Hizi mashine zikitua Yanga wamekwisha

Tuesday June 08 2021
mashine pic
By Mwandishi Wetu

YANGA wanakiri kwamba eneo kubwa lililowaangusha msimu huu kuhusu ubora wa timu yao basi ni eneo la ushambuliaji na sasa kuna mastraika watano kati ya hao wanataka wawili kuingia ndani, ili kuvaa jezi za Michael Sarpong na Fiston Abdulrazack walio mbioni kupewa mkono wa kwaheri.

Uwezekano wa Yanga kuendelea na mastraika wao wawili ni mdogo sana kutokana na kushindwa kuwapa wanachotaka sasa ni kusaka watu wawili wa maana watakaowarudishia mabao msimu ujao.

Usajili wa eneo hilo tayari Mwanaspoti linafahamu kwamba mabosi wa juu wa klabu yao wana majina matano ya washambuliaji hatari ambao kati ya hao wawili lazima wavae uzi wa klabu yao.


FISTON MAYELE

Jina la kwanza kubwa katika orodha ya washambuliaji hao ni Fiston Mayele ambaye msimu unaomalizika aliisaidia AS Vita kuwa bingwa akifunga mabao 12 kwenye ligi akizidiwa mabao mawili tu na mfungaji bora Jean Baleke wa TP Mazembe.

Advertisement

Mayele jina lake limependekezwa na viungo wa Yanga, Mukoko Tonombe na winga Tuisila Kisinda ana ubora wa kujua kufunga ingawa Yanga itatakiwa kupambana kunasa saini yake kutokana na Vita kuwa ndio roho yao chini ya kocha Florent Ibenge.


DARK KABANGU

Mshambuliaji mwingine aliye katika rada za Yanga ni Dark Kadima Kabangu anayeshika nafasi ya nne katika ufungaji katika Ligi Kuu DR Congo akiwa na mabao 9 akiwa na DC Motema Pembe na ubora mkubwa wa Kabangu ni kufunga mabao ya vichwa na msimu huu ameshafunga mabao ya namna hiyo matano.


MAGBI GBAGBO

Yanga inafikiria kurudi tena kwa Magbi Gbagbo raia wa Ivory Coast baada ya mawindo yao ya awali kukwama katika dirisha dogo la usajili kufuatia Rais wa Wydad Casablanca kugomea dau la Yanga.

Gbagbo sasa baada ya kugoma kuendelea kuitumikia Wydad iliyogoma kumuuza Yanga na badala yake kutolewa kwa mkopo klabu ya Al Tai ya Saudi Arabia na huko ameshafunga mabao 10 katika mechi nane.


MAKUSU MUNDELE

Staa mwingine ni Mkongo Jean-Marc Makusu Mundele ambaye sasa anatakiwa kurudi katika klabu yake ya AS Vita baada ya Orlando Pirates kukatisha mkataba wake wa mkopo na hatua kubwa ni straika huyo kukosa mazoezi kwa muda akizidiwa na wenzake aliowakuta baada ya kuvunjika mguu mwaka mmoja uliopita.

Hapa tena Kisinda na Mukoko wamepeleka jina la mshambuliaji huyu kwa mabosi wao wakati Kisinda akieleza kwamba anataka kuungana tena na Makusu katika msimu ambao waliifanyia kitu kibaya Simba wakicheza kwa ushirikiano na kuifunga mabao 5-0 pale jijini Kinshasa kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


LAZAROUS
KAMBOLE

Straika Mzambia Lazarous Kambole ambaye naye huenda akaachwa na klabu yake ya Kaizer Chiefs naye yumo katika hesabu za Yanga hasa baada ya kusikia klabu yake inataka kumtoa.

Hesabu za Kambole Mwanaspoti linafahamu kwamba bosi wa Kaizer Bobby Kaizer ambaye ni mtoto wa mmliki wa klabu hiyo tayari wameshaanza kuongea na bosi wa Yanga Injinia Hersi Said katika kuulizia huduma ya mshambuliaji huyo.


MSIKIE BOSI WA UFUNDI

Katika harakati hizo za usajili Mwanaspoti lilimtafuta Mkurugenzi wa Kamati ya Ufundi ya Yanga Dominic Albinus alisema bado wanafanya mambo yao kimyakimya katika kusaka mastaa wao wapya na kwamba mchakato huo utatanguliwa na hatua ya kukabidhiwa kwa ripoti na kocha wao Nesreddine Nabi ya kipi anataka kukiboresha katika timu yao.

“Niwatoe wasiwasi Yanga ikimsajili mtu mtamuona na tutamtambulisha.”

Advertisement