Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hisia Zangu: Ndayiragije anavyomtumia Samatta kutapeli mabeki

Muktasari:

Nikamwambia Samatta aende kushoto halafu Farid arudi nyuma ya Nchimbi na Msuva acheze kulekule kulia lakini awe anaingia kwa ndani kwa sababu kitendo cha Samatta kwenda kushoto kilisababisha mabeki wa Guinea kwenda zaidi upande wake

NIPO Tunisia na kikosi cha Taifa Stars. Juzi Jumapili nikaanza kupiga soga na kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Etienne Ndayiragije. Anaujua mpira. Nikamuuliza kuhusu Mbwana Samatta. Anamtumiaje Samatta?
Wiki chache zilizopita, jina la Samatta lilikuwa katika vyombo mbalimbali za habari Ulaya. Bao lake la kichwa dhidi ya Liverpool akiwa na Genk pale Anfield lilikuwa kivutio kikubwa kwa wachambuzi wa pambano hilo la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Michael Owen alisikia akisifia kichwa cha Samatta. Ikawa hivyo hivyo kwa Peter Crouch. Ikawa hivyo hivyo kwa Gary Lineker ambaye aliibuka kuwa mfungaji bora wa muda wote katika michuano ya Kombe la Dunia pale Mexico.
Ijumaa katika pambano dhidi ya Ikweta Guine, Samatta alirudi kuonekana kuwa mchezaji wa kawaida kiasi uwanjani. Hapo ndipo nilipomuuliza kocha wa Taifa Stars ilikuaje Samatta akaonekana wa kawaida uwanjani tofauti na mechi ngumu dhidi ya Liverpool. Jibu lake liliniacha hoi.
“Nilijua namna ya kumtumia Samatta. Nilimwambia yeye ana jina kubwa kwahiyo Guinea ya Ikweta watakuwa wamejipanga kumlinda zaidi yeye. Nilimwambia akae katikati na asiondoke kwenda pembeni na wala asiwe na makeke sana,” anasema Ndayiragije.
“Lengo langu ni kuhakikisha kwamba mabeki wawili wa kati wanasimama na Samatta muda wote na hawaendi kusaidia mabeki wa pembeni. Unajua katika mabeki wa kati mmoja huwa anakwenda kumsaidia beki wa kushoto na mwingine anakwenda kumsaidia beki wa kulia.”
“Nilijua kwamba kama Samatta atasimama katikati, basi Msuva upande wa kushoto atabakia na beki mmoja bila ya msaada mkubwa na upande wa kushoto Farid atabakia na beki mmoja bila ya msaada mkubwa,” anasema Ndayiragije.
“Kipindi cha pili niliamua kuongeza mashambulizi na nikaamua kumuingiza Detram Nchimbi nafasi ya Hassan Kessy. Nikamwambia Samatta aende kushoto halafu Farid arudi nyuma ya Nchimbi na Msuva acheze kulekule kulia lakini awe anaingia kwa ndani kwa sababu kitendo cha Samatta kwenda kushoto kilisababisha mabeki wa Guinea kwenda zaidi upande wake.”
“Ndio maana Nchimbi alijikuta peke yake katikati wakati anampa ile pasi Sure Boy. Lakini hata bao la kwanza Msuva alikuja kufungia katikati kwa sababu mabeki wa kati akili yao ilikuwa kwa Samatta aliyekuwa kushoto lakini pia na Nchimbi ambaye alikuwa ameingia,” anaongeza Ndayiragije.
Huu ndio utapeli ambao Ndayiragije anautumia kwa Samatta. Katika hoteli ambayo tumefikia hapa Tunisia, Movenpick Hotel, mwandishi mmoja wa Libya aliyejitambulisha kwa jina la Foudhy alifika kwa ajili ya kufanya mahojiano na Ndayiragije.
Baadaye nilipata nafasi ya kuzungumza na mwandishi huyo na akili yake yote ilikuwa kwa Samatta. Juzi katika uwanja wa mazoezi wa Stars, Khantoui, waandishi wa habari wa Libya walifika kwa wingi katika mazoezi ya Stars kwa ajili ya kuzungumza na Samatta.
Nilichomuuliza Ndayiragije ni kama hali hiyo ni nzuri kwa Stars kwa sababu ni wazi kwamba timu pinzani zitakuwa zinaandaa mkakati maalumu kwa ajili ya kuikaba zaidi Stars, hasa Samatta, badala ya kujaribu kuishambulia Stars na hivyo kuwapa nafasi wachezaji wa Stars kupata nafasi nyingi nyuma ya wapinzani wao. Ndayiragije alikuwa na mawazo mengine ya kitapeli zaidi kuhusu hilo.
“Mimi ndicho ninachotaka na kupenda. Akili zao ziwe kwa Samatta. Lazima umtumie mchezaji mwenye jina kubwa zaidi kwa ajili ya kuhakikisha wengine wanacheza kwa uhuru. Lakini pia unainyima timu pinzani raha ya kucheza kwa uhuru kwa kumhofia mchezaji mmoja au wawili wenye jina kubwa na badala yake utawala wao wa mpira unakuwa duni kiasi kwa sababu ya hofu na tahadhari.”
Ndayiragije anadai alitumia mbinu kama hizo katika pambano kati ya Stars na Burundi pale Bujumbura. Safari hii katika mpango huu alimuweka pia Msuva ambaye naye ana jina kubwa Burundi.
“Niliwaambia Samatta na Msuva wasirudi nyuma kusaidia kulinda na badala yake mmoja kae upande wa kulia na mwingine akae upande wa kushoto. Ilisababisha mabeki wao wa kati wavutike mmoja akaenda upande wa kulia na mwingine akaenda upande wa kushoto. Viungo wakawa wanarudi zaidi eneo la katikati la ulinzi. Mabeki wa pembeni pia hawakuwa na raha sana ya kwenda mbele,” anasema Ndayiragije.
“Matokeo yake pale katikati kina Sure Boy wakawa na uwanja mpana wa kucheza. Ukiwa na wachezaji wenye majina jivunie kuwa nao. Sio kwamba wataonyesha uwezo mkubwa uwanjani kila siku, hapana, lakini watasababisha wenzao wacheze vizuri kwa kutumia tu vivuli vyao.”
Huu ndio utapeli ambao Ndayiragije anajivua kuufanya kwa Mbwana Samatta. Ni namna tu ya kumtumia Samatta na jina lake kwa ajili ya kuifanya timu icheze.
 Mchezaji sio mmoja tu katika kikosi cha Stars kama wengine wanavyofikiria,  bali wapo wengi wengi, lakini watapata raha kubwa uwanjani kama mabeki wa timu pinzani watakuwa wanamhofia Samatta.