligi kama timu ya wanyonge.
“Nimesikia juu ya rekodi ya msimu uliopita waliyoiweka kwa timu kubwa kwenye uwanja wa nyumbani, natakiwa kuiendeleza kwa kushinda kila mchezo na isiwe kwa Simba na Yanga pekee,” anasema.
KIKOSI
Lipuli imetangaza jumla ya wachezaji 29, ambao itawatumia msimu ujao wa 2019/20 katika orodha hiyo kuna makipa, Agathony Mkwando, Rajabu Mbululo, Seif Ng’indo na Shaban Mwinyikheri Mussa.
Mabeki ni Godfrey Kamata ‘Duchu’, David Mwasa, Mussa Mlyingo, Emmanuel James Sekule, Philipo Mwayombya, Emmanuel Kichiba, Hamad Tajir Wazir, Novalty Lufunga, Derick Karulika na Steven Mganga.
Viungo ni Fredy Tangalu, Josephat Tonye Ntamak, Jimmyshoji Mwasondole, Ally Lyungu, Patrick Victory, Mwinyi Elias, Paul Materas.
Washambuliaji ni Issa Rashid, Daruwesh Saliboko, Paul John Nonga, Joshua Ibrahim, Kennethy Masumbuko, Rashid Seif Karihe, Shehuu Magaji na Albert Kisake.
MATOLA AFUNGUKA
Kocha wa zamani wa Lipuli, Seleman Matola ambaye, amejiunga na Polisi Tanzania iliyopanda daraja, anasema viongozi wanatakiwa kushikamana na kocha huyo mpya ili waweze kufanya vizuri msimu huu kama ilivyokuwa msimu uliopita.
“Wanaweza kuwa bora au zaidi ya msimu uliopita kikubwa ni viongozi kumuunga mkono,” anasema kocha huyo.
Matola anasema anajivunia kupata mafanikio msimu uliopita akiwa na Lipuli huku akieleza vile Mohammed Yusuph, William Lucia, Paul Ngalema, Miraji Athumani , Zawad Mauya, Haruna Shamte na Ally Mtoni walivyokuwa muhimu.
“Tulimaliza nafasi ya sita haikuwa mbaya kwetu na ukiangalia tulikuwa na nafasi ya kufanya vizuri zaidi kutokana na upishano wa pointi uliokuwapo na wapinzani wetu, “ anasema.
Pia Matola anasema kucheza fainali ya FA tena kwa kuwaondoa Yanga, ambayo ugumu wake unafahamika tena katika mchezo muhimu kama ule haikuwa kazi nyepesi.
“Wachezaji wote hao walipambana kwa kujitolea huku wakishirikiana na wenzao na mwisho wa siku tukawatoa Yanga.”