Hawa hapa mastaa waliorejesha mataji Yanga

Muktasari:

  • Safari ya kutwaa ubingwa huo kwa Yanga ilihusisha jumla ya wachezaji 34 ambao katika nyakati tofauti walipambana kuhakikisha taji hilo linarejea Jangwani katika msimu huo.

Juni 25, 2022 ilikuwa ni siku ya furaha isiyo na kifani kwa Yanga kwa kukabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2021/2022 baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukata ulioikabili timu hiyo.

Siku hiyo, Yanga ilikabidhiwa taji la ubigwa kwa mara ya 28, ikiwanyang’anya watani zao wa jadi Simba, ambao walikuwa wameutwaa kwa misimu minne iliyopita mfululizo, pia ni msimu huo huo Yanga ilitwaa taji la ASFC baada ya kulisotea kwa muda mrefu tangu ilipobeba mara ya mwisho 2015-2016.

Safari ya kutwaa ubingwa huo kwa Yanga ilihusisha jumla ya wachezaji 34 ambao katika nyakati tofauti walipambana kuhakikisha taji hilo linarejea Jangwani katika msimu huo.

Hata hivyo, katika wanajeshi hao 34, wapo walioanza msimu na timu, pia wapo walioongezeka kwenye dirisha dogo na wapo walioondoka bila kumaliza msimu huo.

Msimu uliopita, Yanga ilitetea tena taji hilo ikilibeba kwa mara ya 29, na msimu huu ipo kwenye mbio za kulitetea tena lakini bado inahitajika kazi ya ziada kwani mechi bado nyingi.

Katika safari hiyo ya kuendeleza ubabe kwenye Ligi Kuu, Yanga imefanya mabadiliko makubwa katika kila eneo lakini kwa wachezaji yamefanyika makubwa zaidi.

Kwa sasa ina kikosi kipya kabisa na ndani yake kuna wachezaji 11 tu ambao wamepenya na kuendelea kusalia Jangwani kati ya wale 34 waliofanya mapinduzi kwa kurejesha ubingwa msimu wa 2021/2022.

Mwanaspoti kupita makala haya linakuletea uchambuzi wa wapi walipo mastaa wa Yanga waliohusika katika mapinduzi ya Ubingwa 2021/2022 bila kusahau hao 11 bora waliosalia Jangwani hadi sasa. Tiririka.

MAKIPA

Yanga katika safari hiyo ilianza na makipa rasmi watatu, Djigui Diarra, Erick Johora na Ramadhan Kabwili, lakini baadae katika dirisha dogo ilimwondoa Kabwili na kumwongeza Aboutwalib Mshery akitokea Mtibwa Sugar.

Hadi sasa katika makipa hao wanne, ni Diarra na Mshery pekee wamesalia Yanga, wengine wameondoka. Johora kwa sasa yupo Mashujaa huku Kabwili akiwa hana timu.

MABEKI

Hapa Yanga ilianza msimu ule na mabeki 10, Djuma Shaban, Kibwana Shomari, David Bryson, Adeyum Saleh, Yassin Mustafa, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Dickson Job, Bakari Nondo, Paul Godfrey ‘Boxer’ na Yanick Bangala na dirisha dogo kumuongeza Ibrahim Hamad ‘Bacca’.

Kati ya hao wote, wanne Job, Kibwana, Mwamnyeto na Bacca ndio wamebaki tu wengine wote wameondoka Jangwani ambao  ni Djuma Shaban (hana timu), Bryson yupo (JKT Tanzania), Adeyum anacheza Dodoma Jiji, Mustafa yupo Mtibwa, Ninja yupo Lubumbashi Sports ya DR Congo, Boxer yupo Ihefu na Bangala anakipiga Azam FC.

VIUNGO

Yanga iliuanza msimu wa 2021/2022 na viungo 11, Khalid Aucho, Mukoko Tonombe, Deus Kaseke, Feisal Salum, Zawadi Mauya, Saido Ntibanzokiza, Farid Mussa, Balama Mapinduzi, Jesus Moloko, Ditraim Nchimbi na Dickson Ambundo na kwenye dirisha dogo ikawaongeza Salum Abubakari ‘SureBoy’ na Denis Nkane.

Kati ya hao 13, watano tu, Aucho, Mauya, Farid, Sure Boy na Nkane ndio wamesalia Jangwani wengine wameondoka na Mukoko yupo TP Mazembe, Saido anacheza Simba, Balama anakipiga Mashujaa, Ambundo yuko Singida FG, Moloko yupo Al Sadaqa ya Libya na Nchimbi ametua Etincelles ya FC ya Rwanda.


WASHAMBULIAJI

Msimu huo Yanga ilianza na washambuliaji wanne, Fiston Mayele, Yacouba Songne, Heritier Makambo na Yusuph Athuman, lakini dirisha dogo iliwaongeza Chico Ushindi na Chrispin Ngushi.

Hata hivyo, katika washambuliaji wote hao, hakuna hata mmoja aliyepo kwenye kikosi cha sasa cha Yanga, kwani Mayele yupo zake Pyramids ya Misri, Yacouba yupo Arta/Solar7 ya Djibouti, Makambo anakipiga Al Murooj ya Libya, Ngushi yupo Coastal Union, wakati Chico na Yusuph wakiwa huru.

BENCHI LA UFUNDI

Katika benchi la ufundi la Yanga msimu huo waliongozwa na kocha Mkuu, Nassredine Nabi, akisaidiana na Cedric Kaze, huku kocha wa viungo akiwa Helm Guldech na wa makipa akiwa Milton Nionev.

Kati ya hao wote hakuna hata mmoja aliyesalia kwenye kikosi cha sasa cha Yanga, kwani Nionev yeye yupo timu ya taifa ya Botswana, huku Nabi akiwa Far Rabat ya Morocco, Kaze akiwa huru na Helm yupo Kaizer Chiefs ya Afrika.