Hapa Simba ilizidiwa ujanja!

Muktasari:
Mfano wa mashambulizi makali aliyookoa ni lile la Meddie Kagere dakika ya 27 na mpira wa tiktak uliopigwa na Sharaf Shiboub katika dakika ya 43 ya mchezo ambayo wengi walidhani yangezaa mabao.
JICHO la Mwanaspoti lilifuatilia mchezo huo kwa dakika zote 90 na ifuatayo ni tathmini ya mchango wa mchezaji mmojammoja katika kikosi cha kila timu na kwa namna gani alichangia katika kupatikana matokeo hayo.
MWADUI
Mahmoud Amir-8
Alifanya kazi nzuri katika kuilinda milingoti mitatu ya Mwadui FC katika mchezo wa jana akiipanga vyema safu yake ya ulinzi na kuokoa mashambulizi ya mara kwa mara ya Simba ambayo yalielekezwa langoni mwake.
Mfano wa mashambulizi makali aliyookoa ni lile la Meddie Kagere dakika ya 27 na mpira wa tiktak uliopigwa na Sharaf Shiboub katika dakika ya 43 ya mchezo ambayo wengi walidhani yangezaa mabao.
Rodgers Gabriel-6
Aliuweka upande wa kushoto wa Simba kwenye wakati mgumu kutokana na namna alivyokuwa anapandisha mashambulizi ya mara kwa mara ya Mwadui kutokea upande wa kulia. Lakini alionyesha uimara katika kuzuia kwa kiasi kikubwa alimudu kumdhibiti Clatous Chama asilete madhara.
Khalfan Mbaruku-5
Alionekana kujikita zaidi katika ulinzi lakini mara chache alizopanda mbele alionekana kuwa na madhara kutokana na krosi zake. Ikumbukwe bao la kwanza la Mwadui lililofungwa na Gerald Mathias lilitokana na krosi yake.
Agustino Samson-8
Alishirikiana vyema na Joram Mgeveke katika kumdhibiti Kagere ambapo alihakikisha anakuwa wa kwanza kuucheza kila mpira ambao mshambuliaji huyo tishio wa Simba alipigiwa.
Joram Mgeveke-7
Aliiongoza vyema safu ya ulinzi ya Mwadui ambapo aliwapanga vizuri mabeki wenzake na kusahihisha makosa ambayo walikuwa wanayafanya mara kadhaa. Alicheza kwa utulivu na aliondosha hatari nyingi zilizoelekezwa langoni mwake.
Emmanuel Memba-8
Uwepo wake kwenye safu ya kiungo ya Mwadui FC ulikuwa na maana kubwa kutokana na jinsi alivyotengeneza balansi ya kitimu ndani ya uwanja kwa kuilinda vyema safu ya ulinzi na kuichezesha timu.
Alipora mipira na kutibua mipango ya Simba katikati mwa uwanja lakini kubwa zaidi alipiga pasi sahihi kwenda mbele ambazo zilionekana kuiweka Simba kwenye wakati mgumu.
Hassan Kapalata-6
Kukosa kwake utulivu kuliinyima fursa Mwadui kupata idadi kubwa ya mabao katika mchezo wa jana kwani alipoteza nafasi kadhaa kwa kupiga mashuti yaliyotoka nje au kupaa huku akiwa kwenye nafasi nzuri na lango la wapinzani.
Mussa Nampaka-7
Alitengeneza muunganiko mzuri na Memba katikati mwa uwanja katika kuinyima uhuru Simba kujenga mashambulizi kutokana na uwezo wake wa kuichezesha timu na kukaba kuanzia kwenye eneo la adui jambo ambalo liliwalazimu viungo na mabeki wa Simba kutocheza mpira wa chini na kujenga mashambulizi.
Gerald Mdamu -9
Ni mchezaji ambaye alionyesha uchu wa kufumania nyavu tangu mwanzoni mwa mchezo kutokana na namna alivyokuwa akijipanga pale ambapo timu yake ilipokuwa inashambulia.
Alifanya mashambulizi mawili ya nguvu kipindi cha kwanza ambapo miongoni mwa hayo moja lilizaa bao la Mwadui dakika ya 32 ambalo liliamua mchezo na kuipa ushindi timu yake.
Ludovick Venance-3
Mwadui ingeweza kuibuka na ushindi wa idadi kubwa ya mabao kama Ludovick angekuwa na utulivu kwani ndiye mchezaji ailiyepata mipira mara kwa mara akiwa kwenye lango la Simba lakini pupa zake zilipelekea apoteze nafasi hizo.
