Hizi hapa timu 24 zilizofuzu Afcon na mafanikio yao

Muktasari:
- Stars imefuzu michuano hiyo ikiwa ni mara ya nne baada ya kufanya hivyo mwaka 1980, 2019 na 2023.
MECHI za kufuzu Afcon 2025 zimehitimishwa jana Novemba 19, 2024, miongoni mwa timu 24 zilizofuzu ni Taifa Stars.
Stars imefuzu michuano hiyo ikiwa ni mara ya nne baada ya kufanya hivyo mwaka 1980, 2019 na 2023.
Afcon 2025 ambayo itakuwa ni ya 35 tangu ilipoanza 1957, inatarajiwa kuchezwa nchini Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 vikitumika viwanja sita vilivyopo kwenye majiji sita.
Hapa kuna orodha ya timu 24 zilizofuzu michuano hiyo na ushiriki wao sambamba na mafanikio yao katika Afcon.
Morocco
Ndio nchi mwenyeji, mwaka 2025 itakuwa ni mara ya 20 kushiriki Afcon baada ya 1972, 1976, 1978, 1980, 1986, 1988, 1992, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008, 2012, 2013, 2017, 2019, 2021 na 2023. Wamebeba ubingwa mara moja mwaka 1976.
Burkina Faso
Walishika nafasi ya pili katika Kundi L. Wanakwenda kushiriki kwa mara ya 14 baada ya mwaka 1978, 1996, 1998, 2000, 2002, 2004, 2010, 2012, 2013, 2015, 2017, 2021 na 2023, huku ikiwa haijawahi kubeba ubingwa zaidi ya kushika nafasi ya pili mara moja mwaka 2013.
Cameroon
Wamemaliza vinara wa Kundi J, tayari wameshiriki mara 21, hii inakuwa ya 22 baada ya kufanya hivyo mwaka 1970, 1972, 1982, 1984, 1986, 1988, 1990, 1992, 1996, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008, 2010, 2015, 2017, 2019, 2021 na 2023. Cameroon wamebeba ubingwa mara tano, 1984, 1988, 2000, 2002 na 2017.
Algeria
Wakiwa ni vinara wa Kundi E, wanakwenda kushiriki kwa mara 21. Miaka waliyoshiriki ni 1968, 1980, 1982, 1984, 1986, 1988, 1990, 1992, 1996, 1998, 2000, 2002, 2004, 2010, 2013, 2015, 2017, 2019, 2021 na 2023. Wamechukua ubingwa mara mbili 1990 na 2019.
DR Congo
Wamemaliza vinara Kundi H, wanakwenda kushiriki kwa mara ya 21 baada ya 1965, 1968, 1970, 1972, 1974, 1976, 1988, 1992, 1994, 1996, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2013, 2015, 2017, 2019 na 2023. Ubingwa wamechukua mara mbili 1968, 1974.
Senegal
Wamekuwa vinara Kundi L, tayari wameshiriki mara 17, mwaka 1965, 1968, 1986, 1990, 1992, 1994, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008, 2012, 2015, 2017, 2019, 2021 na 2023, hii itakuwa ya 18 na tayari nchi hiyo imebeba ubingwa mara moja 2021.
Misri
Vinara Kundi C, tayari wameshiriki mara 26 (1957, 1959, 1962, 1963, 1970, 1974, 1976, 1980, 1984, 1986, 1988, 1990, 1992, 1994, 1996, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008, 2010, 2017, 2019, 2021, 2023). Ubingwa wamebeba mara saba (1957, 1959, 1986, 1998, 2006, 2008 na 2010)
Angola
Wamekuwa vinara Kundi F, wameshiriki mara 9 (1996, 1998, 2006, 2008, 2010, 2012, 2013, 2019, 2023). Mafanikio yao makubwa ni kuishia robo fainali 2008, 2010 na 2023.
Equatorial Guinea
Kutoka Kundi E wameshika nafasi ya pili, wameshiriki mara 4 (2012, 2015, 2021, 2023). Mwaka 2015 walishika nafasi ya nne na ndiyo mafanikio yao makubwa.
