Huko Simba wanaofuata ni hawa

WAKATI mashabiki wakiwa bado wana hasira ya kushuhudia timu yao ikifungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya maafande, mabosi wa klabu hiyo wameanza kusafisha benchi la ufundi ambapo baada ya meneja na kocha wa makipa, inaelezwa wanaofuata ni makocha wenyewe.

Simba ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons mjini Sumbawanga, kabla ya kupigwa tena na Ruvu Shooting wikiendi iliyopita na kuleta taharuki kwa mashabiki wao waliozoea kuona chama lao likifunika.

Hata hivyo, kumbe mabosi wao waliitana kujadili vipigo hivyo na kutoa mapendekezo ya kuwafyeka Meneja Patrick Rweyemamu na Kocha wa Makipa, Mohammed Mharami ‘Shilton’ pamoja na watumishi wengine wawili na kinachofuata sasa ni zamu ya makocha.

Meneja huyo alisema mabosi wake wamemueleza hawataendelea naye baada ya kuona hatoshi, huku timu ikijiandaa kwa mashindano magumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika yatakayoanza mwezi ujao.

“Ni kweli nimeambiwa sifai kuwa meneja ni taarifa kamili kwa kuwa imetoka kwa viongozi wangu, japo hawajanipa barua, hivyo tusubiri,” alisema Rweyemamu, huku Shilton akisema hakuwa na taarifa rasmi, ila hatakuwa na neno kwani wao ndio waliomteua.

Wengine waliofyekwa ni watu wa Idara ya Habari, Ally Shatry ‘Bob Chico’ na Jacob Gamaly, na wanaofuata ni makocha akiwamo Sven na wasaidizi wake, Seleman Matola na wa viungo, Adel Zrane.

Habari za ndani kutoka Simba zinasema baada ya vikao vizito kamati ya uongozi iliwahoji Sven na Matola na kuamua uamuzi utafanywa na Bodi ya Wakurugenzi.

Taarifa zaidi zinasema siku za Sven zinahesabika kwa kilichoelezwa kushindwa kuisimamia timu na maelewano duni na wachezaji na maofisa wenzake.

Kocha huyo ametajwa kuwa na migogoro na wachezaji ikielezwa hata katika mechi dhidi ya Ruvu ndiye aliamua nahodha John Bocco na msaidizi wake Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wasivae beji ya unahodha na badala akampa Jonas Mkude. Licha ya Mwanaspoti kujitahidi kuwasiliana na viongozi wa Simba akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘TryAgain’; Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na Kaimu Mwenyekiti wao, Mwina Kaduguda jitihada ziligonga mwamba kwani vigogo hao hawakupokea simu wala kujibu meseji na wengine hawakupatikana kabisa.