HII NDIO AL- DUHAIL SC, INAYOMTAKA OLUNGA

New Content Item (1)
New Content Item (1)

UNAAMBIWA Nyota ya mja ikiamua kuwaka, hakuna wa kuizima, na kitu pekee kinachoweza kuzuia riziki ni kudra za Mungu. Naam, sio habari mpya tena, ni kwamba baada ya kupiga shughuli la kibabe huko Japan, waarabu wa Qatar wanamtaka Michael Olunga.

Tena sio kwa kubahatisha, Al-Duhail SC, imedhamiria kabisa kuhakikisha Olunga anakuwa wao, kwa kutangaza ofa ya kutisha. Euro 7 milioni, sawa na Ksh920 milioni, ndio ofa iliyofika mezani kwa Kashiwa Reysol, anayochezea mchezaji huyo bora na mfungaji bora wa J1 League.

Taarifa za Olunga kutakiwa na klabu hiyo, zilianza mara tu baada ya msimu wa ligi ya Japan, kumalizika, ambapo Straika huyo, amemaliza akiwa kinara wa mabao, baada ya kufunga mabao 28, pamoja na kutwaa tuzo ya mchezaji bora (2020 Meiji Yasuda Life J-League).

Taarifa hizo zinasema kuwa, Kashiwa Reysol, imeshakubali ofa hiyo na kwamba mazungumzo yameanza, kwa lengo la kufanikisha uhamisho wa Olunga kwenye Al-Duhail, kuchukua nafasi ya straika wa zamani wa Juventus Mario Mandzukic, aliyegura mwaka jana.


Al-Duhail SC ni kina nani?

Wengi hawaifahamu kabisa klabu hii. Hii ni mara ya kwanza kwa jina hili, kutua kwenye masikio ya wengi. Al-Duhail Sports Club, zamani ikijulikana kama Lekhwiya SC, ni klabu ya michezo nchini Qatar, maarufu kwa mchezo wa soka.

Klabu hii, ipo katika wilaya ya Duhail, ikiwa umbali wa kilomita 12, kutoka mji mkuu wa Doha. Al-Duhail SC, inayonolewa na kiungo wa zamani wa Ufaransa, Sabri Lamouchi (49), inatumia uwanja wa Abdullah bin Khalifa, wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 9,000 pekee.

‘The Red Knights’, iliyolazimika kubadili jina kutoka Lekhwiya SC (Aprili 2017), baada ya kuungana na El Jaish SC, ni klabu ya kwanza kwenye historia ya soka la Qatar, kushinda ubingwa wa ligi daraja la kwanza, katika msimu wao kwanza. Haijawahi kutokea.


Historia yao

Klabu hii wala haikuanza zamani. Historia inaonesha kuwa, Al-Duhail, ilianzishwa mwaka 2009. Wakati huo ilikuwa inajulikana kama Al-Shorta Doha, kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Lekhwiya SC. Ndio klabu inaongoza kwa kuwa na bajeti kubwa zaidi Qatar.

Baada ya kuanzishwa, ilianza kushiriki ligi daraja la pili, ambapo ilimaliza katika nafasi ya nne, kabla ya kutwaa uchampioni, mwaka uliofuata (2010). Katika msimu wa kwanza, kwenye ligi daraja la kwanza (Qatar Stars League), Lekhwiya SC, ilitwaa ubingwa wa msimu wa 2010-11.

Kwa kufanya hivyo, waliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza, katika historia ya soka la Qatar. Katika msimu huo, Lekhwiya SC (Al-Duhail), ilifika fainali ya 2020 Sheikh Jassem Cup, lakini bahati haikuwa yao, mbele ya Al-Arabi.

Mechi yao ya kwanza ya mashindano ya kimataifa, ilichezwa Machi 7, 2012, waliposhiriki 2012 AFC Champions League, ambapo walishinda mchezo wao wa kwanza, dhidi ya Al-Ahli (Saudi Arabia), Nam Tae-Hee akifunga bao pekee la ushindi.

Msimu uliofuata, 2011-12 Qatar Stars League, Al-Duhail SC, ilitetea ubingwa wao, zikiwa zimesalia mechi mbili ligi iishe. Februari 15, 2013 walizindua uwanja wao mpya (Abdullah bin Khalifa Stadium), dhidi ya Al Khor, kabla ya kutetea ubingwa wao kwa mara ya tatu mtawalia.

Baada ya kubadili jina kutoka Lekhwiya SC, hadi Al-Duhail SC, kufuatia muungano wao na El- Jaish SC (Aprili 2017), klabu hii ilimaliza msimu wa 2017–2018, ikiwa klabu ya kwanza, kuwahi kushinda mataji matatu ya msimu; ubingwa wa Ligi, Qatar Cup na Emir Cup.


Kikosi


Kikosi cha mabingwa hawa watetezi, kinaundwa na makipa Mohammed Al-Bakri, Khalifa Ababacar na Ahmed Soufiane (wote Qatar). Mabeki ni Ali Malolah, Sultan Al-Brake, Mohammed Musa, Bassam Al- Rawi, Ahmed Yasser, (wote Qatar), Medhi Benatia (Morocco).


Viungo ni Ismaeel Mohammad (Qatar), Luiz Junior (Qatar), Edmilson (Belgium), Karim Boudiaf, Abdullah Al-Ahrak, Abdelrahman Moustafa, Ali afif, Assim Madibo, Salmin Atiq (wote Qatar), Youssef Msakhni (Tunisia), Dudu (Brazil) na Ali Karimi (Iran).


Safu ya Ushambuliaji ya timu hii, inayotumia jezi za rangi nyekundu kwa mechi za nyumbani na kijivu kwa mechi za ugenini, ambayo mwaka jana ilikuwa chini ya Mario Mandzukic, inaongozwa na Almoez Ali na Mohammed Muntari (wote Qatar).


IMEANDIKWA NA FADHIL ATHUMAN