Hao Morocco tunao kesho
MWANZO mzuri. Taifa Stars juzi usiku ilianza vyema mechi za makundi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kuinyoa Niger bao 1-0 na jana ilirejea nchini ili kuikabili Morocco itakaocheza nao kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Kwa jinsi Stars ilivyocheza kwenye Uwanja wa Marrakech, Morocco na kupata ushindi huo uliowapa pointi tatu za kwanza katika Kundi linaloongozwa na Wazambia walioishindilia Congo Brazzaville mabao 4-2, ni wazi kesho Wamorocco kazi wanayo.
Pambano la kesho litakuwa ni la tano kwa timu hizo kukutana kimataifa kwani tayari zilishakutana mara nne zikiwamo mbili za kufuzu Kombe la Dunia 2014 na Tanzania kuifumua Morocco mabao 3-1 nyumbani kabla ya kwenda kupoteza ugenini 2-1 mechi zilizopigwa kati ya Machi na Juni mwaka 2013.
Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa jinsi Stars ilivyocheza na namna inavyoweza kupata matokeo chanya kwa Morocco huku ikikumbukwa kila kundi linahitaji timu moja itakayofuzu fainali hizo zitakazofanyika Canada, Mexico na Marekani (USA).
AMROUCHE HATABIRIKI
Moja ya jambo gumu kulitabiri ni namna Kocha wa Stars, Adel Amrouche atapanga kikosi cha kwanza kwa sababu amekuwa mtu wa kubadilika mara kwa mara kutokana na mpinzani anayekutana naye na kwa kiasi kikubwa amekuwa akipata matokeo chanya.
Licha ya kupata matokeo mazuri ila anapaswa kutambua kwa kocha yoyote ni lazima awe na kikosi cha kwanza kinachoeleweka na mabadiliko yanapotokea iwe kwa sababu tu za msingi ila isiwe mazoea kwani ipo siku yanaweza kumgharimu moja kwa moja.
Ukiangalia mchezo wa juzi Haji Mnoga anayecheza namba mbili kiasili alichezeshwa katikati, hii ni hatari wakati nje una wachezaji wanaoweza kucheza vizuri nafasi hiyo kama Himid Mao na Mudathir Yahya ambao wote walianzia kwenye benchi.
USHAMBULIAJI BADO
Ingawa Stars imepata ushindi huo ila bado kocha Amrouche ana kazi kubwa ya kufanya kwenye eneo la ushambuliaji kutokana na kushindwa kupata mabao mengi licha ya nafasi nyingi kuonekana wazi kutengenezwa kutokea maeneo mbalimbali kiwanjani.
Licha ya kuwategemea Simon Msuva na Mbwana Samatta ila bado safu hiyo hairidhishi hivyo Amroache anapaswa kutupia macho kwa kina eneo hilo kwani kwa kiasi kikubwa ameonekana kufaulu kwenye eneo la ulinzi kutokana na mfumo ambao anautumia.
M’MOMBWA TUMAINI JIPYA
Mfungaji wa bao pekee la mchezo huo, Charles M’Mombwa ameonyesha kwa jinsi gani ni tumaini jipya ndani ya kikosi chetu cha Stars kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha huku ikiwa ndio kwanza mechi yake ya kwanza akiwa na timu ya taifa.
Nyota huyo anayechezea timu ya Macarthur ya nchini Australia licha ya tu ya kufunga ila alikuwa ni kivutio kizuri kwa mashabiki na wachezaji wenzake kutokana na namna alivyokuwa anajituma huku akionekana zaidi nafasi tofauti uwanjani.
KAZI IMEANZA
Mchezo wa kesho dhidi ya Morocco utatoa taswira nzima ya kikosi hicho katika nafasi ya kuwania tiketi ya kufuzu kwenye michuano hiyo kwani licha tu ya ndio kwanza itakuwa mechi ya pili kwetu ila wapinzani wetu ni tishio tofauti na sisi.
Morocco ndio inayopewa nafasi kubwa ya kufuzu michuano hiyo kupitia kundi hilio, kwa vile kila kundi linatoa timu moja, lakini Stars haiwezi kuingia kinyonge na badala yake tunatakiwa kucheza kwa nidhamu kubwa hususan kujilinda vizuri.
Mchezo ni mgumu kwetu na kama nilivyosema awali Amrouche anatakiwa kufanyia kazi eneo lake la ushambuliaji kwani hatutapata nafasi nyingi na hata ikitokea basi tunapaswa kuzitumia vizuri tofauti na ilivyokuwa dhidi ya Niger.
Tukumbuke kundi hili sio jepesi na ukiangalia licha ya ushindi tulioupata ila tuko nafasi pili nyuma ya Zambia yenye pointi tatu tukitofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa hivyo Morocco nayo itataka kuanza vyema kampeni zake.
REKODI TAMU
Mara ya mwisho kukutana ilikuwa pia katika kufuzu fainali za Kombe la Dunia na Stars iliifunga Morocco kwa mabao 3-1, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa yaliyofungwa na washambuliaji, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta aliyefunga mawili.
Katika mchezo huo uliopigwa Machi 24, 2013 bao la Morocco lilifungwa na Youssef El Arabi mwishoni kabisa mwa mechi hiyo huku ikicheza pia pungufu baada ya nyota wa kikosi hicho, Abderrahim Achakir kupata kadi nyekundu dakika ya 79.
WASIKIE MASTAA
Nyota wa Stars, Charles M’Mombwa akizungumza baada ya mchezo huo alisema ni furaha kwake kuifungia timu hiyo bao pekee la ushindi huku akiwataka mashabiki kuendelea kuwaunga mkono katika michezo yao ijayo ili waendelee kufanya tena vizuri.
“Nina furaha kubwa sana leo kufunga bao hilo na kuisaidia timu yetu kupata pointi tatu, bado tuna kazi kubwa ya kufanya na baada ya kumalizia mchezo wetu na Niger, nguvu zetu tunazielekeza kwa Morocco ili tupate kilichokuwa bora,” alisema M’Mombwa, huku mabeki Dickson Job na Bakar Mwamnyeto walifichua watashuka uwanjani na mzuka mwingi kuivaa Morocco.
“Haukuwa mchezo rahisi (dhidi ya Niger), lakini ubora wetu uliamua mchezo, matokeo haya kwetu ni kama chachu kwenye mechi ijayo dhidi ya Morocco ni mchezo mkubwa tukikutana na timu kubwa lakini tutakuwa kwetu mbele ya Watanzania wenzetu tutahitaji ushindi pia,” alisema Job na kuongeza;
“Tuwashukuru serikali na viongozi wetu wa TFF kwa kutupa wepesi wa kutupa ndege ambayo kiukweli imetupunguzia uchovu kwa kiasi kikubwa, mechi zipo karibu sana lakini Watanzania wenzetu waje uwanjani kutupa nguvu sio kutupa presha.
Wakati Job akiyasema hayo beki mwenzake Bakari Mwamnyeto, “Morocco inawachezaji Bora ambao wameshacheza mechi kubwa lakini kwenye soka kila kitu kinawezekana, jambo muhimu ni tunatakiwa kutofanya makosa mengi kama tukitangulia kupata bao la mapema.