Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HAIJAWAHI KUTOKEA

HAIJAWAHI kutokea. Simba au klabu yoyote ya Tanzania kucheza mechi ya kimataifa usiku wa saa 4 kwenye Uwanja wa Mkapa au ndani ya ardhi ya Tanzania.

Lakini siyo hilo tu, haijawahi kutokea klabu ya Tanzania au Afrika kwenye miaka ya hivi karibuni kufuzu robo fainali ya mashindano tofauti ya Afrika mara mbili mfululizo kwenye misimu inayofuatana.

Simba inawania historia mpya ya ubabe kwa timu za Tanzania katika mashindano ya klabu Afrika wakati itakapoikaribisha US Gendarmerie Nationale ya Niger katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Ikiwa inashika nafasi ya tatu katika kundi D, Simba inaingia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na hesabu moja tu ambayo ni ushindi ili itinge robo fainali ya mashindano hayo na kuungana na timu mojawapo kati ya Asec Mimosas au RS Berkane.

Hadi sasa wakati hatua ya makundi ikifikia tamati, Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba, juu yake zikiwepo Asec Mimosas yenye pointi tisa na RS Berkane iliyo na pointi saba wakati US Gendarmerie inashika mkia ikiwa na pointi tano.


USIKU WA KUFA AU KUPONA

Ni mechi inayoandika historia mpya katika soka la Tanzania kwa ngazi ya klabu kwani ndio itakuwa ya kwanza kuchezwa muda wa saa 4:00 usiku tangu Uwanja wa Benjamin Mkapa ulipoanza kutumika mwaka 2007.

Mechi moja tu ambayo iliwahi kuchezwa kuanzia muda huo ambayo hata hivyo haikuwa ya klabu nayo ni ile ya Taifa Stars dhidi ya Tunisia iliyochezwa Novemba 17, 2020 ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Uamuzi wa mchezo huo kuchezwa saa 4:00 usiku unalenga kuufanya uanze ndani ya muda sawa na ule wa RS Berkane dhidi ya Asec huko Morocco ili kuepuka upangaji wa matokeo baina yao.


TIMU NNE, NAFASI MBILI

Ni siku ambayo presha itakuwa kubwa katika dakika 90 za mchezo kwa timu zote nne zilizopo kundi D kutokana na kila moja kuwa na nafasi ya kufuzu robo fainali kimahesabu kulingana na msimamo wa kundi hilo ulivyo.

Timu yoyote inaweza kumaliza na kicheko na yoyote ikamaliza na kilio pasipo kuangalia inashika nafasi ipi kwa sasa katika msimamo wa kundi.

Asec inayoongoza, itaaga kama itapoteza ugenini dhidi ya Berkane iliyo nafasi ya pili na Simba ikashinda kwa Gendarmerie, wakati Berkane iliyo nafasi ya pili kama itatoka sare halafu mojawapo kati ya Simba au Gendarmerie ikashinda, timu hiyo ya Morocco itatupwa nje.

Simba iliyopo nafasi ya tatu, haitofuzu kama itafungwa au kutoka sare leo na Gendarmerie itahitajika kushinda na kuiombea mabaya RS Berkane vinginevyo itaishia kwenye makundi.


ULINZI KILA KONA

Ofisa usalama anayetambulika na shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (Fifa), Inspekta Hashim Abdallah alisema wamejipanga kikamilifu kushughulikia ulinzi katika mchezo huo.

“Kwenye kila eneo tumejipanga kama inavyofahamika kwamba ni jukumu la Jeshi la Polisi kulinda usalama wa raia na mali zao hivyo watu wasiwe na wasiwasi wowote, kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa. Mchezo huu upo chini ya Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam ambao ndio wasimamizi wakuu kwa maana ya ulinzi.

“Kwa upande wa walinzi wa uwanjani (stewards), tumejipanga vizuri. Hii sio mara ya kwaanza kwa mechi kufanyika muda huo hivyo kwa upande wetu tumejiandaa na bahati nzuri kuna kuna ukomo maalum wa idadi ya mashabiki hivyo hakuna kitakachoharibika na watu wataangalia mchezo kwa usalama mkubwa,” alisema Inspekta Hashim.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Clifford Ndimbo alisema kwa upande wa utawala wamejipanga vilivyo kuhakikisha mchezo huo unachezwa kama ulivyopangwa.

“Bahati nzuri ni kwamba zinapokuja mechi hizi huwa tunashirikiana pande zote. Upande wa serikali, shirikisho, klabu na mamlaka nyingine. Kwa serikali maana yake tunazungumzia, idara kama Jeshi la Polisi, Zimamoto, masuala ya tiketi, uwanja na kadhalika.”

Vikao vimeshafanyika na vingine vinaendelea hivyo niwahakikishie tu kuwa mambo yako vizuri na watu wasiwe na wasiwasi wowote,” alisema Ndimbo.


USAFIRI WA KUMWAGA

Kama kuna mashabiki walio na hofu kuhusiana na changamoto ya usafiri usiku huo, wanapaswa kuiondoa kutokana na mpango mahususi ulioandaliwa wa kuhakikisha uwepo wa mabasi ya kuwatoa Uwanja wa Benjamin Mkapa hadi katika maeneo wanayoishi kama ilivyothibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Tanzania (TADU), Jaeka Mdami.

“Usafiri utakuwepo hadi saa 5, 6 usiku. Tutawapeleka maeneo yote wakazi wa jiji la Dar es Salaam ambao watakuwepo uwanjani siku hiyo, utakuwepo pia usafiri wa kwenda Kibaha,” alisema Mdami.

