Hersi: Twendeni uwanjani, mechi haijaahirishwa

Rais wa Yanga, Hersi Said amekanusha taarifa za kuahirishwa kwa mchezo wao dhidi ya US Monastir akisema mashabiki wao waendelee kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hersi amesema mpaka sasa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha lakini bado hakuna taarifa waliyopokea ya kuahirishwa kwa mchezo wao.

Amesema hata wao viongozi wako njiani kuelekea uwanjani kutokana na taratibu za mchezo huo kubaki palepale.

"Hatujapokea taarifa yoyote kutoka kwa wanaosimamia mashindano haya ambao ni Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na wenyeji wao Shirikisho letu hapa Tanzania (TFF),"amesema Hersi

"Kitu ambacho nataka niwaambie mashabiki wetu kama hawajatoka majumbani basi muda huu watoke haraka twendeni uwanjani tutapata muafaka hukohuko hata sisi viongozi tupo njiani.

Tangu mchana mvua zimeanza kunyesha sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam sambamba na Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao utatumika kwenye mchezo huo wa hatua ya makundi.