HISIA ZANGU: Mayele vs Yanga, shida iko wapi?

Muktasari:

  • Kwa muda mrefu sasa Mayele amekuwa akitoa shutuma kadhaa kwa watu wa Yanga. Amekuwa akiongea hili na lile. Wakati mwingine kumekuwa na utoto ndani yake ambao unawashangaza mashabiki. Utoto mwingi unatoka katika upande wa Mayele.

Swali la msingi zaidi ambalo linaweza kuulizwa ni hilo hapo. Swali ambalo nadhani hata Azam TV lilikaribia kuwaingiza matatizoni na Yanga wiki iliyopita. Shida iko wapi kati ya Fiston Mayele na klabu ya Yanga?

Kwa muda mrefu sasa Mayele amekuwa akitoa shutuma kadhaa kwa watu wa Yanga. Amekuwa akiongea hili na lile. Wakati mwingine kumekuwa na utoto ndani yake ambao unawashangaza mashabiki. Utoto mwingi unatoka katika upande wa Mayele.

Amekuwa akiishambulia zaidi kwa ujumla wake. Inawezekana baadaye alikuwa na shida na kiongozi mmoja wa Yanga hilo haliwezi kumfanya agombane na taasisi nzima. Inawezekana amekuwa na shida na shabiki mmoja au wawili ambao amegombana nao mitandaoni, hilo halimfanyi awe na ugomvi na mashabiki wote wa Yanga ambao hadi anaondoka walikuwa wanamhusudu.

Mashabiki wa Yanga walikuwa wameumia kuona Mayele ameondoka. Ni kawaida tu katika soka. Lakini baada ya Mayele kuwa na maneno dhidi ya Yanga kwa sasa wamekuwa wakimchukia mazima. Ameitengeneza zaidi chuki hii yeye mwenyewe kwa kuacha kujikita na soka lake la kulipwa Pyramids na badala yake kujikita zaidi na simu yake katika mtandao wa Instagram.

Katika mrundikano wa shutuma Mayele anaamini kwamba watu wa Yanga walimroga mguu wake ukavimba akashindwa hata kucheza. Sidhani kama ni kweli, lakini kama ni kweli je huu ni msimamo wa klabu dhidi yake? Kwamba walikutana wakaweka kikao cha kuharibu mguu wa Mayele. Baada ya hapo unajiuliza, kwa lipi hasa wamroge Mayele?

Katika jambo rahisi kueleweka ni kuondoka kwa Mayele. Afrika ina washambuliaji wachache hatari kama yeye na kwa mambo aliyofanya msimu uliopita ilikuwa wazi kwamba Yanga walikuwa katika hatari ya kumpoteza Mayele. Lazima wakubwa wangekuja kumchukua mtu wao. Inasemwa kwamba samaki mkubwa huwa anamla samaki mdogo.

Lazima angekuja mkubwa mmoja na dau kubwa la kumnunua Mayele lakini pia na dau kubwa la mshahara ambalo lingewaletea Yanga kasheshe ya kumlipa. Na ndicho kilichotokea. Inawezekana kukawa na shingo upande kutoka kwa kiongozi au viongozi wa Yanga lakini huu ndio ukweli ilibidi waumeze. Baada ya hili sijaona sababu ya kumroga mtu avimbe mguu. Sijaona sababu ya kumtupia majini. Ili iweje? Historia inaonyesha chuki kubwa inayokuwepo kwa mchezaji anayehama hizi timu za Kariakoo ni pale anapokwenda kwa mtani. Na sasa mchezaji anapokwenda Azam pia kama alivyofanya Fei Toto. Feisal aliondoka kwa chuki kubwa na mpaka leo bado anang’ara. Yanga hawajamrushia majini. Kwanini wafanye kwa Mayele ambaye aliuzwa vizuri bila ya timbwili la chuki? Mayele alipendwa zaidi ya Edibily Jonas Lunyamila ambaye mwaka 1994 aliamua kwenda kuvuta pesa za tajiri wa klabu ya Malindi ya Zanzibar, Naushad Mohamed?

Nadhani kuna tabia ambayo Mayele aliificha akiwa Yanga na sasa ameifichua. Kutaka kuonekana mkubwa na mfalme. Bahati mbaya inamuumiza pia kwamba Yanga wanasonga mbele bila ya yeye. Huwa inatokea unapoachana na mpenzi wako. Hautaki yamtokee mema mbele ya safari.