“Hakuna kupandisha bei ya nauli kwani ile nauli iliyopangwa na serikali kutoka kwenye eneo moja kwenda jingine ndio itakuwa ikitumika hiyo hiyo kwa mashabiki baada ya mechi kwisha,” alisema Odilo.


REKODI MPYA

Ushindi kwa Simba katika mchezo huo utaifanya Simba iweke rekodi mpya ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika katika misimu miwili mfululizo tena kwenye mashindano mawili tofauti.

Msimu uliopita Simba ilitinga hatua hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ilikwama mbele ya Kaizer Chiefs baada ya kutolewa kwa kichapo cha jumla cha mabao 4-3.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa wamejipanga vyema kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi hiyo na ametoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.

“Tumehakikisha kwamba tunaweka mazingira salama, shabiki akija uwanjani kuangalia timu inaingia robo fainali anakuwa sawa kweli kweli. Nawakaribisha Wanasimba wote kuja uwanjani muda huo kuishangilia timu yao,” alisema Ahmed Ally.


MO AIBUKA KAMBINI

Wachezaji wa Simba jana walifanya kikao cha hamasa na Mwenyekiti wa heshima wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ na kumuahidi kwamba watapambana kupata ushindi. Mo alisema kwamba katika kikao hicho kifupi alikitumia kuwakumbusha wachezaji malengo ya mchezo huo kwa klabu na nchi. “Tumeongea ishu za bonasi, nimewaahidi bonasi kubwa kama tukishinda huu mchezo, nimewasisitiza umuhimu wa mchezo huu kwenye malengo ya klabu na wameniahidi matokeo mazuri. Niwaombe mashabiki kujitokeza kwa wingi kutoa sapoti kwa wachezaji, hii mechi muhimu sana kwetu kushinda,”alisema Mo. Mwanachama kindakin-daki wa Simba, Justine Joel kutoka tawi la Wekundu wa Terminal alisema, watu wanaipenda Simba yao, waje kwa wingi sana kuisapoti timu bila ya kujali muda.

“Simba ni yetu hatuna budi kuisapoti, iwe mvua iwe jua tumeipenda wenyewe na tutaenda kwa wingi kabisa, na hivi mfungo utakuwa umeanza tutafuturu nyumbani halafu taratibu kwa Mkapa, mechi ya kwanza kuchezwa saa nne usiku na tunaenda kuandika historia ya muda huo,” alisema Justine.

Shabiki Big Simba kutoka tawi la Chalinze alisema, wao hata mechi ikipangwa kuanza saa saba usiku wako tayari tu na wao mashabiki licha ya kutoka mkoani watakuja.

Mchezaji wa zamani wa Simba Boniface Pawasa alisema, ratiba ilikuja kwa sababu ya muda wa Morocco ambao RS Berkane watakuwa wenyeji wa ASEC Mimosas kutokana na wachezaji wao kuwa katika Mfungo wa Ramadhani.

“Morocco ndio wamesababisha haya, wao wamepewa feva kwa kuwa wanakuwa wamefunga, Simba wasitoke mchezoni wajielekeze kwenye mechi yao ili kufikia malengo ambayo wamejiwekea katika mchezo huo, naamini watafanya vizuri tu,” alisema Pawasa.

Kwa upande wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ofisa Habari, Clifford Ndimbo alisema, kwa kuwa ni utaratibu ulioletwa na CAF wao kama Shirikisho hawana budi kukubaliana na muda huo.

“CAF ndio wamepanga huo muda, hivyo sisi tutajipanga kwa ajili ya mchezo huo sio kitu kigeni, tuliwahi kucheza mechi ya Taifa Stars usiku, na hata za ligi zinachezwa usiku, hivyo tutakabiliana na huo muda, na hata kabla ya mchezo kunakuwepo na vikao vingi tu vya mchezo,” alisema Ndimbo ambaye pia ameteuliwa kuwa ofisa habari wa mchezo huo.


WASIKIE WAKONGWE

Mchezaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan alisema muda wa mchezo siyo tatizo bali wachezaji wanatakiwa kuonyesha ukomavu wao katika dakika zote tisini hilo ndio suala kubwa.

“Kwenye kikosi cha Simba hakuna mchezaji ambaye hajawahi kucheza usiku ila kilichokuwa tofauti hapo ni kutoka saa 2, kwenda saa 4, sioni kama kutakuwa na athari kubwa,” alisema Mgosi na kuongeza;

“Changamoto inaweza kuwa kwa mashabiki, ule wingi ambao ungefika uwanjani kama mechi ingechezwa saa 10 jioni au saa 1 usiku ni tofauti kabisa na watakaokuja muda huo, ila kikubwa ni jinsi gani wachezaji wanatakiwa kuonyesha ukomavu ili kushinda.”

Mchezaji wa zamani wa Simba, Amri Kiemba alisema kuna baadhi ya mashabiki wao kutoka katika mikoa ya jirani watashindwa kufika kutokana na changamoto ya muda wa kuanza mechi.

Kiemba alisema kwenye masuala ya kiufundi kuna namna inaweza kuwa tofauti kutoka kucheza mechi saa 1 usiku mpaka saa 4 usiku ila anaamini benchi la ufundi Simba litalifanyia kazi hilo walau kupata awamu mbili za kufanya mazoezi kwa muda huo.

“Hili la Simba ni kama kuzoea kucheza mechi saa 10 jioni halafu ukaambiwa ucheze saa 8 mchana, ila namna gani ukomavu kwa wachezaji wakubwa kama wa Simba wanatkiwa kuonyesha muda wote wa mchezo,” alisema Kiemba.


Imeandikwa na Charles Abel, Thobias Sebastian na Clezencia Tryphone