Hasira za Bandari zihamie Ligi Kuu Kenya

Muktasari:
Kufuatia kuondolewa katika mashindano hayo, Horoya FC hivi sasa wamefuzu kuingia katika hatua ya makundi ya Shirikisho.
Mombasa, Kenya.BANDARI FC FC iliyopigwa full-stop na Horoya AC ya Guinea kwenye mashindano ya Caf Confederation Cup, imetakiwa itumie nguvu zake zote kuhakikisha kushinda taji la Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Admiral Youth FC, Aref Baghazally alipokuwa akiipongeza timu hiyo kwa jinsi ilivyojitahidi kwenye mechi zao ingawa ilibanduliwa nje ya dimba hilo la barani Afrika.
“Tunastahili kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi la Bandari FC kwa jitihada iliyofanya timu katika ushiriki wake wa mashindano hayo ya Caf Confederation,” akasema Baghazally.
“Tunaamini wachezaji wamepata uzoefu na watafanya vizuri msimu ujao.”
Alimwambia Kocha Mkuu wa Bandari FC Bernard Mwalala awaandae vijana kwa mechi za Ligi Kuu ili timu ipate kushinda na kuwa timu ya pili ya Mkoa wa Pwani kutwaa kombe hilo baada ya klabu ya Feisal FC kuwa washindi mnamo mwaka 1965.
Pia, baadhi ya mashabiki wa Mombasa wakaipongeza timu hiyo kwa mafanikio iliyoyapata katika mashindano hayo makubwa barani Afrika.
John Kivuki wa Malindi anasema Bandari wanastahili sifa kwa kupigana kiume japo wametolewa mashindanoni.
“Tunataka msimu huu timu yetu hiyo ishinde kombe la Ligi Kuu ambalo tunalitamani sana,” akasema Kivuki.
Ramadhan Sudi wa Msambweni anasema wangelipendelea timu ya Bandari FC nyakati hawana mechi watembelee sehemu hiyo ambayo anadai ina wanasoka wengi wazuri wanaoweza kuichezea na kuihami kwenye mechi zao.
“Mkoa wa Pwani una wanasoka wengi wazuri wanaoweza kusajiliwa na Bandari. Tunawaomba maofisa wa klabu yetu hiyo wawafikirie na kuwajaribu kwani nina uhakika wataweza kucheza kwa ari ya kuipatia ushindi,” akasema Sudi.
Kufuatia kuondolewa katika mashindano hayo, Horoya FC hivi sasa wamefuzu kuingia katika hatua ya makundi ya Shirikisho.