Huko kwa Msuva ni uzungu mtupu

Muktasari:

  • Ufiti wa Msuva umedaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na programu hiyo ya kurejesha ufiti wa mwili, ambayo ni kukaa sehemu maalumu iliyojazwa vipande vya barafu vinavyomfunika kuanzia kiunoni hadi chini.

USIONE Mtanzania Saimon Msuva anayetesa na Difaa El Jadida anafunga mabao kila kukicha ukawa unachukulia poa, unaambiwa kuna programu maalumu ambayo huwa wanafanya kwa dakika 10 kila siku ndiyo maana amekuwa fiti kucheka na nyavu kila wakati.

Ufiti wa Msuva umedaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na programu hiyo ya kurejesha ufiti wa mwili, ambayo ni kukaa sehemu maalumu iliyojazwa vipande vya barafu vinavyomfunika kuanzia kiunoni hadi chini.

Akizungumza kuhusu programu hiyo ambayo huwa wanaifanya kila siku baada ya kumaliza mazoezi ya kawaida na hata baada ya mechi, Msuva amesema inasaidia kupunguza uchovu na kuondokana na majeraha ya mara kwa mara.

“Ni mazoezi ya kurejesha utimamu wa mwili, kama mchezaji unapata majeraha madogo yanasaidia kuondoa, ni kama vile unavyoona matabibu wengi huingia na barafu uwanjani ili kutibia,” alisema.

“Sasa tunachokifanya huku ni kwa jumla, kurejesha ufiti wa maeneo yote ambayo yaligongwa kwa bahati mbaya wakati wa mazoezi ya kawaida na mechi, inasaidia sana kukufanya kuwa bora uwanjani,” alisema Msuva.