Hitimana: Nyie subirini muone mambo!

Tuesday September 14 2021
hitimana pic
By Daudi Elibahati

KOCHA Thiery Hitimana yupo kambini Arusha akianza kibarua chake ndani ya klabu hiyo, huku akisisitiza kutua kwake Msimbazi sio kwa bahati mbaya na kwamba mashabiki wakakae kwa kutulia kwani kwa mipango na ukubwa wa klabu hiyo mambo mazuri yakuwepo msimu huu.
Simba iliamua kuimarisha benchi lake la ufundi kwa kummuajiri kocha huyo wa zamani wa Biashara United, Namungo na Mtibwa Sugar iliyokuwa imemrejesha nchini ili ainoe kuziba nafasi ya Mohammed Badru aliyempokea wakati alipotimika Manungu msimu uliopita.
Hitimana ni miongoni mwa makocha wanaoheshimika Rwanda na aliwahi kufanya kazi na Kocha Mkuu wa sasa wa Simba, Didier Gomes wakati Rayon Sports ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Rwanda mwaka 2012 na akizungumza na Mwanaspoti alisema uamuzi wake wa kutua Msimbazi uliokuwa sahihi licha ya kuwa tayari alishazungumza na Mtibwa na kushindwa kuafikiana baadhi ya mambo.
“Ni kweli ilibidi nijiunge na Mtibwa na kama ulivyoona tulishaanza maandalizi ya msimu, lakini sikuwa nimesaini nao mkataba, hivyo Simba waliponiletea ofa yao nikaona ni nzuri na bora nifanye nao kazi na kwamba Simba ni timu kubwa na naamini nitashirikiana kutimiza malengo ya msimu,” alisema.
Hitimana aliyeipandisha daraja Namungo kutoka Daraja la Kwanza misimu miwili iliyopita, alisema ametua Simba akijua ina malengo yake kwa msimu ujao naye anaijua vyema kazi yake atashirikiana na wenzake kuhakikisha wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wanaendelea kupata raha zaidi.
“Simba ni Klabu yenye malengo makubwa hivyo kitu cha kwanza nitakachofanya ni kuleta umoja ambao utatusaidia kufikia kule tunapopahitaji, lakini ni timu yenye wachezaji wa viwango vya juu ambao wana uwezo wa kupambana na kuipa mafanikio makubwa kitaifa na kimataifa,” alisema Hitimana.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alifafanua juu ya ujio wa Hitimana akisema ilitokana na ombi la Gomes aliyeutaka uongozi kuongezewa msaidizi mwingine kwenye benchi la ufundi na sifa za Hitimana zinakidhi kila kitu.
“Ni jambo la kawaida kwa timu kubwa kuwa na makocha wasaidizi zaidi ya mmoja kutokana na mahitaji ya timu hivyo tumeamua kuongeza nguvu katika timu kwa kuwa na mtu wa aina ya Hitimana,” alisema Barbara, huku Gomes mwenyewe akisema amefurahishwa na ujio wa kocha huyo aliyekiri ni wa daraja la juu.
“Wakati nikija Afrika kwa mara ya kwanza nilianzia Rwanda na Rayon Sports ndio ilikuwa timu ya kwanza, Nakumbuka nilikuwa mkali sana enzi zile na Hitimana alikuwa anasaidia kupooza joto kidogo. Ni mtu mzuri na ni kocha wa viwango,” alisema Gomes.
Hitimana ni msomi wa Shahada ya Uzamili katika masuala ya fedha aliyopata Ubelgiji, pia ana leseni ya ukocha daraja A inayotolewa na CAF na ametua Msimbazi wakati Gomes akiwa miongoni mwa makocha waliozuiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kufanya kazi katika mashindano yote yanayoandaliwa na shirikisho hilo kwa kukosa sifa ya kuwa na leseni za CAF A au UEFA Pro.
Hata hivyo uongozi wa Simba umeshafafanua kuwa, tayari Gomes aliyeipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC pamoja na kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alishaanza kusoma kozi hiyo na atakamilisha masomo yake Januari mwakani na kupewa leseni ya UEFA Pro.


KAMBI YANOGA
Ujio wa Hitimana umeelezwa umeongeza mzuka katika kambi ya Simba iliyopo jijini Arusha, huku baadhi ya mastaa wakiamini kuungana kwake na Gomes, kutaifanya chama lao litishe zaidi kuliko ilivyokuwa msimu uliopita walipotetemesha vigogo Afrika kwa kuongoza Kundi A mbele ya Al Ahly ambao hata hivyo walikuja kuibuka kuwa mabingwa tena wakitetea taji kwa mara mbili mfululizo.
Kocha Hitimana alitambulishwa jioni kambini na fasta alianza kulimsha pamoja na makocha wenzake kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na ile ya kimataifa, lakini kubwa ni tamasha lao la Kilele cha Wiki ya Simba Day kitakacofanyika Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar.
Simba imepiga kambi hiyo ya maandalizi baada ya ile ya kwanza ya Rabat, Morocco kuwa na mafanikio ikiwamo kucheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa zilizoishia kwa sare na ikiwa Arusha imeshacheza mechi na Coastal Union na kutoka suluhu na mipango yao sasa ni kucheza nyingine mbili kabla ya kurudi Dar es Salaam kuvaana na TP Mazembe katika Simba Day kisha kuisubiri Yanga katika Ngao ya Jamii.Advertisement