HISIA ZANGU : Madagascar wamekusanya kina Farid Mussa wengi

Muktasari:
Maisha yao ni mapambano. Kuna kundi kubwa la wachezaji katika madaraja ya chini ambalo linapambana kwa ajili ya kujiuza kwenda madaraja ya juu na kuna wale waliowekwa katika klabu hizo kama Farid kwa ajili ya kupata uzoefu wa kucheza Ulaya kisha kwenda timu kubwa.
UNAWASHANGAA Madagascar? Ni kama Farid Mussa tu. Nilimpenda Farid Mussa niliyemuona katika michuano hii. Anajiamini. Ana kasi. Anajua anachokifanya. Ile pasi yake kwa Mbwana Samatta kuelekea bao la pili la Taifa Stars dhidi ya Kenya ilikuwa maridadi.
Achilia mbali Samatta na Genk yake, Farid alikuwa anaonyesha kuwa tofauti na wachezaji wengi wa Stars. Akiupata mpira haumnyang’anyi kiurahisi. Anajiamini katika njia anazotaka kupita bila ya kuhofia stamina yake. wachezaji wetu wengi walishindwa walau kuulinda mpira na kuchukua maamuzi binafsi. Ilikuwa kama vile mpira ni kaa la moto.
Kwanini Farid? Wachunguze wachezaji wa Madagascar wengi wanacheza katika aina ya timu ambayo Farid anacheza pale Hispania. Sio timu ya juu sana, lakini ni tofauti na kucheza nyumbani. Farid anacheza katika Klabu ya Tenerife ya Hispania. Hii si Barcelona, Real Madrid wala Atletico Madrid, ila ni tofauti kubwa na kucheza nyumbani.
Maisha yao ni mapambano. Kuna kundi kubwa la wachezaji katika madaraja ya chini ambalo linapambana kwa ajili ya kujiuza kwenda madaraja ya juu na kuna wale waliowekwa katika klabu hizo kama Farid kwa ajili ya kupata uzoefu wa kucheza Ulaya kisha kwenda timu kubwa.
Wachezaji kama kina Diego Costa walipelekwa Ulaya kule Ureno na kucheza Ligi Daraja la Pili kama kituo cha muda kwa ajili ya kuuzwa kwenda timu kubwa. Hawa ni wapambanaji hasa. Ligi Daraja la Tatu Ulaya ni kitu tofauti kabisa na Ligi Kuu ya Tanzania.
Staa wa Madagascar, Faneva Adriatisma anacheza Klabu ya Clemont Foot ya Daraja la Kwanza Ufaransa. Ligue 2. Hauwezi kumfananisha na John Bocco aliyecheza mpira wake wote katika Ligi Kuu Bara.
Kiungo wao mahiri, Anicet Abel anacheza katika Ludogorets Razgard ya Ligi Kuu ya Bulgaria ambayo pia inashiriki katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Kiungo wao mwingine mahiri, Rayan, Ravelson anacheza Troyes iliyopo Ligi Daraja la kwanza Ufaransa.
Beki wao wa kulia aliyepika bao la pili dhidi ya DR Congo, Romain Metanire anacheza Minnesota United ya Ligi Kuu ya Marekani. Beki wao wa kati, Thomas Fontaine anacheza Stade de Reims ya Ligi Kuu ya Ufaransa.
Hawa ni mifano tu, lakini kuna mchezaji mmoja au wawili wanaocheza Madagascar. Kwa ukweli wa dhati, Madagascar wanaelekea mwisho wa safari yao. Wanacheza pambano lijalo la robo fainali dhidi ya Algeria. Hapo tutaweza kuona tofauti ya uzoefu kati ya Algeria na Madagascar.
Hapo tutaona tofauti kati ya wachezaji wa Manchester City kama Riyad Mahrez na wale wa Madagascar ambao timu zao sio kubwa sana. Lakini katika hali ya kawaida usiwadharau Madagascar kwa sababu kwa hali ya kawaida walikusanya kina Farid Mussa wengi wa kuwafikisha walipofika.
Kama wachezaji hawa wangekuwa wanatoka katika Ligi Kuu ya Madagascar ningeshangaa sana na ningesafiri mpaka kwenda Madagascar kujua ni kitu gani ambacho klabu zao zimefanya kuweza kutoa wachezaji wa kufika robo fainali.
Lakini baada ya kufuatilia vema wasifu wa wachezaji wao nadhani hakuna kitu kikubwa cha kushangaa. Walitazamiwa kufanya hivi siku moja kama wangeamua kujituma. Msingi wa kuanzia walikuwa nao tofauti na wachezaji wa Taifa Stars.
Wachezaji wao wanalelewa kishindani katika timu zenye miundombinu na ambazo zinawafanya kila mwisho wa wiki wapambane na timu nyingine. Lilikuwa ni suala la muda tu kabla ya wao kushiriki Afcon kwa mara ya kwanza na kufika robo fainali.
Leo tuna ligi ambayo timu ya kihistoria kama Coastal Union inafika Dar es salaam kutoka Tanga siku hiyohiyo na kucheza siku hiyohiyo na kuchapwa mabao 8-0. Ni rahisi kujisifu na kushangilia, lakini kumbe hawakuandaliwa kucheza Ligi Kuu. Na bado timu ipo Ligi Kuu.
Huo ni mfano mmoja kati ya mifano mingi kuelekea katika kutengeneza timu ya taifa mbovu ambayo imesheheni asilimia 80 ya wachezaji wanaocheza ndani. Tulitegemea nini Cairo? Lakini kama tungekuwa na kina Farid Mussa wengi si ajabu nasi tulikuwa na nafasi ya kujigeuza Madagascar.
Haya yote yanatokea wakati Ibrahim Ajibu anagoma kwenda TP Mazembe, anasaini Simba na watu wanashangilia. Wanataka aimarike kupitia mechi dhidi ya JKT Tanzania, Mwadui na Ndanda. Unashindana vipi na mchezaji ambaye anacheza Klabu ya Troyes na anashindana kila wikiendi?
Sitaki kuzizungumzia timu kubwa ambazo zina wachezaji wakubwa wanaocheza Ulaya katika klabu kubwa zinazojulikana. Ni vema kuwazungumzia Madagascar kwa sababu bado ni timu ndogo, lakini walipofika bado sisi hatujasogelea. Nenda katika Wikipedia kisha pitia uone wachezaji wao wanacheza wapi. Hawajafika walipofika kwa bahati mbaya.