Hee! Kumbe Mgeta alipasuliwa mara mbili

Muktasari:

  • Mgeta amefichua hayo wakati akiwa kwenye programu maalumu ya mazoezi mepesi kabla ya kujiunga na kikosi cha kwanza cha timu yake ambayo ipo kwenye harakati za kupanda daraja.

IMEBAINIKA beki Mtanzania, Emily Mgeta anayeichezea VfB Eppingen ya Ligi Daraja la tano ‘Verbandsliga’ nchini Ujerumani alifanyiwa upasuaji wa bega lake la kushoto mara mbili.

Mgeta amefichua hayo wakati akiwa kwenye programu maalumu ya mazoezi mepesi kabla ya kujiunga na kikosi cha kwanza cha timu yake ambayo ipo kwenye harakati za kupanda daraja.

“Upasuaji wa kwanza ulifanyika kuunga mfupa kisha nikaambiwa niendelee kufanya mazoezi taratibu (Physiotherapie) kisha baada ya miezi saba, wakafanya upasuaji wa pili wa kunishona mdomo wa bega,” alisema Mgeta.

Akizungumzia uwezekano wa VfB Eppingen kupanda daraja, Mgeta alisema utategemea na matokeo yatakayopatikana kwenye michezo iliyosalia.

“Tupo nafasi ya tano, ili tupande daraja moja kwa moja inatakiwa tumalize kwenye nafasi mbili za juu, kilichopo ni kuendelea kukazana kupata matokeo ya ushindi kwenye michezo mfululizo.

“Utofauti wa pointi ni mdogo, bado kuna michezo 14 ambayo imebaki kwetu, lengo letu ni kumaliza kwenye nafasi mbili za juu ili kupanda lakini kama tukiteleza basi tusikose nafasi ya kucheza mchujo,” alisema Mgeta.