Hapa lazima kazi ipo

Mrisho Ngassa akishughulika uwanjani
Muktasari:
Tofauti na Kocha wa Simba, Patrick Phiri ambaye huu ni mchezo wake mwingine dhidi ya Yanga, Kocha wa Yanga, Marcio Maximo ndiyo anashiriki kwa mara ya kwanza mechi ya watani, hivyo ana mtihani mkubwa mbele ya mashabiki wa timu yake ambao wanahitaji matokeo mazuri.
TAYARI homa ya pambano la watani wa jadi Simba na Yanga inapanda huku kila upande ukijitahidi kuandaa kikosi chake ili kupata matokeo mazuri Oktoba 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tofauti na Kocha wa Simba, Patrick Phiri ambaye huu ni mchezo wake mwingine dhidi ya Yanga, Kocha wa Yanga, Marcio Maximo ndiyo anashiriki kwa mara ya kwanza mechi ya watani, hivyo ana mtihani mkubwa mbele ya mashabiki wa timu yake ambao wanahitaji matokeo mazuri.
Simba ipo kambini Afrika Kusini na hata wachezaji wake waliokuwa katika kikosi cha Taifa Stars kilichocheza na Benin juzi Jumapili waliifuata timu hiyo jana asubuhi.
Simba inashika nafasi 10 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi tatu tu baada ya kutoka sare tatu dhidi ya Coastal Union (2-2), Polisi Moro (1-1) na Stand United pia sare ya bao 1-1, hali ni tofauti kwa watani zao Yanga ambao wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi sita.
Yanga awali ilifungwa na Mtibwa Sugar mabao 2-0, lakini ikazinduka na kuzifunga Prisons na JKT Ruvu mabao 2-1 katika mechi zake. Mtibwa ipo kileleni ikiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi tatu.
Makocha wanakuna vichwa kuelekea mchezo huu lakini hata wachezaji nao vichwa vyao havijatulia kwani wana wakati mgumu katika nafasi wanazocheza, hebu tazama mchuano ulivyo katika vikosi vya Simba na Yanga;
Casillas na Manyika Peter
Hakuna ubishi kipa namba moja wa Simba, Ivo Mapunda ni majeruhi wa kidole, hivyo hatacheza mechi hii na hata kambini Afrika Kusini hajaenda hii ina maana Hussein Sharrif ‘Casillas’ na chipukizi Manyika Peter ndiyo wanaotegemewa kulinda lango la Simba dhidi ya Yanga.
Wakiwa kambini Afrika Kusini, Kocha Phiri atatazama nani aanze kulinda lango kwani uwezo wa Manyika si mdogo na anaweza hata kumpiku mwenzake na kupewa nafasi kwa mara ya kwanza kwenye mechi ngumu. Kitu kingine kinachochagiza uwezekano wa Manyika kucheza ni ile hali ya Casillas kuwa majeruhi wa ugoko alioumia mazoezini hivyo itategemea na hali yake.
Tshabalala na Baba Ubaya
Phiri ana kazi kubwa ya kuamua nani acheze katika nafasi ya beki ya kushoto kwani wachezaji wote wa nafasi hiyo kuanzia Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Abdi Banda na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wote wako vizuri na wanashiriki mazoezi kikamilifu.
Banda anaweza asichezeshwe kutokana na uzoefu mdogo lakini Baba Ubaya naye japokuwa ametokea katika majeruhi anaweza kupewa nafasi kutokana na uzoefu wake katika mechi kama hizi.
Tshabalala anaweza kuanza pia kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika mechi mbili za mwisho ambazo Simba imecheza dhidi ya Polisi Moro na Stand United, hapa kazi anayo Kocha Phiri.
Edward Charles na Oscar Joshua
Ilipopoteza mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Yanga ilipotea baada ya kuumia kwa beki wake wa kushoto Oscar Joshua ambaye ana nguvu za kuzuia na kupanga mashambulizi, Kocha Maximo akamrudisha kiungo Mbuyu Twite kushoto halafu katikati akampanga Omega Seme, hapo Yanga ikapotea na kufungwa mabao 2-0.
Maximo sasa anamtumia chipukizi Edward Charles aliyezaliwa Aprili 2, 1994 kama beki wa kushoto na amecheza vizuri katika mechi mbili ambazo Yanga imeshinda dhidi ya Prisons na JKT Ruvu.
Utamu wa vita ya nafasi kwa wawili hawa unakuja hata katika timu ya Taifa kwani wote waliitwa kuikabili Benin wikiendi iliyopita. Hata hivyo Joshua ana nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza kutegemea na mfumo wa kocha siku hiyo.
Mgeveke na Isihaka
Kokote ilipo kila shabiki wa Simba ana wasiwasi na nafasi ya mabeki wa kati kwani ukiachana na Joseph Owino mabeki wawili wa kati wa timu hiyo, Joram Mgeveke na Hassan Isihaka bado hawajawashawishi makocha na hata mashabiki kuhusu uwezo wao uwanjani, kwani wana makosa madogo madogo yanayosababisha mabao lakini uzoefu unatajwa kuwa mdogo kwao.
Phiri ataamua kumpanga mmoja kati yao kwani Mgeveke anaonekana kuwa na nguvu na uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya juu huku akiwa na uzoefu mdogo lakini Isihaka ana uzoefu kidogo lakini umakini wa kuzuia unaweza kuwa tatizo kwake.
Ngassa na Msuva
Wote wapo moto na ukitazama kiwango alichoonyesha Mrisho Ngassa juzi Jumapili akiwa na Stars dhidi ya Benin ni hatari kwani Maximo anaonekana kupenda kumwanzisha Msuva katika winga ya kulia ili apate mabao ya haraka akiamini ana uamuzi wa haraka kuliko Ngassa anayependa kuchezea mpira muda mrefu.
Mmoja wao lazima acheze ili wagawane upande na Andrey Coutinho lakini itategemea na mfumo ambao kocha anapanga kuutumia na uwajibikaji wao mazoezini.
Makapu na Dilunga
Kama atataka kujilinda, Maximo atamwanzisha Said Juma ‘Makapu’ ili kuzuia mbinu zote za Simba kupitia katikati lakini kama atataka kushambulia kuanzia mwanzo ni lazima atampanga Hassan Dilunga katikati wakati Mbuyu Twite akiwajibika kuwa kiungo namba sita kama kawaida.