Haina ujanja Kirumba

Muktasari:
Mabingwa hao wa zamani wa soka nchini, wanatarajia kuumana na Mwadui katika pambano litakalochezwa Jumamosi ijayo, ikiwa inatokea jijini Mwanza.
SIMBA ipo safarini kwa sasa kuelekea Shinyanga kuwahi pambano lake lijalo la Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui FC.
Mabingwa hao wa zamani wa soka nchini, wanatarajia kuumana na Mwadui katika pambano litakalochezwa Jumamosi ijayo, ikiwa inatokea jijini Mwanza.
Jumamosi iliyopita, timu hiyo ilivaana na Toto Africans kwenye Uwanja wa Kirumba katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara na pambano hilo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Wenyeji Toto walichomoa bao dakika za majeruhi, wakati Wekundu wa Msimbazi wakiamini wameshamaliza kazi.
Bao la Danny Lyanga, lilielekea kufuta ‘gundu’ ambalo Simba imekuwa nayo kila ikivaana na Toto kwenye uwanja huo.
Ni kama Simba ina mkosi na uwanja huo kwani hata kabla ya kushuka daraja na kupanda tena msimu huu, Toto ilikuwa ikiisumbua Simba kwenye uwanja wa Kirumba.
Kwa misimu kama saba ambayo timu hizo zimekutana tangu Toto ilipopanda Ligi Kuu mwaka 2007 na kushuka 2012-2013, Simba iliifunga Toto mara tu kwenye uwanja huo wa Kirumba na baada ya hapo ilikuwa ni mateso kwao.
Mwanaspoti inakuletea mechi ilizokutanisha timu hizo kwenye uwanja huo na hata zile za ugenini Toto ikiifuata Simba nazo ziliwataabisha Msimbazi.
2007-2008
Okt 28, 2007 -Toto 3 Simba 2
Timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza Oktoba 28, 2007 na Toto ikiwa ndio kwanza imetoka kupanda Ligi Kuu msimu huo na katika mchezo huo wa uliopigwa Kirumba, wenyeji waliibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Mabao ya Toto yalifungwa na Philip Alando aliyefunga mawili na jingine beki Said Koko wa Simba alijifunga, huku mabao ya Joseph Kaniki na Haruna Moshi ‘Boban’ yakitumika kuwafuta machozi ya Wekundu wa Msimbazi.
Katika mechi ya marudiano iliyochezwa jijini Dar es Salaam Aprili 14, 2008 Simba ililipa kisasi kwa kuichakaza Toto kwa mabao 3-0 yaliyotumbukizwa na Mkenya Moses Odhiambo aliyefunga mawili na jingine la Mohammed Kijuso.
2008-2009
Oktoba 17, 2008- Toto 4 Simba 1
Kama ulivyokuwa msimu wa nyuma, Simba iliifuata Toto nyumbani katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huo na kwa bahati mbaya dozi yao kwenye Uwanja wa Kirumba iliongezeka maradufu.
Simba na ukali wao wote ikiwa na Mnigeria Orji Obinna walichezea kipigo cha mabao 4-1. Ndio 4-1 wala hujakosea kwa mabao ya Juma Seif aliyefunga mawili, Oscar Joshua na Said Dilunga, huku Obinna akifunga bao pekee na la kufutia machozi la Simba.
Hata hivyo, Simba ililipa kisasi kwenye Uwanja wa nyumba kwa kuilaza Toto bao 1-0 katika pambano lililochezwa Aprili 12, 2009 na kuwa msimu wa pili mfululizo, Simba ikishindwa kuitamba Toto kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza.
2009-2010
Januari 31, 2010 - Toto 0 Simba 2
Baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wao wa kwanza uliochezwa nyumbani jijini Dar es Salaam katika pambano la Sept 5, 2009, Simba iliifuata Toto kwa tahadhari kubwa katika mchezo wao wa marudiano.
Pambano hilo lilichezwa Januari 31, 2010 huku Simba ikiwa na kumbukumbu ya vipigo viwili mfululizo kwenye Uwanja wa Kirumba.
Hata hivyo msimu huu Simba ilikuja kivingine, kwani iliifumua kwa mara ya kwanza Toto kwao kwa mabao 2-0 kwa mabao ya Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Ramadhani Chombo ‘Redondo’.
Huo ndio ushindi pekee ambao Simba iliupata Kirumba katika mechi za Ligi Kuu Bara.
2010-2011
Februari 16, 2011- Toto 2 Simba 2
Toto ilianza msimu huu vibaya kwa kuifuata Simba jijini Dar es Salaam katika mchezo uliochezwa Septemba 25, 2010 na kulazwa mabao 2-1.
Wekundu wa Msimbazi wakaifuata Toto wakijiamini baada ya ushindi wa mechi ya msimu uliotangulia wa 2009-2010, lakini hali haikuwa kama walivyotarajia kwani Toto waliwabadilikia na kutoka nao sare ya mabao 2-2.
Simba ilipata mabao yake kupitia kwa Fete Kang’angi na Mohammed Soud wakati ya Simba yalitumbukizwa kimiani na Rashid Gumbo ‘Chid’ na Mbwana Samatta.
2011-2012 - Toto 3 Simba 3
Msimu huu ndio Simba ilipotwaa taji lao la mwisho la Ligi Kuu Bara ambapo katika mechi zake mbili ilizokutana na Toto nyumbani na ugenini zilimalizika kwa sare.
Ilitoka sare 0-0 jijini Dar es Salaam kabla ya Simba kwenda kufanya kazi ya ziada kuchomoa mabaao ya Toto ikiwamo kipa Juma Kaseja kufunga bao katika mchezo huo ulioisha kwa sare ya mabao 3-3.
2012-2013
Aprili 10, 2013 - Toto 2 Simba 2
Huu ndio uliokuwa msimu wa mwisho wa Toto kuwapo katika Ligi Kuu Bara kabla ya kuibuka tena msimu huu, kwani ilishuka daraja kutokana na pointi ilizokusanya kutotosha kuwabakisha katika ligi hiyo iliyokuwa ngumu msimu huo.
Toto kwa mara ya kwanza iliweza kupata ushindi ikiwa ugenini mbele ya Simba kwa kuilaza bao 1-0 katika mchezo wa kwanza, kabla ya kukutana tena April 10, 2013 jijini Mwanza na Wana Kishamapanda kuendelea kuikamia Simba kwa kuilazimisha sare ya mabao 2-2, ingawa ilishuka daraja.
2015-2016
Desemba 19, 2015 Toto 1 Simba 1
Baada ya juhudi kubwa hatimaye Toto ilirejea katika Ligi Kuu msimu huu na ratiba ikawakutanisha na Wekundu wa Msimbazi kwenye Uwanja wa Kirumba kwa mchezo wa duru la kwanza.
Danny Lyanga alifunga bao dakika ya 22 kiufundi na kuwanyamazisha mashabiki wa Toto, hata hivyo dakika za majeruhi kila mwanasimba akiamini wamevunja mwiko wa kupata ushindi Kirumba, wenyeji Toto walichomoa bao dakika za majeruhi kupitia kwa Everist Benard.