Ivory Coast
Nafasi ya pili Kundi G ndiyo wameishika, hii ni mara 26 wanakwenda kushiriki baada ya 1965, 1968, 1970, 1974, 1980, 1984, 1986, 1988, 1990, 1992, 1994, 1996, 1998, 2000, 2002, 2006, 2008, 2010, 2012, 2013, 2015, 2017, 2019, 2021 na 2023. Ndio mabingwa watetezi wakiwa pia wamebeba ubingwa mara tatu 1992, 2015 na 2023.
Gabon
Wameshika nafasi ya pili Kundi B, huku wakienda kushiriki Afcon ya 9 kwao baada ya mwaka 1994, 1996, 2000, 2010, 2012, 2015, 2017 na 2021. Mafanikio yao makubwa ni kucheza robo fainali 1996 na 2012.
Uganda
Imeshika nafasi ya pili Kundi K, hii itakuwa ni Afcon ya 8 kwao baada ya 1962, 1968, 1974, 1976, 1978, 2017 na 2019. Mafanikio makubwa ni kushika nafasi ya pili 1978.
Afrika Kusini
Ndiyo vinara Kundi K, wanakwenda kushiriki mara ya 12 baada ya 1996, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008, 2013, 2015, 2019 na 2023. Mafanikio yao ni kubeba ubingwa mara moja 1996.
Tunisia
Nafasi ya pili Kundi A ni yao, inakwenda kushiriki kwa mara ya 21 baada ya 1962, 1963, 1965, 1978, 1982, 1994, 1996, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008, 2010, 2012, 2013, 2015, 2017, 2019, 2021 na 2023 huku ikiwa imebeba ubingwa mara moja 2004.
Nigeria
Ndiyo vinara Kundi D, wanashiriki kwa mara ya 21 baada ya 1963, 1976, 1978, 1980, 1982, 1984, 1988, 1990, 1992, 1994, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008, 2010, 2013, 2019, 2021 na 2023. Ubingwa wamebeba 1980, 1994 na 2013.
Mali
Vinara Kundi I, wanashiriki kwa mara ya 14 baada ya 1972, 1994, 2002, 2004, 2008, 2010, 2012, 2013, 2015, 2017, 2019, 2021 na 2023. Haijawahi kuwa bingwa zaidi ya kushikja nafasi ya pili mwaka 1972.
Zambia
Wamemaliza vinara Kundi G, wanakwenda kushiriki kwa mara ya 18 baada ya 1974, 1978, 1982, 1986, 1990, 1992, 1994, 1996, 1998, 2000, 2002, 2006, 2008, 2010, 2012, 2013, 2015 na 2023. Wana taji moja walilobeba mwaka 2012.
Zimbabwe
Kutoka Kundi J wameshika nafasi ya pili na wanakwenda kushiriki kwa mara ya 6 baada ya 2004, 2006, 2017, 2019 na 2021. Kila mara iliposhiriki imeishia hatua ya makundi.
Comoros
Hii itakuwa ni Afcon yao ya pili baada ya kushiriki mwaka 2021 na kuishia hatua ya 16 bora. Katika kufukuzia ushiriki wao wamemaliza vinara Kundi A.
Sudan
Nafasi ya pili Kundi F ndiyo wameshika, wanakwenda kushiriki kwa mara ya 10 baada ya 1957, 1959, 1963, 1970, 1972, 1976, 2008, 2012 na 2021 huku kabatini wakiwa na kombe moja walilobeba mwaka 1970.
Benin
Wamemaliza nafasi ya pili Kundi D, wanakwenda kushiriki kwa mara ya 5 baada ya 2004, 2008, 2010 na 2019. Mafanikio yao makubwa ni kucheza robo fainali mwaka 2019.
Tanzania
Wameshika nafasi ya pili Kundi H, wanakwenda Afcon ya 4 baada ya 1980, 2019 na 2023 ambapo zote hizo wameishia makundi.
Botswana
Wameshika nafasi ya pili Kundi C, hii inakuwa ni Afcon yao ya 2 baada ya mwaka 2012 ambapo waliishia 2012.
Msumbiji
Imeshika nafasi ya pili Kundi I, inakwenda kushiriki kwa mara ya 6 baada ya 1986, 1996, 1998, 2010 na 2023. Mara zote wameishia makundi.