Heh! Bebi wangu anaachwa!

Muktasari:

Lakini mkewe ambaye ni Mcongomani anayeitwa, Bijoux Mbelenge anashangaa habari za kuachwa kwa mumewe ndani ya kikosi hicho kwa sababu alimshuhudia akifanya vizuri kwa kipindi chote cha maisha yake Yanga.

MKATABA wa kiraka wa Yanga, Mnyarwanda Mbuyu Twite unasoma siku 30 yaani utakwisha Desemba mwaka huu, lakini mchezaji huyo amesema, hana wasiwasi juu ya hilo na kila kitu amemwachia Mungu.

Lakini mkewe ambaye ni Mcongomani anayeitwa, Bijoux Mbelenge anashangaa habari za kuachwa kwa mumewe ndani ya kikosi hicho kwa sababu alimshuhudia akifanya vizuri kwa kipindi chote cha maisha yake Yanga.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mbuyu ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani kama beki ya kati, pembeni na kiungo alisema: “Sijui lolote, bado nina mkataba na Yanga, lakini kwangu kila kitu nimemwachia Mungu lolote litakalotokea sawa tu.”

“Natambua kiwango changu anayejua anajua, sijali juu ya habari hizo kwani Yanga nimeitumikia kwa kipindi kirefu nao wanajua uwezo wangu, lakini mwisho wa yote kama nilivyosema awali, kila kitu nimemwachia Mungu,”alisema.

Naye mke Mbuyu alisema: “Mbuyu ni mchezaji mzuri na kwa kipindi chote amecheza kwa kiwango Yanga sasa hizo habari za kuachwa mimi sijui na kama kweli iko hivyo ni sawa, sisi kila kitu tumemwachia Mungu.”

Hata hivyo, Mbuyu hakutaka kuzungumzia mkataba wake, lakini Mwanaspoti inatambua unaisha mwezi Desemba na hadi sasa Yanga bado haijaanza kufanya mazungumzo naye.