Lakini kuna uwezekano mkubwa Mayele anaumwa ugonjwa wa kupenda nyumbani (home sickness). Tayari Tanzania kulishakuwa nyumbani kwake na aina ya maisha ya Tanzania yalimuingia kwelikweli. Maisha ya uwanjani, mitaani na mitandaoni. Tanzania bado haijamtoka. Bado ipo akilini mwake. Mwili upo Misri, lakini akili ipo Tanzania.

Inawatokea wageni wengi waliowahi kuishi Tanzania. Sio tu wanasoka kama kina Bernard Morrison ambao tunaona kila siku wanazurura Dar es salaam ingawa wanacheza soka la kulipwa Morocco, lakini pia kwa wageni wengine. Hata kuna mabalozi wa nchi za nje hawaishi kurudi kutembea Tanzania baada ya muda wao kwisha.

Mayele sio maarufu DR Congo kuliko Tanzania. Hii ina maana simu yake yote ina habari za Tanzania na yeye binafsi angependa kuwa sehemu ya habari hizo. Haishangazi kuona haachi kuzusha jambo hili na lile. Inawezekana kweli alipitia anachopitia lakini inawezekana pia imewatokea wachezaji wengi waliopita Simba na Yanga, hata hivyo hawana habari ya kulalamika kupitia simu zao wala redioni. Niliwahi kusikia mahali Azam wamemwambia Prince Dube arudishe nyumba aliyopangiwa na Azam. Sijawahi kusikia Dube akilalamika kupitia mtandao wa Instagram. Clatous Chama amepitia kipindi kigumu Simba ikiwemo kusimamishwa karibuni. Umewahi kumuona Chama akielezea kilichotokea? Alichofanya ni kuitakia heri Simba kila inapocheza. Mashabiki wanatukana lakini anakaa kimya. Hivi ndivyo anavyotakiwa kuwa mchezaji wa kulipwa. Mchezaji ni jalala. Kocha ni jalala. Kiongozi wa timu ni jalala. Mashabiki tu ndio ambao wanajiona kuwa wapo sawa kwa kila jambo.

Hapo hapo imenishangaza kuona Mayele akiibukia katika kambi ya timu nyingine na kufanya mahojiano na mtandao wa klabu. Sielewi utaratibu wa Pyramids uko vipi lakini ndani na nje ya Tanzania jambo hilo haliruhusiwi na klabu nyingi. Walau kama angekuwa mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, lakini ni klabu ambayo hajawahi kugusa jezi yake.

Kitu kibaya zaidi ni pale alipoonekana kama anatoa siri za klabu. Namna rais alivyomfukuza kocha. Namna ambavyo hawapewi posho licha ya kulipwa mishahara mikubwa. Hayakuwa mazungumzo ya maana kuzungumzia mambo hayo. Mshikamano ndani ya klabu unaweza kupungua kwa kiasi kikubwa.

Mwisho wa yote nadhani Mayele angejikita zaidi na kazi yake huku Yanga pia wakijikita na kazi yao. Nadhani Yanga wapo bize zaidi na kazi yao na ndio maana wamefanikiwa kuziba pengo la mchezaji mwenyewe. Hawajaziba kwa uwezo binafsi wa mchezaji mmoja, bali kwa uwezo wa kitimu katika kutumia nafasi mbalimbali wanazopata. Mayele angeisahau kidogo Tanzania akajikita katika mshahara mkubwa anaoupata kwa sasa. Tanzania ipo tu. Anaweza kurudi baadaye akaangukia Simba au Azam. Ni jambo la muda tu kwa namna ambavyo anaonekana anaipenda Tanzania. Lakini kwa sasa angeiweka simu yake kando na kuwa bize zaidi na kazi yake ya soka.

Ukiangalia kwa haraka haraka tu Mayele na Yanga hauoni tatizo la msingi. Ni upotevu wa muda tu ambao hauna maana yoyote. Sioni sababu ya Yanga kugombana na Mayele wala sababu ya Mayele kugombana na Yanga. Mchezaji akishahama hakuna sababu ya mgogoro mwingine wa muda mrefu. Labda kama mgogoro wa malipo yake anayodai, au mgogoro wa klabu kutolipwa pesa na klabu aliyohamia. Mengine yanakuwa hayana sababu.