Omary Daga-5
Hakuwa na kasi na alionekana kupooza tofauti na alivyozoeleka. Hakumsaidia beki wake wa pembeni wakati wa kujilinda lakini hata kwenye kushambulia hakuonekana kuwa na mchango mkubwa.
Simba
Aishi Manula-6
Alitimiza majukumu yake ya msingi katika nafasi yake, akiwapanga vyema mabeki wake na kuokoa hatari zilizoelekezwa na washambuliaji wa Mwadui. Hapaswi kulaumiwa kwa bao alilofungwa jana kwani halikutokana na uzembe wake.
Haruna Shamte-3
Alizidiwa ujanja na mawinga wa Mwadui na upande wake ulionekana kuelemewa na kutumiwa mara kwa mara na wapinzani wao kupeleka mashambulizi langoni mwake. Ni upande wa Shamte ambao uliruhusu krosi iliyozaa bao la Mwadui.
Gadiel Michael-5
Alijitahidi kupandisha mashambulizi lakini idadi kubwa ya krosi alizopiga zilipotea bila kuzaa matunda. Alishindwa kumdhibiti Gerald Mathias asiifungie bao Mwadui FC wakati alipounganisha krosi ya Khalfan Mbaruku.
Erasto Nyoni-4
Hakuwa na siku nzuri jana kwani alipitwa kirahisi na washambuliaji wa Mwadui na kuiweka safu ya ulinzi ya Simba matatani. Alionekana kupooza na alimpa wakati mgumu Tairone Da Silva.
Tairone Santos-6
Alijitahidi kurekebisha makosa ya Erasto Nyoni lakini hata hivyo, alifanya uzembe wa kutokuwa kwenye eneo sahihi wakati Mwadui walipofanya shambulio lililozaa bao na pengine uwepo wake ungesaidia kuokoa shambulizi hilo akisaidiwa na umbile lake kubwa.
Gerson Vieira-2
Simba ilikosa muunganiko mzuri katikati hasa kipindi cha kwanza na kwa kiasi kikubwa hilo lilichangiwa na kiwango cha chini kilichoonyeshwa na kiungo huyo raia wa Brazil. Alifanya faulo za mara kwa mara alipoenda kuwania mpira na adui na alipotezwa na viungo wa Mwadui.
Francis Kahata-4
Alicheza taratibu na hakuwa na madhara kwa Mwadui. Idadi kubwa ya krosi alizopiga zilipotea na alikosa ubunifu wa kupenya mabeki wa timu pinzani.
Mzamiru Yassin-7
Ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Simba walioonyesha uhai kwenye mchezo wa jana. Aliichezesha vyema timu kwa kupiga pasi zilizofikia walengwa kwa usahihi lakini pia alisaidia katika kupika na kushiriki kwenye mashambulizi ambayo Simba waliyafanya.
Meddie Kagere-3
Jana hakufurukuta mbele ya Jerome Mgeveke na Agustino Samson. Alikosa huduma sahihi kutoka kwa wenzake jambo lililowapa urahisi mabeki wa Mwadui kumdhibiti.
Sharaf Shiboub-2
Hakuonyesha makeke na alipoteza mipira mara kwa mara na hakushangaza kuona akifanyiwa mabadiliko kabla ya kipindi cha pili kuanza.
Clatous Chama-4
Kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele ndivyo Chama anavyozidi kuporomoka kiwango na hilo limejidhihirisha jana ambapo kasi yake ilikuwa ndogo kulinganisha na msimu uliopita. Chama alikosa ubunifu wa kutengeneza nafasi na alipiga pasi nyingi za kwenda pembeni au nyuma ambazo hazikuwa na faida kwa Simba.
Walioingia
Miraji Athuman-5
Kwa muda aliocheza alionyesha kuwa hatari kwa mabeki wa Mwadui ambao walimfanyia faulo za mara kwa mara lakini hata hivyo hazikutumiwa vyema na Simba.
Hassan Dilunga-6
Alijitahidi kuufungua mchezo kwa kuhaha huku na kule lakini mipira yake ya mwisho aliyoipiga kuelekea langoni mwa Mwadui, haikuwa na faida kwani mara kwa mara ilitua miguuni au vichwani mwa mabeki wa wapinzani wao.
Ibrahim Ajibu-7
Alistahili kuingia mapema kwenye mchezo wa jana kwani kwa muda aliocheza, aliifanya Mwadui kurudi nyuma na kutopanda mbele kama ambavyo ilikuwa ikifanya kipindi cha kwanza.
Ajaribu kupenyeza mipira kwenda langoni mwa Mwadui lakini wachezaji wa Simba walishindwa kujipanga vyema katika nafasi ili kuweza kupata mipira kutoka kwake.