Hiyo Burundi imempa mzuka mpya Ndayiragije

Muktasari:

  • Timu nne zitakazoiwakilisha Afrika Mashariki katika fainali hizo za 32 tangu kuasisiwa kwa Afcon mwaka 1957 ni Burundi, Kenya, Tanzania na Uganda ambazo zimepangwa kwenye makundi matatu tofauti.


KOCHA mpya wa Azam FC, Etienne Ndayiragije amezitabiria neema timu za Afrika Mashariki kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Misri kuanzia wiki ijayo.

Raia huyo wa Burundi alisema kiwango cha soka kwa ukanda wa Afrika Mashariki kwa sasa kimeimarika na haitakuwa jambo la kushangaza iwapo timu zake nne zitafika mbali.

“Hakuna kitu cha ajabu. Umeona jana (juzi) Burundi imetoka sare ya bao 1-1 mchezo wa kirafiki dhidi ya Algeria iliyojaza mastaa kibao wa Ulaya akiwemo Riyad Mahrez.

“Kama imeweza kupata sare dhidi ya Algeria nadhani hilo linawezekana kwa timu nyingine,” alisema Ndayiragije ambaye jana alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuinoa Azam FC.

Timu nne zitakazoiwakilisha Afrika Mashariki katika fainali hizo za 32 tangu kuasisiwa kwa Afcon mwaka 1957 ni Burundi, Kenya, Tanzania na Uganda ambazo zimepangwa kwenye makundi matatu tofauti.

Uganda ipo kundi A sambamba na Misri, Zimbabwe na DR Congo ilhali Tanzania na Kenya zipo kundi C pamoja na timu za Algeria na Senegal wakati Burundi ipo kundi B na timu za Madagascar, Nigeria na Guinea. Kipute kinaanza Juni 21.